Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Pamoja na Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya
Jimbo (CDTF), kuweka sharti la miradi itakayotekelezwa iibuliwe na
wananchi, halmashauri sita nchini zimebainika kukiuka.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), iliyowasilishwa bungeni, inaonyesha kuwa Halmashauri
hizo zilitumia Sh195.5 milioni kwa miradi ambayo haikuibuliwa na
wananchi.
Aidha, halmashauri za wilaya tatu zilitumia Sh19.9
milioni za mfuko huo kugharimia posho za kujikimu nje ya kituo cha
kazi, gharama za usafiri na posho za vikao kinyume cha sheria.
Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Jimbo ya
mwaka 2009, kinaeleza kuwa orodha ya miradi inayoweza kutekelezwa
inatakiwa kuibuliwa na wananchi wanaoishi katika jimbo husika.
Pia Kifungu cha 10(4) cha sheria hiyo kinaitaka
kila kata kuandaa miradi inayopewa kipaumbele na kuiwasilisha kwenye
kamati ya mfuko wa jimbo kwa ajili ya kuidhinisha au kutoidhinisha
miradi hiyo.
CAG Ludovick Utouh katika taarifa yake alisema
tofauti na matakwa hayo ya sheria, miradi yenye thamani ya Sh195.5
milioni iliyotekelezwa mwaka 2012/2013 haikuwa na ushahidi kuwa
iliibuliwa na wananchi. Halmashauri hizo na kiasi cha fedha kwenye
mabano ni Iramba (Sh62.2 milioni), Chato (Sh21.6 milioni), Handeni
(Sh32.7milioni), Sengerema (Sh12.8 milioni), Lushoto (Sh9 milioni) na
Tabora Sh57 milioni.
CAG alisema Kifungu cha 19(2) cha Sheria ya Mfuko
wa Jimbo kinaeleza kuwa, miradi itakayoibuliwa inaweza kuhusisha gharama
za masomo, mipango na ubunifu au nyenzo za kiufundi kwa ajili ya
miradi.
Halmashauri zilizotumia fedha za CDTF kulipana
posho ni Ludewa iliyotumia Sh3.4 milioni kununua mafuta, Urambo
iliyotumia Sh12.8 kwa ajili ya posho za safari na Kondoa iliyotumia
Sh3.7 kulipana posho za vikao.
Katika kipindi hicho pia, halmashauri 66
hazikutumia kabisa kiasi cha Sh2.59 bilioni za mfuko wa jimbo, huku
Halmashauri ya Bariadi ikiongozwa kwa kutotumia Sh248 milioni.
Halmashauri nyingine ni Kilosa Sh190.7 milioni, Mvomero Sh116.3 milioni
na Ilemela Sh106 milioni.
Chanzo:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment