Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAKAZI wa Mlimwa C mjini Dodoma, wamepinga uamuzi wa Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuwaamuru wabomoe nyumba zao bila
kuwalipa fidia.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumatano, walielezea
masikitiko yao kwa kuitwa wavamizi kwenye eneo wanaloishi kihalali,
huku wakisema hawana tatizo la kuhamishwa ila wanachohitaji ni CDA
kuwalipa fidia kabla ya kuwahamisha.
Wamemlalamikia pia mwekezaji wa hoteli ya Africa Dream na kudai kuwa
anawasababishia tabu kwa kuwahonga watendaji wa mamlaka na mwenyekiti
wa mtaa huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa CDA, Pascas Mulagili, akijibu tuhuma hizo,
alisema wakati wanaanza zoezi la kuwatambua wavamizi walikubaliana
mambo makuu matatu.
“Katika kuhalalisha ukaazi wao moja ilikuwa wakazi wote wa eneo hili
ni wavamizi, pili tulikubaliana kuwapimia maeneo hayo na tatu
tulikubaliana kuwa wananchi watakaojikuta wako wawili kwenye sehemu
moja itabidi mmoja aondoke na hatalipwa fidia.
“Mambo yote matatu yaliyokuwa msingi wa kuamua kupima eneo husika
yaliafikiwa, nawashangaa wanaoibuka kwa hoja ya kulipwa fidia jambo
ambalo halikuwa makubaliano ya awali,” alisema mkurugenzi huyo.
Kwa mujibu wa Mulagili walichokifanya ni kutambua mipaka ya ile
barabara na kuwawekea X na kuwapelekea taarifa ya kwamba wanatakiwa
kuvunja nyumba zao na kupisha barabara.
Alisema baada ya wananchi hao kuona hali hiyo, waliamua kukimbilia
mahakamani hatua ambayo mamlaka iliiona ni nzuri kwa kuwa wamekwenda
kwenye chombo kinachosimamia sheria, kesi ambayo ilichukua zaidi ya
miaka miwili.
Mulagili alisema muda waliowapa kimsingi umekwisha na hivi sasa
wanajipanga kwenda kuwaondoa huku akisisitiza kwamba anatoa rai kwa
wananchi wote wenye nyumba barabarani waondoke bila kusubiri matumizi
ya nguvu ili kuwaondoa.
Alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
inaendelea na zoezi la uchunguzi ili kuwabaini watu waliohusika na
tuhuma za rushwa katika zoezi la ugawaji wa viwanja ambalo lilisimamiwa
na uongozi wa serikali ya eneo husika na kuwachukulia hatua za
kisheria.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment