Home » » KIKWETE-WAJUMBE WAACHE KASHFA

KIKWETE-WAJUMBE WAACHE KASHFA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS Jakaya Kikwete amewataka wabunge wa Bunge Maalum la Katiba, kuacha kuwakashifu waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume. Amesema yeye hatishwi na vijembe, wanavyotoa baadhi ya wabunge wa Bunge hilo. Lakini, ameonya waache kutoa vijembe vikali, alivyoviita “vya chini ya mkanda”, mfano kukashifu waasisi wa Taifa. Rais amesisitiza kuwa ana matumaini makubwa na mchakato wa Katiba mpya, unaoendelea na kwamba anafurahia jinsi mijadala, inavyoendeshwa bungeni.
“Mimi na-enjoy(furahia) sana debate (mjadala). Nataka waendelee kuzungumza kwa uhuru. Mtu akipata nafasi ya kusema, joto linapungua ” alisema Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam juzi, kwenye mahojiano maalum na TBC1, yaliyohudhuriwa pia na waandishi wa vyombo vingine.
Akifafanua kuhusu vijembe, alisema unaweza kukuta mjumbe anasema “Kikwete nchi imemshinda” au “CCM imeshindwa kutawala.” Alisema vijembe kama hivyo, havimpi taabu, kwa sababu hayo ni mawazo binafsi ya mjumbe, wakati kwa hali halisi yeye nchi haijamshinda wala CCM haijashindwa kuongoza.
“Lakini vijembe vingine vinapigwa chini ya mkanda, hivi siyo vizuri,” alisema Rais. Rais alisema wanaotumia lugha chafu (wanaopiga chini ya mkanda), wanakosa adabu na dunia ndiyo itawafundisha. “Si vizuri kuwashambulia waasisi wa Taifa kwa sababu wamefanya kazi kubwa. Kwa mfano Mzee Karume ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyowezesha Waafrika wa Zanzibar kujikomboa kutoka kwa utawala wa Sultan na Waarabu.
Mwalimu Nyerere ametuachia Taifa moja, lenye amani na utulivu, lenye makabila 120,” alisema. Rais alisema Mwenyekiti wa Bunge, Samwel Sitta amemhakikishia kuwa atampa kila mjumbe wa Bunge la Katiba, nafasi ya kuchangia mijadala na wale wasiosema, alisema atawaamsha waseme, ili wasije wakatoka na kudai hawakupewa nafasi.
“Mambo yanakwenda vizuri na hili ni jambo jema,” alisema Rais katika mahojiano hayo, ambayo yalichukua muda wa saa mbili. Aliongeza;“Kuna baadhi ya wajumbe wamekuwa wakinitumia meseji, juu ya lugha kali wanazotumia baadhi ya wabunge, na kuhoji huyu jamaa vipi, lakini mimi huwajibu kuwa hayo ni mawazo ya mtu binafsi, hiyo ni hulka ya mtu, muacheni aseme alivyofikiria yeye.”
Rais alisisitiza kinachosubiriwa na Watanzania wengi ni wabunge hao, kutengeneza Katiba itakayokubaliwa na wananchi wengi. Alitoa rai kwa wajumbe hao, wasome vizuri Rasimu ya Katiba mpya sura kwa sura, mstari kwa mstari na neno kwa neno, kuona dhana itakayofaa kwa jamii.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, uliopangwa kufanyika mwaka huu, alisema mwaka huu una mwingiliano na mchakato wa Katiba mpya, hivyo wataangalia suala hilo serikalini.
Mathalani, alisema baada ya Bunge Maalumu la Katiba kukamilisha kazi yake, kutakuwa na muda mwingine wa kura ya maoni, jambo litakaloathiri maandalizi ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa.
Kwa upande wa vyombo vya habari, Rais alisema Serikali imetoa uhuru mkubwa kwa vyombo vya habari nchini; na hakuna wakati wowote tangu Uhuru, ambapo nchi iliwahi kuwa na magazeti mengi, kama wakati huu.
Hata hivyo, Rais alionya kuwa uhuru huo, usiwe wa kuchochea, kubomoa nchi au kuingiza nchi kwenye machafuko. Alisema Serikali ndiyo yenye dhamana ya kulinda amani na usalama wa nchi, hivyo itachukua hatua kwa chombo chochote cha habari, kitakachofanya uchochezi, kubomoa nchi au kujaribu kutumbukiza nchi kwenye vurugu.
Ugomvi na marehemu Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela ameonya na kulaani kitendo cha wajumbe wa Ukawa kuwafananisha wajumbe wengine wa Bunge hilo na wauaji wa kundi la waasi la Intarahamwe lililoongoza mauaji ya kimbari nchini Rwanda.
Askofu Mtetemela pia alisema ukiona mtu anagombana na kumkosoa marehemu (waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume), anasababisha watu wajiulize maswali mengi kwa kuwa marehemu hana nguvu na mwenye uwezo wa kukosoa ubaya wa marehemu ni Mungu mwenyewe.
Mtetemela aliyasema hayo jana, bungeni alipokaribishwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kusema neno kuhusu hali inayoendelea katika mjadala huo baada ya Ukawa kususia Bunge na kutoka nje juzi.
“Ukiona mtu anagombana na marehemu, utajiuliza maswali mengi sana, unakashifu marehemu, asiye na nguvu ya kukujibu, ubaya wa marehemu mwenye uwezo kuukosoa ni Mungu mwenyewe, wewe ni nani, na una kipimo cha kiasi gani kukashifu kiongozi anayesifiwa duniani kote,” alisema Askofu huyo.
Akizungumza kwa masikitiko, Askofu Mtetemela ambaye ni mjumbe kupitia taasisi za dini kundi la 201, alisema, “Profesa Ibrahimu Lipumba, katika mchango wake jana (juzi) alilinganisha Bunge hili na Intarahamwe wa Rwanda, ni kauli nzito sana kwa mtu maarufu kama Lipumba kuchafua Bunge hili.”
“Intarahamwe ni wauaji, wajumbe wa Bunge hili hawawezi kulinganishwa na hao wauaji, kutuita sisi wauaji ni mbaya, inafufua maumivu ya ndugu zetu wa Rwanda ambao ni juzi tu walikumbuka mauaji yale mabaya ya kimbari, hakuna mtu anayetaka kuua mtu hapa,” alisema Askofu Mtetemela.
“Kwanini tutumie jambo la utata lililotokea kwa wenzetu, wakati tukiwa na tofauti fulani baina yetu na Rwanda? Hili linahitaji kukemewa, tena kwa kuwa limefanywa na kiongozi (Lipumba), angekuwa mtu mwingine tungesema haelewi,” alisema Askofu Mtetemela.
Chanzo:Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa