Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
UMOJA wa Makanisa ya Kikristo mjini Dodoma, umekemea baadhi ya
viongozi wa serikali na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kumbeza
aliyekuwa Mwenyekiti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu,
Joseph Warioba.
Akiwasilisha tamko hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Makanisa ya
Kikristo, Askofu, Dk. Elia Mauza, alisema anayepaswa kulaumiwa si Jaji
Warioba bali Rais Jakaya Kikwete aliyemuamini na kumteua.
Alisema mwelekeo wa Bunge hilo unayumbishwa na wana siasa wanaojali masilahi yao.
“Kimsingi wanasiasa wanatupeleka pabaya, sisi Umoja wa Makanisa ya
Kikristo mjini hapa tunatoa tamko la kulaani mwenendo wa Bunge hilo
hasa kwa kumkejeli Jaji Warioba.
“Jaji Warioba na tume yake wamefanya kazi kubwa, hatuoni sababu ya
yeye kudhalilishwa kwa kumshambulia kwa maneno mengi, kama kuna sababu
ya kutoa lawama basi alaumiwe Rais Kikwete.
“Kikwete ndiye aliyeunda tume ya katiba na wakati akipokea rasimu ya
kwanza na ya pili aliisifia kwamba ni nzuri sana na aliipongeza tume
hiyo, je, kama kulikuwa na upungufu kwanini hakumkosoa tangu mwanzo ili
aurekebishe kabla ya kuutoa kwa Watanzania?” alihoji Dk. Mauza.
Dk. Mauza alisema ni fedheha kwa Bunge Maalumu kuacha kujadili
mchakato wa Katiba na kuelekeza mashambulizi kwa Jaji Warioba na tume
yake.
“Katiba si mali ya wanasiasa wala chama chochote cha siasa, katiba
ni mali ya wananchi na kinachotakiwa kujadiliwa na kuboreshwa ni kile
kilichopo ndani ya rasimu kwani hayo ndiyo mawazo ya Watanzania.
“Nasema katiba si mali ya wajumbe zaidi ya 600, bali ni ya
Watanzania zaidi ya milioni 45, hivyo watu wachache kukaa ndani ya
Bunge badala ya kujadili mambo ya kwenye rasimu na kuanza kujadili
mambo yao ni aibu kwa taifa,” alisema Askofu Dk. Mauza.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment