Home » » BAJETI YA KILIMO 'CHUPUCHUPU' KUKWAMA

BAJETI YA KILIMO 'CHUPUCHUPU' KUKWAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imepita kwa kusuasua baada ya wabunge wanane kutishia na kujaribu kuiondoa shilingi katika mshahara wa waziri.
Bajeti hiyo, ambayo ilisomwa na kupitishwa juzi, ilikutana pia na kauli za kutaka Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza ajiuzulu kwa madai kuwa ni mzigo na ameshindwa kuiendesha wizara hiyo.
Ilibidi Chizza afanye kazi ya ziada kujieleza baada ya mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage kutishia kuondoa shilingi kutokana na tatizo la ugonjwa wa migomba, unaojulikana kama mnyauko, kutotatuliwa.
“Nasikitika Serikali haikunielewa nilichosema kuwa sasa Kagera kuna njaa. Haikunielewa kinachopaswa kufanyika kwa sababu huu ni ugonjwa unatokana na mgusano,” alisema Mwijage, hoja iliungwa mkono pia na mbunge wa Viti Maalumu, Benadeta Mshashu (CCM).
Kutokana na mabishano hayo, mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alimtaka Waziri Chizza kukubali kupeleka chakula ili shilingi yake ibaki akatumie na mkewe, jambo alilokubali.
Moto mwingine uliwashwa na mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) aliyeondoa shilingi baada ya kushikilia msimamo wake wa kutaka Serikali kukaa na wadau wa kilimo na kutafuta njia ya kuondoa ubadhilifu katika pembejeo.
Uamuzi huo uliungwa mkono na mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) aliyesema kutengeneza mfumo ambao unamlazimisha mkulima kuwa mwanachama wa chama cha ushirika ili apate mkopo, ni kutengeneza chujio kwa wakulima katika suala la upatikanaji wa pembejeo.
Hata hivyo, Chizza alisema si wakulima wote waliokuwa wanapata ruzuku ya pembejeo katika utaratibu uliopita.
Hoja ya kuondoa shilingi ilishindikana kupita baada ya Zungu kuwahoji wabunge.
Wengine waliotishia kuondoa shilingi walikuwa ni pamoja na mbunge wa Lindi Mjini Salum Barwany (CUF), na wa Bariadi Mashariki John Cheyo, (UDP) ambaye alitaka kuruhusiwa kwa wafanyabiashara wote kununua pamba.
Hoja ya Cheyo iliungwa mkono na mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema) na mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi).
Hata hivyo, kulitokea malumbano mengine juu ya muda watakaokutana wadau na Serikali baada ya Cheyo kutaka Chizza kutamka siku hiyo bungeni.

Kauli hiyo ilizua minong’ono na kumfanya, Samuel Sitta, ambaye alikuwa anakaimu nafasi ya usimamizi wa shughuli za serikali bungeni, kusimama na kusema hakuna haja ya kuvutana kuhusu jambo hilo wakati wakulima wakisubiri majibu.
Alimtaka Chizza kukutana na wadau wa pamba kati ya leo na kesho ili kulimaliza tatizo hilo.
Bajeti kutokwenda katika Kamati
Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul alitaka bajeti hiyo ya kilimo irudi katika Kamati ya Bajeti ili fedha zilizopangwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinazotokana na vyanzo vya ndani ziongezwe ili ziweze kujibu matatizo ya wakulima.
Hoja ya kuondoa shilingi katika mshahara wa waziri endapo bajeti hiyo haitapelekwa katika kamati kufanyiwa marekebisho, iliungwa mkono na mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), Mnyika na Machali.Akijibu Chizza alisema miongoni mwa fedha zilizolalamikiwa kutengwa katika maeneo yasiyomnufaisha mkulima, ikiwamo za watoa huduma Sh1.4 bilioni, ni muhimu katika kuwasaidia wakulima kupata elimu.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema kamati ya bajeti ilishakaa na kuipitia bajeti hiyo.
“Kwenye kamati tuna wabunge wa Chadema, labda kama wametuma wabunge wenye akili ndogo.
“Kabla ya kuwasilisha bajeti ya kila wizara, lazima iwe imeipitiwa na Kamati ya Bajeti,” alisema na kuongeza kuna wizara nyingine ambazo Kamati ya Bajeti imeshika shati sasa hivi na wanazijua .
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa