Home » » MACHALI,MNYIKA WABEZA WAWANAOENDELEA KUJADILI -KATIBA

MACHALI,MNYIKA WABEZA WAWANAOENDELEA KUJADILI -KATIBA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Dodoma. Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika na Mbunge wa Kasulu(NCCR-Mageuzi), Moses Machali, kwa nyakati tofauti wamesema mjadala unaoendelea bungeni bila kuwepo kundi la Ukawa, haliwezi kutoa Katiba Mpya.
Akizungumza juzi, Mnyika alisema Katiba lazima ipatikane kwa maridhiano hivyo busara ingetumika kutafuta utaratibu mwingine wa kuendelea na Bunge Maalumu badala ya kulazimisha mambo.
Alisema wamesusia Bunge hilo kwa sababu za msingi, moja kati ya sababu hizo anaitaja kuwa ni kulazimishwa kujadili masuala ya Serikali mbili, ilhali ni tofauti na mfumo unaopendekezwa kwenye rasimu ambayo ndiyo mwongozo wa mijadala hiyo.
Mnyika alisema wanaoendelea kujadili rasimu hiyo kwa lengo la kupata Katiba Mpya, wanapoteza muda na rasilimali kwa kuwa lazima kuwe na maridhiano ya pande mbili.
Naye Moses Machali alisema hawakukosea kususia Bunge hilo kwa kuwa lengo lao la kufikisha ujumbe limetimia. Pia hiyo ni sehemu ya kutekeleza malengo maalumu waliyojiwekea.
Machali aliongeza kusema kuwa Rasimu ya Katiba yenye muundo wa Serikali mbili inakihusu zaidi chama tawala (CCM), ndiyo maana wamekiachia chama hicho na washirika wake waendelee nayo.
“Tumejiridhisha, badala ya kujadili rasimu sura kwa sura, walilazimisha ianzwe sura ya kwanza na sita zinazohusu muundo ili wafumue muundo na kuweka wa Serikali mbili. Waendelee na Katiba yao ya CCM sisi hatuhusiki nayo,” alieleza Machali ambaye mara nyingi michango yake bungeni huonekana kuwa mwiba.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa