Home » » MIPASHO HAITATULETEA KATIBA MPYA

MIPASHO HAITATULETEA KATIBA MPYA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katuni
 
Watanzania  wapo katika fazaa kubwa kwa kile kinachoendelea katika Bunge Maalum la Katiba. Fazaa hii siyo ya bure ni matokeo ya mwenendo wa hali ya mambo ndani ya chombo hicho kilichotungwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 kwa nia ya kujadili rasimu ya katiba mpya kisha kuipitisha ili wananchi wakaipigie kura ya ama kuikubali au kukataa.
Ni Bunge Maalum la Katika kwa kazi maalum ya kutunga au kutengeneza katiba mpya ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania.

Huu ni wajibu mkubwa wenye kumgusa kila Mtanzania awe mtu mzima au mtoto, maamuzi ya Bunge hili yatamfunga kila raia wa nchi hii kuanzia mdogo, kijana hadi wazee.
Katiba ni makubaliano ya watu, katika mchakato wa sasa kinachotafutwa ni makubaliano ya Watanzania wote kwamba wamekubaliana kujitawala vipi, wamekubali kuweka utaratibu gani wa kutumia rasilimali zao, wanakubaliana viongozi wao wawe wa namna gani, wachaguliwe vipi, waongoze vipi na kwa muda upi.

Ndiyo maana kwa kutambua unyeti wa kazi za Bunge Maalum la Katiba umma unakubali na kuridhia kwa moyo mweupe kabisa gharama za kuwaweka wabunge Dodoma bila aina yoyote ya tashwishwi. Unakuwa hivyo kwa sababu kazi wanayoifanya wabunge hao inastahili gharama hizo.

Kwa bahati mbaya kwa kipindi kirefu sasa hali ya mijadala na majibizano ndani ya Bunge Maalum la Katiba haiakisi siha njema ya umakini na kina katika kushughulikia rasimu ya katiba.

Kinachoonekana kwa sasa ni kuhama kutoka hoja kuu ya mijadala kwenda kwenye mipasho, kejeli na hata mara nyingine lugha za kuudhi mno.
Imekuwa ni kawaida mjumbe kutumia rasilimali za umma kuongea vitu ambavyo kwanza havimsaidii mwananchi kuelewa mchakato husika unavyoendelea, lakini pia havisaidii hata Bunge hilo kupiga hatua kwa maana ya kutambua umuhimu wa vifungu mbalimbali vinavyopendekezwa kwenye katiba husika.

Kwa bahati mbaya sana wajumbe wa namna hii ndiyo walio wengi. Hawana kina katika kuichambua, kuielezea na kutoa suluhu mbadala kwa yale ambayo ama hayajakaa sawa katika rasimu ya katiba iliyo mbele ya Bunge kwa sasa. Ni bahati mbaya kweli kweli Bunge la Katiba limegeuzwa kuwa uwanja mwingine wa hadhara wa kisiasa licha ya ukweli kwamba kuna kanuni zinazoongoza chombo hiki muhimu cha kuwaletea Watanzania katiba mpya.

Jumatano wiki hii kundi la wabunge linalounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka vyama vya Chadema, Cuf na NCCR-Mageuzi wakiwamo pia wa baadhi ya vyama vingine na wale wa kundi la wajumbe 201 kutoka makundi mengine, waliamua kususia kikao cha jioni wakieleza kuchoshwa na hali waliosema ‘ubaguzi’ na nia ya kutaka kuvuruga maoni ya wananchi ambayo yalizingatiwa kwenye rasimu ya katiba mpya ambayo ipo mbele ya Bunge kwa mjadala.

Siyo nia yetu kusema kususia kwao kikao hiyo Jumatano jioni ilikuwa sahihi au la, hata hivyo itoshe tu kusema kuwa hatua hii ya kususa inazidi kushindilia msumari wa moto juu ya fazaa ya wananchi kwamba huenda katiba mpya isipatikane kama ambavyo ilikuwa imepangwa kwamba mwaka huu Tanzania itapata katiba mpya.

Wapo wanaodhani kwamba kutoka kwa Ukawa na wale wanaowaunga mkono ni upuuzi na hakuna maana kwani mjadala wa katiba mpya unaendelea bila wasiwasi kwa kuwa wapo wajumbe kutoka makundi mbalimbali mengine wakiwamo wa vyama vya siasa ambavyo havina wabunge.

Kadhalika, wapo wanaobeza kuwa kinachowasumbua Ukawa ni posho tu, na kwamba baada ya kuipata wameamua kutoka bungeni, na kwamba hawana nia njema yoyote na katiba mpya.

Inawezekana wote wanaoeleza haya wanajua wamejiegemeza wapi na dhana au nadharia zao, lakini sisi tungependa kutoa angalizo moja muhimu kwamba katika mchakato wa katiba wa sasa kila mjumbe kwenye Bunge Maalum la Katiba ni sehemu muhimu katika maamuzi ili katiba itakayotoka hapo ipate uhalali mbele ya umma.

Hata kama Bunge kwa sasa limegawanyika katika misimamo isiyoshikamana ya ama serikali mbili au tatu, bado mgawanyiko huo hauwezi kuwa sababu ya wabunge kushindwa kuongozwa kwa moyo wa kuipenda nchi yao, kujizuia kutoa lugha za kuudhi na kukejeli dhidi ya wengine.

Tinafikiri ni vema na haki kabisa katika muktadha wa haya tunayozungumzia hapa ieleweke kwamba hata kama itafikia mwisho kwamba katiba mpya imeshindikana kupatikana, bado Tanzania kama nchi na watu wake wataendelea kuwako. Kwa maana hiyo siyo busara kuanza kupalilia moto wa uhasama kwa kushindwa tu kuheshimiana.

Kila mbunge ana wajibu wa kujizua kumuudhi mwenzake, ana wajibu wa kuisoma rasimu ya katiba mpya na kuchangia kuiboresha kwa uaminifu au kama wasemavyo Waingereza constructively. Tunaamini vijembe, mipasho na vituko vingine kama hivyo haitatupa katiba mpya.

Tunaungana na wito wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, kwa wabunge wote alioutoa Jumatano jioni wakati akiwasilisha hoja ya kuahirishwa kwa Bunge, kwamba ni vema sasa mipasho ikawekwa pembeni. Kwa hakika mipasho, kejeli na lugha nyingine zisizo za staha vinavuruga Bunge Maalum la Katiba, ni aibu.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa