Home » » UKAWA WAKANA KUSAINI POSHO KINYEMELA

UKAWA WAKANA KUSAINI POSHO KINYEMELA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mmoja wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),Moses Machali
 
Mmoja  wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Moses Machali, amesema hakuna mjumbe yeyote wa umoja huo aliyerejea katika Ofisi za Bunge kwa ajili ya kudai au kuchukua posho za vikao vya Bunge.

 Aidha, alisema kwa upande wake iwapo itagundulika amelipwa posho za vikao hivyo toka siku waliyotoka bungeni, yupo tayari kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge wa Jimbo la Kasulu Mjini.

Kauli hiyo ya Machali imekuja baada ya baadhi ya wajumbe wa bunge Maalum la Katiba kudai kwamba wajumbe hao wa Ukawa wanalipwa posho wakati hawahudhurii vikao vya Bunge.

Alisema posho za mwisho kuchukuliwa na wajumbe hao wa Ukawa zilikuwa ni siku ambayo walitoka bungeni na hakuna posho nyingine iliyochukuwa na Ukawa.

“Huu ni upotoshaji wa makusudi unaofanywa na Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya Ukawa kwamba wajumbe wa Ukawa tumerudi bungeni kuchukua posho,” alisema.

Machali alisema jambo hilo si la kweli na kuwahakikishia Watanzania kwamba hakuna mwana-Ukawa aliyerejea katika ofisi za Bunge kwa ajili ya kudai wala kuchukua posho.

“Kauli ya upotoshaji kama hii ni dalili za CCM na vibaraka wao kukosa hoja za kujibu hoja nzito za Ukawa zilizowasilishwa ndani ya Bunge Maalum zilizohusu Muungano wetu,” alisema na kuongeza:

“Mara baada ya Ukawa kutoka baadhi ya CCM walisema kwama Ukawa wamechukua posho za hadi Aprili 30 na kukimbia, lakini pia ikasema tena ndani ya Bunge kuwa Ukawa warudishe fedha za wananchi walizochukua…hii ni dalili ya kushindwa kuwa na hoja na kuamua kuwachafua wajumbe wa Ukawa.”

Alisema Ukawa hawawezi kukaa na kujadili Rasimu na watu waliopoteza muelekea hadi watakapojisahihisha na kuheshimu maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Maajabu CCM wamekalia mipasho na kutaka Ukawa tukae na watu waliopoteza muelekeo katika mchakato huu wa kupata Katiba mpya…Ukawa ni watu makini na tusiokurupuka,” alisema

Kuhusu Ukawa kutumika na mataifa ya nje, alisema kamwe umoja huo hauwezi kushawishiwa na taifa lolote na hawataacha kutetea maoni ya Watanzania kwani ndiyo msingi na utawala wa kidemokrasia na maoni yaliyowasilishwa na tume hiyo.

“CCM na vibaraka wao wanataka kuwafanya Ukawa washindwe kusimamia maoni ya wananchi na badala yake Ukawa tuendelee kujadili mambo mengine,” alisema.

Akizungumzia tuhuma kuwa Ukawa kuwatukana waasisi wa taifa, alisema Ukawa hawajamtukana muasisi yeyote Muungano.

Alisema baadhi ya wajumbe wa Ukawa hajakutukana bali walikosoa dosari au mapungufu ya Muungano wa taifa hili katika kuanzishwa kwake.

“Ukawa ni watu makini, lakini mimi kama mwana-Ukawa naweza kumkosoa mtu yeyote yule wakiwamo waasisi wa Muungano wetu kwa yale waliyoyafanya na sitakiwi kutafsiriwa kuwa nimetukana kwa kuwa kuna tofauti kubwa katika ya kukosoa na kutukana viongozi au mtu mwingine yeyote,” alisema.
 
TANZANIA KWANZA YAWAITA
Wakati huo huo, Tanzania Kwanza wamewashauri wajumbe wa Ukawa waliotoka nje warudi bungeni kwani kazi ya kupata Katiba inayopendekezwa inafanywa katika bunge maalum la siyo katika viwanja vya mikutano.

“Muda wa kuendelea kususia machakato huu haujafika kufanya hivyo ni kwanyima wananchi wanaowawakilisha, ambao wanamatumaini makubwa ya kupata katiba iliyo bora,” alisema mwenyekiti wa Tanzania Kwanza, Said Mkumba.

Aidha waliwaomba wananchi wawe watulivu, watafakari, wasiyumbishwe, wapime na kuchambua matukio na wafanye maamuzi sahihi kwa manufaa yao na ya nchi yao.

Waliwaeleza Watanzania kwamba pamoja na wajumbe wachache kuondoka, akidi bado imetimia na shughuli za bunge hilo zinaendelea.

“Kwa umoja wetu tutatetea maslahi ya wafugaji, wakulima, wachimbaji wadogowadogo, wajasiriamali, watu wenye ulemavu, wanawake, vijana, wazee na watoto na makundi yote," walisema katika taarifa yao iliyosomwa na Mkumba, aliyeongozana na wajumbe kadhaa wakiwamo Adam Malima, Dk. Emmanuel Nchimbi, Paul Makonda na Evodius Mmanda.

Hata hivyo, walipoulizwa kwa nini wasimuite mjumbe yeyote wa Tume ya Jaji Warioba ili kutoa ufafanuzi wa takwimu ambazo wanazilalamikia kwamba zilichakachuliwa kama sheria inavyosema, Dk. Nchimbi, alisema hakuna sababu ya kuwaita kwa kuwa tume imeshavunjwa kisheria baada ya kukamilisha kazi yake.

MISA YA KUOMBEA KATIBA
Wakati huo huo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma Mhashamu Gervas Nyaisonga, ameshauri wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuendeleza uvumilivu na kuwa na moyo mkuu  wakati wanapoandika katiba.

Alisema kazi ya kuandika katiba ni ngumu, lakini wajipe moyo hadi  itakapokamilika na kufanyakazi hiyo kwa upendo wakiepuka kuweka mbele maslahi yao.

Alimuomba Mungu awajalie hekima na busara na hekima katika kutafuta yaliyo mema kwa taifa na mustakabali wake

Mhashamu Nyaisonga alisema hayo wakati alipoongoza ibada ya kuliombea Bunge Maalumu la Katiba na kulibariki jengo la bunge jana mjini Dodoma.

Katika ibada hiyo alisambaza pia sala maalumu ya kuliombea Bunge hilo maalumu iliyoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na kusainiwa na Rais wake Mhashamu  Tarcisius Ngalalekumtwa.

Juzi Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad, alisema  baadhi ya wajumbe wa Ukawa waliosusia Bunge wiki iliyopita, wamejaza kinyemela fomu za malipo ya posho za vikao, ambavyo hawajashiriki

Yahya alisema juzi walitangaza wajumbe wajaze fomu kwa ajili ya malipo yao na inavyoonekana baadhi ya wajumbe wa Ukawa, kwa kujua wahasibu hawawafahamu wapo upande gani, walichukua fomu hizo na kuzijaza.

“Kabla ya malipo yoyote, utaratibu wetu ni lazima wajumbe wajaze fomu za malipo, jana (juzi) tulitangaza wajumbe wajaze fomu kwa ajili ya malipo, Ukawa nao waliingia na kuna fomu walijaza, nimechukua orodha ya majina kuangalia waliohudhuria,” alisema Yahya.

Aliongeza: “Nimeagiza leo (juzi) asubuhi fomu zote niletewe, ambaye hakuwapo ndani hata kama si Ukawa ataeleza alikuwa wapi, kama hakuwa ndani hatutamlipa mpaka Mwenyekiti (Sitta) aidhinishe kwamba muhusika alikuwa na dharura ya muhimu akiwa Dodoma ndio atalipwa,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa