Home » » SITTA AIFUTA UKAWA Z'BAR

SITTA AIFUTA UKAWA Z'BAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta akimpatia taarifa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  Dk Ali Mohammed Shein juu ya mwenendo Bunge hilo na ulipofikia alipomtembelea Ikulu ya Migombani Zanzibar.

Wakati viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiweka kambi Zanzibar, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta jana naye alitumia siku nzima visiwani humo akikutana na baadhi ya viongozi wa Serikali, katika kile kinachotafsiriwa kuwa kulinusuru Bunge hilo.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka Zanzibar zinasema Sitta alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Rais Mstaafu, Aman Karume na mwanasiasa wa siku nyingi wa CCM, Mzee Hassan Nassor Moyo.
Zanzibar kwa sasa ndiyo moyo wa upatikanaji wa Katiba Mpya kutokana na wajumbe wake katika Bunge kutegemewa ama kuipitisha au kuikwamisha kwa kuwa kila upande kati ya mbili zinazovutana, hauna uhakika wa kupata theluthi mbili za kura.
Baada ya kuondoka bungeni na kutangaza kususia vikao vya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, siku mbili baadaye viongozi wa Ukawa waliingia Zanzibar wakitaka kufanya mikutano ya hadhara kuwaeleza wananchi sababu za kufanya hivyo, lakini wakazuiwa na polisi na hadi jana walikuwa wanasubiri kibali.
Safari ya Sitta
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad pamoja na kuthibitisha ziara ya Sitta Zanzibar kuwa alikuwa akutane na Dk Shein, alisema hafahamu lolote kuhusu mkutano wake na Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF.
“Sifahamu malengo ya safari wala walichokwenda kuzungumza, ila ni kweli kwamba alifika Zanzibar leo (jana) na alitarajiwa kuondoka jioni kurejea Dodoma,” alisema Hamad na kuongeza:
“Hilo la kuonana na Maalim Seif silifahamu ila ninachojua aliniambia nimfanyie miadi ya kuonana na Dk Shein na nikaifanya kama alivyoelekeza.”
Mapema habari zilizolifikia gazeti hili kutoka Zanzibar zilisema, Sitta baada ya kukutana na Karume, Shein na Mzee Moyo alitarajiwa kukutana na Maalim Seif saa 9:00 alasiri.
Katibu wa Maalim Seif, Issa Kheri Hussein alithibitisha kwamba Sitta alikutana na kiongozi huyo nyumbani kwake, Mbweni saa 9:30 alasiri jana, lakini alidai kutokuwa na taarifa za mazungumzo hayo.
“Hilo naweza kulithibitisha kwamba mkutano huo umefanyika lakini mazungumzo yenyewe yalikuwa ya faragha na mimi baada ya Sitta kufika niliondoka, hivyo sikuweza kufahamu kilichozungumzwa kwa undani, pengine mpaka nizungumze na Maalim mwenyewe,” alisema Hussein.
Ziara ya Sitta kwenda Zanzibar imekuja wakati ambao kumekuwa na wasiwasi mkubwa wa kukwama kwa vikao vya Bunge hilo kutokana na msimamo wa Ukawa.
Leo vikao vya Bunge hilo vinatarajiwa kuendelea mjini Dodoma bila wajumbe wa Ukawa ambao viongozi wake wamesisitiza kwamba hawatarudi hadi pale watakaporidhika kwamba kuna utashi wa kweli wa kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Ukawa unaundwa na wajumbe wapatao 200 kutoka vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, NLD, DP na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la 201.
Viongozi wa Ukawa
Viongozi wa Ukawa kwa nyakati tofauti walisema wamesikia kuhusu safari ya Sitta kwenda Zanzibar lakini hawakuwa na taarifa za ndani kuhusu mazungumzo yake na Maalim Seif.
Hata hivyo, walisema hata kama amekwenda kwa lengo la kupata suluhu, hawezi kufanikiwa pasipo kuwashirikisha.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Inawezekana kweli Sitta ataonana na Maalim Seif, lakini lazima afahamu kwamba kurejea kwetu katika Bunge lazima uwe uamuzi wa chama ambacho mimi ni mwenyekiti wake na Maalim ni Katibu Mkuu.”
“Kwa hiyo uamuzi wetu wa kuondoka pale bungeni ulikuwa ni uamuzi wa kichama, maana mimi kama mwenyekiti wa CUF niko katika Bunge hilo na tulishauriana na wabunge pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi lakini zaidi ya hapo tuna makubaliano na wenzetu katika Ukawa,” alisema.
Alisema Ukawa wataweza kurejea katika Bunge kwa sharti moja kubwa kwamba lazima rasimu itakayojadiliwa iwe ni ile inayotokana na kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
“Kinachoonekana pale bungeni ni kwamba wapo watu wanataka kutushirikisha sisi tujadili rasimu yao wanayotaka kuileta kwa njia wanazozijua wao, hilo hatutalikubali, kwa hiyo mazungumzo yoyote lazima yawe na lengo,” alisema.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye pia ni mjumbe katika Bunge hilo alisema: “Sisi msimamo wetu uko wazi, kwa sababu CCM wameonyesha msimamo mkali kuhusu kile wanachokitaka, wanataka kutumia wingi wao basi tumewaachia waendelee kwani tatizo liko wapi? Mimi sioni kwa nini wanahangaika wakati uwezo wa kupitisha Katiba wanayoitaka wanao.”
Aliungana na Profesa Lipumba kwamba hakuna maridhiano yatakayofanywa nje ya Ukawa na kwamba hata kama Sitta amekutana na Maalim Seif, tayari walishakubaliana kuwa na msimamo wa pamoja katika suala hilo la Katiba.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia mbali na kusema amesikia kuhusu ziara ya Sitta Zanzibar, alisisitiza kwamba utashi wa kisiasa ndiyo utakaoiokoa Katiba Mpya.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa