Home » » BAJETI ZA MAJI,NISHATI ZAIVURUGA SERIKALI

BAJETI ZA MAJI,NISHATI ZAIVURUGA SERIKALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma jana.

Wakati Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika akisema atamwandikia barua Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe akimtaka kutowasilisha bajeti yake leo, akidai ina kasoro nyingi, Serikali imenyoosha mikono na kuamua kuisogeza mbele kwa hofu ya kukwamishwa.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema jana kuwa siyo tu Serikali imesogeza mbele Bajeti ya Wizara ya Maji, bali pia hata ya Wizara ya Nishati na Madini na sasa zitasomwa mwezi ujao baada ya kubaini kuwa wabunge wengi wamekamia kuzikwamisha kutokana na miradi mingi iliyopangwa mwaka jana kutokamilika.
Wizara ya Maji ilikuwa iwasilishe bajeti yake leo bungeni wakati bajeti ya Nishati na Madini ilikuwa imepangwa kuwasilishwa Mei 23.
Katika kile kinachoonekana ni Serikali kusoma alama za nyakati, imemwandikia Barua Spika wa Bunge, Anne Makinda ikimwomba zisogezwe mbele.
Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi imependekeza bajeti hizo zisogezwe mbele hadi Juni.
Lukuvi jana alithibitisha kumwandikia Spika barua akiomba kusogezwa mbele kwa bajeti hizo akisema ni kutokana na mazungumzo yanayoendelea kati ya Hazina na wizara hizo kuhusu fedha zinazohitajika.
Hata hivyo, chanzo chetu kimeeleza kwamba lengo la Serikali kusogeza mbele bajeti hizo ni ‘janja’ ya kusubiri munkari wa wabunge utulie baada ya kupitisha bajeti za wizara nyingine zisizokuwa na maswali mengi.
Akizungumzia suala hilo Lukuvi alisema: “Bajeti ya Maji hatuiahirishi kwa sababu ya Mnyika, hapana! Nilishamwandikia barua Spika siku nyingi… Hii ya Maji haitasomwa kesho (leo) kwa sababu bado hawajaweka bajeti zao vizuri,” alisema.
Lukuvi alisema baada ya Spika kupokea barua hiyo, alimweleza kuwa ni lazima Kamati ya Uongozi ya Bunge ikutane na itakutana leo na kuna uwezekano leo ikasomwa Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa badala ya Maji.
Wakati Lukuvi akisema kuna mazungumzo na Hazina, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alipoulizwa jana alisema hajui chochote.
Madai ya Mnyika
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni jana, Mnyika alisema lengo lake ni kutaka bajeti hiyo irejeshwe kwenye Kamati ya Bajeti kwa ajili ya kupitiwa upya.
“Ninasema hivyo kwa sababu Serikali imelidanganya Bunge kwa kushindwa kuongeza Sh184 bilioni zilizotakiwa kuongezwa katika Bajeti yake ya mwaka 2013/14,” alisema na kuongeza: “Kati ya Sh184 bilioni, Serikali imeongeza Sh86 bilioni tu… Maana yake ni kwamba Sh98 bilioni hazijatoka mpaka sasa kwenda kwenye miradi ya jamii.
Mnyika alisema hali hiyo imesababisha miradi mbalimbali ya maji, ukiwamo wa vijiji 10 katika halmashauri zote nchini na mradi maalumu wa maji Dar es Salaam kukwama, hivyo atamshauri Maghembe ajiuzulu wadhifa wake kwa sababu ameshindwa kusimamia vyema miradi ya maji.
Waziri Maghembe pamoja na kukiri kupata fedha kidogo, alisema walizopewa zimetekeleza miradi kwa ubora wa hali ya juu.
Alisema pamoja na ufinyu wa bajeti, miradi iliyotekelezwa kati ya Julai, 2013 hadi Machi mwaka huu, imeongeza watumia maji hadi kufikia 2,640,000.
“Kila mwaka tulikuwa tunaongeza watumiaji 200,000 lakini kwa Julai hadi Machi tumeongeza watumiaji mara 10,” alisema.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa