imetosha

imetosha

TAMKO: MTANDAO WA WANAWAKE NA KATIBA WAWAKUMBUSHA WAKUU WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU KUBEBA AJENDA YA USAWA WA JINSIA


http://1.bp.blogspot.com/-RqUnpocH3_M/VALjR3zRoKI/AAAAAAAGXvk/2dWGDyLTp78/s1600/PIX%2B16.JPG
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakifuatilia Semina iliyoandaliwa na Mtandao wa Wanawake na Katiba kwaajili ya Wajumbe wa Bunge Maalum kuhusu masuala ya Jinsia na Katiba iliyofanyika Agosti, 2014 kwenye Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa Mjini Dodoma.


Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania unaounganisha wanawake kutoka asasi za kiraia za nyanja mbali mbali za kisiasa, kijamii na kiuchumi, unatambua jitihada zote zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa katika kuhakikisha kwamba Katiba Mpya ya Tanzania inajengwa katika misingi ya usawa wa jinsia. Kwa mtazamo wa Mtandao, Katiba Pendekezwa imejengwa katika misingi inayotambua  ulinzi wa utu, heshima na haki za wanawake  na hivyo inahitaji kuthaminiwa na kulindwa na wahusika mbalimbali, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa nchini.  

Kwa mantiki hiyo ya kuhakikisha kwamba yaliyomo katika Katiba pendekezwa yanalindwa, Mtandao wa Wanawake na Katiba umekua ukifuatilia kwa makini mwenendo wa viongozi, na haswa viongozi wa vyama vya kisiasa katika matamko yao mbalimbali wanayoyatoa,  yakiwemo yale yanayohusu  mapendekezo ya kubadilisha sheria ya uchaguzi. 

Kwa mfano, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wamekuwa wakiikumbusha serikali kuzingatia katika mabadiliko ya Sheria mpya ya Uchaguzi, madai matano yakiwemo: Ushindi wa Mgombea Urais uwe wa kura za asilimia hamsini na zaidi, Nafasi ya Mgombea Binafsi itambuliwe, Tume Huru ya Uchaguzi iwepo na uwezekano wa kupinga matokeo ya uraisi mahakamani. 

Hata hivyo, matamko haya hayajumuishi kuingizwa kwa msingi wa usawa wa jinsia katika mabadilko ya Sheria yanayopendekezwa, pamoja na michakato mingine mbalimbali ya uchaguzi na matokeo yake. Mwenendo huu wa viongozi wa Vyama vya Siasa unatushangaza na kutuonyesha kuwa viongozi wengi wa kisiasa hawatilii maanani ajenda ya kuleta usawa wa jinsia katika uongozi wa nchi hii. Kwa maana hiyo, viongozi hawa wanaashiria  kutotambua mchango, nguvu, nafasi na haki wa mwanamke katika nyanja hii muhimu na hivyo kuduwazaa demokrasia na maendeleo ya nchi hii kwa ujumla.

Mtandao wa Wanawake na Katiba unawakumbusha na kuwataka viongozi hawa kutambua kwamba: 
·         Wanawake ni Zaidi ya asilimia 51% ya raia wa Tanzania ambao utawala wa nchi unawahusu.
·         Wengi wa wanachama wao ni wanawake, na hivyo wana nafasi kubwa ya kushawishi wananchi kutounga mkono itikadi, sera na mwenendo wa vyama vyao vya kisiasa;wanawake tumechoka kutumika na vyama vya siasa kama wapiga debe; wahamasishaji wa michangi ya vyama;
·         Wanawake ni idadi kubwa ya wapiga kura pamoja na watunzaji wakuu wa familia na amani ya nchi hii;
·         Vyama vya kisiasa visivyozingatia usawa wa jinsia na hivyo kuchochea sera za kibaguzi havina nafasi katika ujenzi wa taifa letu haswa kufuatia kukomaa kwa harakati za jinsia nchini
Hivyo basi, tunatoa rai kuwataka viongozi wa vyama vya kisiasa kuhakikisha wanazingatia yaliyomo katika Katiba pendekezwa na kuendelea kuyatetea huku wakihakikisha kwamba matamshi na sera za kibaguzi hazitavumuliwa.
# # #
Kama ungependa habari zaidi kuhusu mada hii, tafadhali wasiliana na TGNP ambao ni mojawapo wa wanachama wa mtandao kupitia +255754784050.


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

TUKISHIKA DOLA , SERIKALI ITAHAMIA DODOMA-ZITTO

 
CHAMA cha ACT Wazalendo, kimesema kama wananchi watakipa ridhaa ya kuongoza dola katika Uchaguzi Mkuu ujao, kitaunda Serikali na kuwaapisha viongozi wake katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ili kuhakikisha kuwa shughuli za Serikali zinahamia mkoani humo.

Kiongozi wa chama hicho, Bw. Zitto Kabwe aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Mashujaa, mkoani Dodoma na kuongeza kuwa, haiwezekani nchi ya Nigeria ifanikiwe kuhamisha Makao Makuu yake kutoka Lagos hadi Abuja; lakini Tanzania inashindwa.

Alisema ramani iliyotumika kujenga jiji la Abuja ndio iliyokuwa ya Tanzania, lakini Tanzania imeshindwa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kwenda Dodoma.

"CCM imewadanganya Watanzania kwa miaka mingi, Serikali inatumia gharama kubwa kuwalipa posho wafanyakazi wake kuja Dodoma ambako kuna ofisi zao na makazi yao.

"Katika orodha ya mikoa yenye maendeleo lakini inashika nafasi ya mikoa mitatu maskini ni pamoja na Dodoma ambao licha ya kuchangia pato la Taifa, inashangaza kuona kila Rais anapotakiwa aapishwe, huapisho huo hufanyika Dar es Salaam katika Uwanja wa Taifa," alisema Bw. Kabwe.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimeahidi kujenga zahanati  kwenye Kijiji cha Chidilo, Kata ya Chipanga, Tarafa ya Mpalanga Wilaya ya Bahi, mkoani humo ambayo hadi kufikia Juni mwaka huu, itakuwa imekamilika.

Akitoa ahadi hiyo, Bw. Kabwe alisema sababu ya kujenga zahanati hiyo ni kutokana na wananchi wa kijiji hicho kukiamini na kuchagua Mwenyekiti wa kijiji kupitia chama hicho.

"Tutajenga zahanati hii kama zawadi kwenu kwa kutuamini na  kumchagua Mwenyekiti wetu anayetokana na ACT, pia tutafuatilia fedha zote kwa viongozi wa halmashauri hii ambazo mlichanga ili mjenge zahanati," alisema Bw. Kabwe.

Alisema inashindikana kujenga maisha bora kwa kila Mtanzania kwa sababu uchumi wa nchi unamilikiwa na watu wachache ambapo Bw. Kabwe pia alisimikwa kuwa Chifu na Mtemi wa Kabila la Wagogo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bi. Anna Mghwira, alisema kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi ambapo mkoa huo ni moja kati ya mikoa yenye migogoro hiyo.

"ACT itahakikisha migogoro yote ya ardhi tunaikomesha mara moja bila kumuonea mtu haya," alisema Bi. Mghwira.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimevuna wanachama  2,071 katika mikoa minne ambayo viongozi wake wamefanya
ziara kwa mara ya kwanza tangu waingie madarakani.

Katibu  Uenezi na Mawasiliano, Msafiri Mtemelwa, alisema mkoani Ruvuma wamepata wanachama 528, Njombe 26, Makambako 103, Mafinga 228, Iringa 471, Morogoro 715  ambapo hadi kufikia jana, kimevuna zaidi ya wanachama 3,000.


CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

Ukiwa na tukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

NEWS ALERT: BASI LA PRINCES MUNAA LAPINDUKA MKOANI DODOMA LEO


 Kwa Hisani ya Michuzi Blog
 Muda mfupi uliopita, kumetokea ajali ya Basi la Princes Munaa lililokuwa likitokea Jijini Dar es Salaam kwenda Mwanza, katika kijiji cha Mtanana Kibaigwa Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma. Hakuna aliepoteza maisha katika ajali hii, watu kadhaa wamejeruhiwa.

SHULE YA SEKONDARI MPWAPWA YAFUNGWA KUTOKANA NA UKOSEFU WA CHAKULA


Mkoani Dodoma Shule ya Sekondari Mpwapwa iliyopo katika Wilaya ya Mpwapwa ilitakiwa kufunguliwa tangu Aprili 8, lakini imeshindikana kutokana na ukosefu wa chakula.
Akizungumza na MTANZANIA, mkuu wa shule hiyo, Nelson Mbilinyi, alisema walifunga shule kwa ajili ya likizo fupi, lakini hadi sasa hawajajua ni lini watafungua kutokana na tatizo hilo.
“Hadi sasa hatujajua tutafungua lini, lakini leo tuliambiwa kutakuwa na kikao na Ofisa Elimu wa Mkoa (REO) ndipo tutapata uhakika lini tutafungua shule,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato iliyopo katika Manispaa ya Dodoma, Mwasi Chibuni, alisema licha ya wanafunzi kuendelea na masomo, hali ya chakula si nzuri.
Alisema shule yao haijafungwa, lakini wanaendelea kuona chakula kitaishia wapi ndipo wachukue uamuzi.
“Sisi hatujafunga, tunaendelea hivyo hivyo tunajikongoja ila kama tukishindwa tutafunga,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, alipoulizwa kuhusu tatizo hilo la ukosefu wa chakula shuleni, alisema hana taarifa vizuri na kwamba atalisemea suala hilo leo atakapowasiliana na maofisa elimu kutoka wilaya zote.


CHANZO GAZETI LA MTANZANIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAKAZI WA DODOMA WAJITOKEZA KWA WINGI KATIKA SEMINA YA UJASIRIAMALI KUHUSU BIASHARA YA MTANDAO


Mfanyabiashara wa kimataifa na mjasiriamali aliyefanikiwa katika biashara ya mtandao dada Mariam Njemu alikuwa ni mmoja wa wazungumzaji waliotoa hamasa kubwa kwa umati wa wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani  uliojaa kupata mafunzo ya kuweza kutimiza ndoto zao kwa kufanya biashara hii iliyoaminika na kufanikisha kuwezesha kupatikana mamilionea wengi ndani na nje ya Tanzania Semina ilifanyika jumanne wiki hii katika hoteli ya Dodoma hotel


Wadau wakifuatilia kwa makini semina hiyo ambayo ilfanyika katika ukumbi wa dodoma  jumanne wiki hii na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na mikoa jirani


Mkurungezi wa MWANAHARAKATI MZALENDO MEDIA na  KAJO ITECH Ndg Krantz Mwantepele ambaye mtaalamu wa biashara ya mtandao na mhamasishaji wa mafanikio akipata taswira na mfanyabishara aliyefanikiwa kwa biashara hiyo toka mkoa wa Dodoma ndg Patrick komba  na mdau mwingine


Mfanyabiashara wa kimataifa na mjasiriamali aliyefanikiwa katika biashara ya mtandao dada Mariam Njemu alikuwa ni mmoja wa wazungumzaji waliotoa hamasa kubwa kwa umati wa wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani  uliojaa kupata mafunzo ya kuweza kutimiza ndoto zao kwa kufanya biashara hii iliyoaminika na kufanikisha kuwezesha kupatikana mamilionea wengi ndani na nje ya Tanzania


Mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani juzi jumanne tarehe 7 /04/2015  karume DAY walijitokeza kwa wingi kwa semina kuhusu biashara ya mtandao ambayo ni biashara ambayo ya karne ya 21 na kuendelea kukua kwa kasi duniani pia hapa nchini na kuwezesha kutengeneza mamilionea kwa wingi bila kujali kiwango chao cha elimu wala kipato na pia huanza kwa mtaji kidogo na bila mkopo toka benki.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SPIKA MAKINDA AITAKA SERIKALI KUKETI NA KUTOA TAMKO JUU YA KUWEPO KURA YA MAONI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkutano wa kumi na tisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano umemalizika usiku  wa manane huku Spika wa Bunge akiigiza Serikali na kamati ya bunge ya masuala ya sheria kuketi baada ya mapumziko ya sikukuu ya Pasaka na kutoa tamko kuhusiana na kuwepo au la kura ya maoni ya katiba pendekezwa na mwenendo wa uandikishaji wapiga kura katika mfumo mpya wa BVR.
Spika amesema ni vyema masuala hayo yakajulikana ili utata ambao unaendelea kulikabili Taifa kuhusiana na uwepo au la kwa kura hiyo ya maoni ya katiba pendekezwa ukamalizika na kuwafanya wananchi wakaweza kuendelea na mambo mengine. 
 
Katika hitimisho la mkutano huo waziri mkuu Mizengo Pinda amelieleza bunge kuhusiana na mustakabali wa muswada wa sheria ya kutambua maamuzi mahakama ya kadhi ambapo amesema Serikali imeamua kulirejesha suala hilo kwa wadau ili utata unaoendelea kuhusiana na muswada huo ukamalizika.
 
Bunge limeahirishwa mpaka tarehe 12 mwezi wa tano ambapo mkutano wa kumi na tisa ambao utakuwa ni wa bunge la bajeti  utaanza.
Chanzo:ITV

Jamii itoe ushirikiano kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini‏


Na. Johary Kachwamba - MAELEZO, DODOMA
JAMII imetakiwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi nchini katika kutoa taarifa zitakazo fanikisha kukamatwa kwa wote walioshiriki mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.


Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani  Mhe. Pereira Silima bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mhe. Al -Shaimaa Kwegyir, Mbunge wa Viti Maalum aliyehoji kuchelewa kwa taarifa ya kupatikana kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Pendo Emmanuel.


“Pendo alitekwa kutoka mikononi mwa mama yake mzazi, hii changamoto ni kubwa sana, tunaomba jamii itusaidie kutoa taarifa zitakazo saidia kufanikisha kukamatwa kwa wahusika, tushirikiane kwa pamoja kukomesha tatizo hili” alisema Mhe. Silima


“tangu kutekwa kwa mtoto Pendo watu 14 wanashikiliwa na jeshi la polisi akiwemo baba mzazi, uchunguzi bado unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani hivi karibuni, ila Pendo bado hajapatikana” aliongezea Mhe. Silima


Aidha akijibu Swali la msingi la Mhe. Salumu Barwany, Mbunge wa Lindi Mjini, aliyehoji idadi ya kesi za mauaji ya walemavu wa ngozi na sababu za kuchelewa kutolewa hukumu. Mhe. Silima alisema kesi 10 zinaendelea kisikilizwa mahakama mbalimbali


“kati ya mwaka 2006 hadi 2015 jumla ya matukio 56 ya uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa nchini. Matukio 41 yalihusisha vifo 43, matukio 13 yalihusisha majeruhi 13 na matukio 2 ya kupotea kwa watu wenye ulemavu wa ngozi” alifafanua Mhe. Silima


“kesi 46 kati ya matukio 56 zilifikishwa Mahakamani ambapo kesi 10 zenye watuhumiwa 12 zilitolewa hukumu ya kifo na kumi ziko chini ya upelelezi. Aidha kesi 26 watuhumiwa wake waliachiwa huru kwa kukosa ushahidi” aliongezea Mhe. Silima


Kuchelewa kwa hukumu au upelelezi wa baadhi ya kesi zilizotajwa kunachangiwa na sababu mbalimbali kama vile matokeo ya uchunguzi wa DNA toka Mamlaka ya Uchunguzi na/au mashahidi kutopatikana kwa urahisi na kwa wakati.    

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wananchi watakiwa kudai Risiti kwenye vituo vya Petroli na Dizeli‏Na. Johary Kachwamba - MAELEZO, DODOMA


Serikali  imewahimiza Wananchi kudai risiti pindi wanunuapo mafuta kwenye vituo vya kuuza Petroli na Dizeli ili kurahisisha ukusanyaji wa Kodi ya Mapato, Aidha kutokuchukua risiti ni kosa kisheria hivyo wote muuzaji na mnunuzi  wanastahili adhabu kwa mujibu wa sheria.


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba amesema hayo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Rukia Ahmad, Mbunge wa Viti Maalum aliyehoji kwanini Serikali isitoze kodi kwa jumla pale vituo hivyo vinaponunua mafuta

Mhe. Nchemba amesema ulipaji wa kodi ya mapato hususani kwa makampuni yanayouza mafuta unafuata mfumo wa wafanyabiashara kujikadiria wenyewe na kulipa kodi kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato sura 132, kisha ukaguzi wa hesabu kufuata baadaye.


“baada ya kubaini kuwa kuna udhaifu katika utoaji risiti ambao husababisha upotevu wa mapato, Serikali imeanzisha mfumo wa matumiz ya mashine ya kodi ya kielektroniki kwenye biashara mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo vya kuuza mafuta” Mhe. Nchemba
Hata hivyo mfumo wa matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki katika kutoa risiti za mauzo umetekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza iiwahusu wafanyabiashara waliosajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) wakati awamu ya pili inahusu wafanyabiashara wengine waliobaki


“vituo vingi vya mafuta nchini havijasajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kuwa mafuta ya Petroli na Dizeli hayatozwi kodi ya VAT” aliongezea Mhe. Nchemba


Kodi za Ushuru wa bidhaa, ushuru wa mafuta na ushuru wa Petroli hukusanywa Forodhani mara tu bidhaa hizi zinapoingizwa nchini, isipokuwa kwa mafuta ya Petroli na Dizeli yanayoenda nchi za jirani. Kodi hizi ulipwa forodhani na makampuni yanayoagiza mafuta ya Petrol na dizeli kwa kuzingatia kiasi cha ujazo wa lita zilizoingizwa nchini kabla ya kuuza kwenye vituo vya mafuta.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

PINDA AITWISHA MZIGO NEC

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema hatima ya upigaji wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa itatokana na tathmini itakayofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuona jinsi hatua hiyo ilivyotekelezwa katika Mkoa wa Njombe.
Pinda aliyasema hayo jana nje ya Ukumbi wa Bunge baada ya waandishi wa habari kutaka kujua msimamo wa serikali juu ya tarehe ya kupiga kura.
Alisema Serikali imekwisha kutoa asilimia 70 ya fedha za kununulia mashine 8,000 za Biometric Voters Registration (BVR) zitakazotumika katika uandikishaji huo.
Alisema uandikishaji nchi nzima unatarajiwa kuanza mapema Aprili na kila kata zitawekwa mashine mbili hadi tatu.
“Tukianza uandikishaji nchi nzima ndiyo tutaona changamoto zaidi zipo wapi na zinaweza kutupeleka katika uamuzi wa aina gani. Ila hilo litakuwa jukumu la tume (NEC), sisi kazi yetu ni kuhangaika BVR zinazotakiwa ziwe zimepatikana kwa wakati.
“Tume ndiyo inaweza kulizungumzia suala hilo kwa undani. Unajua inatakiwa mpaka kufikia Aprili 28 mambo yote yawe yamekamilika na siku mbili baadaye (Aprili 30) ndiyo siku ya kura. Kama wanasema mwezi mmoja ni sawa, tunaweza kuendelea na mambo mengine huku elimu ikitolewa kwa wananchi.
“Tulichojifunza ni kwamba katika maeneo ya mijini (Makambako na Njombe Mjini), tukianza uandikishaji nchi nzima ni lazima maeneo kama hayo tuyape nafasi kubwa zaidi tofauti na vijijini,” alisema.
Chanzo:Mtanzania

MWANDISHI ATAKAYEPOTOSHA JELA MIAKA MITATU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

agBUNGE limetuma salamu kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari kwa kupitisha Muswada wa Takwimu wa Mwaka 2013, ambao pamoja na mambo mengine unataka mwandishi atakayefanya makosa kwenye kuripoti taarifa za takwimu kufungwa jela miaka mitatu ama kutozwa faini ya Sh milioni 10.
Muswada huo umepitisha wakati ambapo, Machi 31, mwaka huu Serikali inatarajiwa kuwasilisha muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015 na ule wa Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015, yote kwa hati ya dharura.

Tayari wadau wa habari wameshapinga kuwasilishwa kwa miswada hiyo kwa hati ya dharura wakisema wanataka washirikishwe ili wajue kilichomo ndani yake.
Awali muswada wa takwimu uliwasilishwa kwenye mkutano wa 17 uliofanyika Novemba mwaka jana, ambapo baada ya wabunge kupinga vifungu vinavyobana waandishi, Serikali iliutoa bungeni kwa maelezo kuwa inaenda kuurekebisha.
Jana Bunge lilivyokaa kama kamati ili kupitisha muswada huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alihoji juu ya kifungu hicho kinachotoa adhabu kali na Serikali kusema imekifanyia marekebisho.
Hata hivyo, mbunge huyo alisema hakuna kilichofanyiwa marekebisho na kuwa adhabu bado inaendelea kuwa kali. Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), alihoji iweje Serikali iweke kinga kwa mtumishi wa Serikali anayetoa taarifa zisizo sahihi, lakini ikaacha kuweka kwa mwandishi anayepewa taarifa zisizo sahihi na ofisa huyo wa Serikali na kuziripoti.
Akijibu hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema “ataenda kujieleza mahakamani ama polisi”.
Kabla ya kuondolewa bungeni Novemba mwaka jana, muswada huo pamoja na mambo mengine, ulikuwa ukipedekeza faini ya Sh milioni 10 au adhabu isiyopungua kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa chombo cha habari kitakachotoa taarifa za kitakwimu za uongo au zenye upotoshaji.
Chanzo:Mtanzania
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa