Home » » BAADA YA TIBAIJUKA,CHADEMA YAMGEUKIA ZITTO

BAADA YA TIBAIJUKA,CHADEMA YAMGEUKIA ZITTO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Joseph Mbilinyi
 
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), jana alilipuliwa bungeni akidaiwa kuchota zaidi ya Sh. milioni 119 kwa kutumia kampuni mbili zinazodaiwa kuwa yeye ni Mkurugenzi wake.
Fedha hizo zinadaiwa kutolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Shutuma hizo zilitolewa bungeni jana ikiwa ni siku moja baada ya kambi hiyo, kumshutumu kwa ‘ufisadi’ Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi, alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), ifanye uchunguzi kuhusiana na malipo na matumizi husika kwa kurejea masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na sheria nyingine zinazohusika.

Pia, kambi hiyo imemtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na Tanapa na NSSF, msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi yake kwa kuzingatia masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika kusimamia matumizi ya fedha za umma.

Kwa mujibu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto anatuhumiwa kuwa na maslahi na kampuni mbili za Leka Dutigite Limited na Gombe Advisors Limited.

Mbilinyi, ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), alifafanua kuwa kampuni ya Leka Dutigite ilipewa usajili wake na Wakala wa Usajili wa kampuni na Leseni (Brela) Agosti 13, mwaka 2012 na kwamba ofisi zake ziko katika jengo la City House lililoko kwenye mtaa wa Mkwepu jijini Dar es Salaam.

Alisema mwenye hisa nyingi katika kampuni hiyo ya Dutigite ni kampuni ya Gombe Advisors ya jijini Dar es Salaam ni Zitto.

Mbilinyi alisema Kambi ya Upinzani inazo taarifa kwamba Desemba 10, mwaka 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani inayomilikiwa na Tanapa na hivyo ni shirika la umma, ilihamisha jumla ya Sh. milioni 12.2 kwenda katika akaunti namba 0150357447800 iliyoko Benki ya CRDB tawi la Pugu Road, Dar es Salaam inayomilikiwa na Leka Dutigite Limited, lakini siku moja baadaye, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo.

Aidha, alisema kati ya Januari 14 na Februari 7, mwaka 2013, akaunti ya Leka Dutigite, iliingiziwa jumla ya Sh. milioni 28.6 kama fedha taslim na anayeitwa Mchange (Sh. milioni 3.6 Januari 14, mwaka 2013) na Leka Dutigite (Sh. milioni 25 Januari 23 na Februari 7, mwaka 20130.

Hata hivyo, Mbilinyi alisema kufikia Januari 7, mwaka 2013, fedha zote hizo zilikwisha tolewa benki.

Vile vile, alisema Februari 28, mwaka 2013, akaunti ya Leka Dugitite Limited, iliingiziwa Sh. milioni 32.367 na NSSF."Kwa mujibu wa taarifa za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo," alisema.

Kadhalika, alisema Machi 4, mwaka 2013, NSSF ilifanya malipo mengine kwenye akaunti ya Leka Dutigite Ltd kwa mikupuo miwili ya jumla ya Sh. 46,663,000 na siku hiyo hiyo fedha hizo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo  kwa mikupuo miwili.

"Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu kati ya tarehe 10, Desemba, 2012 na Machi 4, 2013, Leka Dutigite Ltd, ililipwa Sh. 119,930,000 kwa utaratibu huo huo wa ingiza toa fasta," alisema.

Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, Sh. 79,027,000 zililipwa na NSSF na Sh. 12,200,000 zililipwa na Tanapa.

"Ukweli ni kwamba, kwa upande wa malipo yaliyofanywa na Tanapa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Bunge lako tukufu, imepata nakala ya mkataba unaohusu maandalizi ya filamu  kwa ajili ya kuhamasisha shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya  Saadani  kwa kutumia wasanii kutoka Kigoma," alisema.

Kwa mujibu wa Mbilinyi, mktaba huo ulisainiwa Desemba 5, mwaka 2012 kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Leka Dutegite Ltd  na una thamani ya Sh. 12,200,000, ikiwa ni kiasi kile kile kilicholipwa  na hifadhi hiyo.

Aliongeza kuwa kwa maana hiyo, Zitto kwa kutumia kampuni zake za Leka Dutigite Ltd na Gombe Advisors Ltd, amefanya biashara na Tanapa, shirika la umma analolisimamia kama Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha (PAC).

Alisema kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge, moja ya majukumu ya PAC, ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika wizara na mashirika ya umma yaliyoainishwa katika taarifa ya CAG.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa