Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kuna tuhuma nzito kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilichakachua
takwimu za maoni ya wananchi ili tu kukidhi hoja ya muundo wa Serikali
tatu.
Ndiyo maana baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba wanamnyooshea kidole moja kwa moja aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume
hiyo, Jaji Joseph Warioba na wengine wakiilaumu tume kwa jumla wake.
Binafsi, sielewi msingi wa shutuma hizi kuelekezwa
moja kwa moja kwa Jaji Warioba ama Tume, wakati ilikuwa na watumishi wa
umma waandamizi ambao nao walishirikishwa katika Tume hii.
Hata Machi mwaka huu wakati akiwasilisha bungeni
Rasimu ya Katiba, Jaji Warioba alisema juu ya uwepo wa watumishi hawa
ambao kimsingi, ndio waliochambua na kuchakata maoni ya wananchi.
Jaji Warioba alisema: “Namshukuru Rais kwa
kuipatia Tume watumishi wa Sekretarieti walio makini, wenye ujuzi,
utaalamu na uelewa katika fani zao waliowezesha kukamilisha kazi yake
kwa ufanisi.”
Ni watumishi hao ambao walimfanya Jaji Warioba na
wenzake kusimama kifua mbele na kutoa takwimu za wananchi waliotoa maoni
yao Tanzania Bara na Zanzibar waliotaka Serikali tatu.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kati ya waliotoa maoni
yao kwa upande wa Zanzibar, asilimia 34 walitaka Serikali mbili,
asilimia 60 Serikali ya mkataba na asilimia 0.1 walipendekeza Serikali
moja.
Halikadhalika kwa upande wa Tanzania Bara,
asilimia 13 ya waliotoa maoni walitaka Serikali moja, asilimia 24
wakapendekeza muundo wa Serikali mbili na asilimia 60 wakataka Serikali
tatu.
Mbali na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
kutilia shaka takwimu hizo, hata Rais Kikwete mwenyewe, aliyeiteua Tume
hii haiamini.
Akihutubia Bunge Machi 21,2014, Rais Kikwete
anasema: “Wanasema pia kwamba mbona taarifa ya Tume yenyewe ukurasa wa
66 na 67 inaonyesha watu waliotoa maoni juu ya muungano ni 47,820”
“Kati ya hao ni watu 17,280 sawa na asilimia 37.2
ndio waliotaka Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili,
asilimia 29.8 wakataka Serikali ya mkataba na asilimia 7.7 wakataka
Serikali moja.”
Rais akahoji swali ambalo limekuwa ndiyo msingi wa
hoja za wajumbe wengi wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotoka CCM.
Aliuliza: “Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake
upi?”
Mbali na Rais Kikwete, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Benard Membe naye akaleta hoja kuwa Tume ya Jaji Warioba
italaaniwa kwa kuleta pendekezo la Serikali tatu.
Miongoni mwa wajumbe wa Tume hii wanaotuhumiwa
kuchakachua takwimu ni watu walioitumikia nchi kwa uadilifu mkubwa tena
wengine wakiwa ni wateule wa Rais.
Jaji Warioba aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa
kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jaji Agustino Ramadhan
aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania. Wote hawa hatuwaamini?
Katika kuilaumu Tume ya Jaji Warioba, si Rais
Kikwete, mawaziri wake wala wajumbe wa Bunge Maalumu wanaogusa uwepo wa
watumishi waandamizi wa Serikali ndani ya Tume hiyo.
Kama hata Rais hana imani na watumishi hawa
waandamizi wa Serikali walioisaidia Tume kuchambua takwimu, kwa nini
hawafukuzi kazi au kuwawajibisha kwa kukiuka maadili ya Utumishi wa
Umma?
Nauliza swali hili kwa sababu, tumeelezwa Tume hii
ilitumia karibu Sh70 bilioni za walipa kodi masikini wa Tanzania. Kama
ni kweli takwimu zina kasoro, Rais anasubiri nini kuwawajibisha?
Hebu tuamini kwamba takwimu hizo zimepikwa ili
kuhalalisha tu muundo wa Serikali tatu, tujiulize na Tume nyingine zote
zilizowahi kuja na mapendekezo ya muundo huo huo nazo zilipika takwimu?
Sasa kama takwimu hizi si sahihi, kwanini Rais
asitumie mamlaka yake akalivunja Bunge Maalumu la Katiba na kuunda Tume
nyingine kukusanya maoni? Kuna maswali mengi kuliko majibu.
Kinachoonekana hapa, Serikali ya CCM haina dhamira
ya dhati ya kuwaletea Watanzania katiba bora kwa vile mapendekezo ya
Serikali tatu hayaletwa leo wala jana. Ni wimbo usiopendwa na wakubwa.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment