Home » » Fedha Bunge la Katiba zazua balaa bungeni

Fedha Bunge la Katiba zazua balaa bungeni

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Katiba na Sheria,Dk. Asha-Rose Migiro.
 
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka serikali kutoa ufafanuzi wa kiasi halisi cha fedha zilizotumika na zitakazotumika kwenye Bunge Maalum la Katiba.
Tangu kuanza kwa Bunge hilo Kambi hiyo imesema kumekuwapo kauli tata kuhusu kiasi halisi kilichotengwa kwa ajili ya Bunge hilo kutoka kwa viongozi waandamizi wa serikali, huku mmoja akidai kuwa kilichotumika ni Sh. bilioni 27 na mwingine akisema ni bilioni 24.

Naibu Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, Rashid Ali Abdallah alihoji hayo jana wakati akiwasilisha maoni ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Wizara hiyo kwa mwaka 2014/15.

Alisema vyombo vya habari vilimnukuu Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, akisema hadi kuahirishwa kwa Bunge Maalum la Katiba limetumia zaidi ya Sh. bilioni 27.

Ali Abdallah alisema kilichotajwa na Waziri wa Fedha kinalingana na kiasi kilichotajwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera,Utaribu na Bunge), William Lukuvi, aliyeiambia Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwamba hadi linaahirishwa Aprili 25, mwaka huu Bunge Maalum lilikwishatumia Sh. bilioni 27.

Aidha, alisema kauli za mawaziri hao zinatofautiana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, aliyesema Bajeti ya mwaka 2013/14 ilipitisha Sh. bilioni 24.4.

Alisema wakati Waziri Dk. Migiro, alipohojiwa na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala wakati wa Kupitia Makadirio ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2014/2015, alisema:  "Bajeti ya Bunge Maalum ya shilingi bilioni 24.4 ilipitishwa na Bunge katika mwaka wa fedha 2013/2014 kupitia Fungu 21 - Hazina kwenye kifungu cha 'Special Expenditure," alisema.

Alisema serikali ilifanya hivyo kwa kutambua kwamba Bunge Maalum lingeanza kazi zake katika mwaka huo wa fedha  huku mahitaji halisi ya uendeshaji wa Bunge hilo yalikuwa hayafahamiki.

Alimnukuu Waziri Migiro kuwa: "Kwa kutumia uzoefu uliopatikana katika uendeshaji wa Bunge hilo, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 20.0 kwenye Fungu 21 - Hazina kwenye kifungu cha 'Special Expenditure' katika mwaka wa fedha 2014/2015 ili kukamilisha kazi zilizosalia.”

“Tunaitaka serikali ieleze Bunge lako tukufu ni kauli ya Waziri yupi kati ya hawa watatu ndiyo iaminiwe na kuchukuliwa kuwa ndiyo kauli sahihi na Bunge?” alihoji.

Ali Abdallah alisema wakati Bunge la Bajeti katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Kamati ya kudumu ya Bunge iliagiza bajeti hiyo ipelekwe Bungeni kujadiliwa na kupitishwa.

"Kamati ilitoa agizo hilo kwa sababu wakati Wizara ilikuwa imewasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yaani Fungu 08, hakukuwa na fungu lolote linalohusu Bunge Maalum.

Hii ni licha ya ukweli kwamba hadi kufikia mwaka jana, tayari ilikuwa inajulikana kwamba kutakuwa na Bunge Maalum kwa sababu vifungu husika vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vilikwishapitishwa na Bunge lako tukufu,” alisema.

"Serikali hii ya CCM si kivu haikuleta makadirio ya mapato na matumizi ya Bunge Maalum kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge lako tukufu.

Na hata mwaka huu agizo hilo limepuuzwa kwani hakuna makadirio ya mapato na matumizi ya Bunge Maalum ambayo yameletwa kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge lako tukufu,” alibainisha.
Alisema kauli za Dk. Migiro ni kutaka kuiaminisha Kamati kwamba hakukuwa na haja ya fedha za Bunge Maalum kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge kwa sababu tu fedha hizo zilikuwa zinatoka kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.

Alisema kwa mujibu wa sheria, fedha zinazolipwa kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina hazina budi kuidhinishwa na sheria iliyotungwa Bunge na matumizi yake kuidhinishwa na Sheria ya Matumizi ya Serikali, na kwamba Waziri amebadili kauli na kudai kwamba fedha za matumizi ya Bunge Maalum ziliidhinishwa na Bunge.

Aidha, alimnukuu Waziri wa fedha  Mkuya katika taarifa yake ya kikao cha 29 cha Bunge Maalum la Katiba, Aprili 24, mwaka huu, Mkuya akisema:

“Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kwamba hatutumii fursa hii, nasikitika tumechukua fedha, yaani kodi ya wananchi ambayo kila siku wanalia na wameweza ku-sacrifice tunakwenda kwenye twenty seven billions kwa ajili ya session hii (mkutano huu), tumeweza ku-sacrifice kupeleka umeme kwa wananchi, hususan vijijini.”

Aidha, alisema kama itajulikana kwamba mmojawapo kati ya mawaziri hawa watatu ametoa taarifa za uongo kwa Kamati ya Bunge, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka mamlaka ya uteuzi wao, yaani Rais,awawajibishe kwa kuwafukuza kazi.

“Tunaamini kwamba Waziri anayedanganya Bunge au Kamati zake siyo tu analidharau Bunge, bali pia anaidharau mamlaka ya uteuzi wake, yaani Rais. Vinginevyo Bunge lako tukufu liambiwe kwamba Waziri huyo ametumwa na Rais kuja kudanganya Bunge,” alisisitiza.

Alisema uongo wa pili wa kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria unahusu madai yake kwamba bajeti ya Bunge Maalum iko kwenye Fungu 21 – Hazina huku ikiwa kwenye kitabu cha II cha Makadirio ya Matumizi ya Umma ya Huduma za Mfuko Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kilichowasilishwa Bungeni mwaka jana.

Alisema katika Vitabu vyote viwili hakuna kifungu chochote kinachoitwa 'Special Expenditure' au kasma yoyote inayohusu Bunge Maalum.

Aidha, alisema hakuna kifungu chochote chenye makadirio ya matumizi ya shilingi bilioni 24.4 kwa ajili ya Bunge Maalum au kwa ajili nyingine yoyote katika Kitabu cha mwaka 2013/2014; na wala hakuna makadirio ya matumizi ya shilingi bilioni 20.0 kwa ajili ya matumizi ya Bunge Maalum katika Kitabu cha mwaka 2014/2015.

Alisema kwenye Vitabu vya Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na mwaka wa fedha 2014/2015, hakuna kifungu chochote kinachoitwa 'Special Expenditure' au chenye kiasi cha fedha kilichotajwa na Waziri wa Katiba na Sheria.

Alli Abdallah alisema kama hakuna vifungu vyovyote vya 'Special Expenditure' kwa ajili ya Bunge Maalum, na kama hakuna kiasi chochote kilichoonyeshwa kwenye Vitabu vya bajeti, maana yake ni kwamba Bungelako tukufu halijaidhinisha bajeti yoyote kwa ajili ya Bunge Maalum.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, alisema inasikitisha kuwa Wizara hiyo inaongoza katika kusigina na kuvunja utekelezaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema Sheria iko wazi ikieleza michakato minne ambayo ni maoni ya wananchi, mabaraza ya Katiba ya Kata, Bunge Maalum la Katiba na kura ya maoni.

“Ni masikitiko yangu kuwa chini ya Mawaziri (Dk. Migiro na Naibu wake Angela Kairuki) Bunge la Maalum la Katiba likajigeuza sehemu ya kutoa maoni upya huku Spika ukiwapo wakati sheria hii inavunjwa, badala ya Bunge kutekeleza wajibu wake wakujadili Rasimu ya Katiba likaanza kufanya utaratibu mpya wa maoni kinyume na Sheria,” alifafanua.

Mdee alisema Bunge la Katiba akiwemo Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wajumbe wanazungumzia Mabaraza ya Katiba kwamba sheria imeyapa nguvu kubadilisha maoni yaliyotolewa na wananchi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Tume ya Mabadiliko ya Katika mpya, ilitumia zaidi ya Shilingi bilioni 70  huku tunaelezwa Bunge Maalum la Katiba limetumia Shilingi bilioni 27 au 24.4, tunataka mtufafanulie utata huu," alihoji.


“Haiwezekani mfanye usanii wa kuturudisha kwenye Katiba ya sasa wakati inaturuhusu kufanya mabadiliko chini ya kifungu cha 68...Rais kaongeze siku 60 kama watu wanakwenda kuvunja misingi ya Katiba na misingi ya Rasimu ya Katiba ambayo ni chimbuko la maoni ya wananchi, huo ni usanii na matumizi mabaya ya fedha,” alisema.

Mdee alisema hatarajii Bunge la Katiba litaendelea wakati sheria imevunjwa na misingi ya Rasimu ya wananchi imevurugwa.

Alisema makada wa CCM zaidi ya asilimia 95 wamejikusanya ndani ya Bunge hilo na kujiona wana mamlaka ya kubadilisha yaliyopo kwenye sheria na kwamba halikubaliki na wataendeleza mapambano ndani ya nje ya Bunge.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa