Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakina haja wala mpango wa
kuzungumza na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliosusia
Bunge la Katiba, badala yake watashughulika nao mitaani kwa kujibu
mapigo yao.
“Hatuna mpango wa kuzungumza nao, lakini tuna
mpango wa kushughulika nao mtaani… Tutaendelea kwenda huko wanakopita,”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa
habari mjini hapa jana na kuongeza:
“Nadhani waendelee kukaa barabarani... watu
wenyewe hawajai mkononi, hiyo theluthi mbili inapatikana bila wao, kwa
nini tuwabembeleze?”
Nnauye alikuwa akizungumzia mambo yaliyojadiliwa
katika Kamati Kuu (CC) ya CCM ambayo ilikutana kwa dharura chini ya
Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na kupokea taarifa ya yaliyojiri
ndani na nje ya Bunge Maalumu la Katiba.
Maelezo ya Nnauye yanaonyesha kuwa mjadala kuhusu
Ukawa ulitawala mazungumzo ya kikao hicho hasa ikizingatiwa kwamba
hakueleza jambo jingine lolote lililojadiliwa zaidi ya hilo.
Alisema CC imeipongeza sekretarieti ya Halmashauri
Kuu ya CCM (Nec), chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, kwa kujibu
alichoita uongo na uchochezi unaoenezwa na Ukawa mitaani juu ya mchakato
wa Katiba Mpya.
Sekretarieti hiyo imeshafanya mikutano mbalimbali ya hadhara Pemba na Unguja.
“CC imeitaka sekretarieti na wanachama wanaoitakia
nchi yetu mema kuendelea kujibu kila uongo unaozungumzwa au kuenezwa…
Ujibiwe kwa uzito unaostahili,” alisema.
Alisema pamoja na upungufu uliojitokeza, Kamati
Kuu imeridhishwa na mwenendo na mchakato wa mabadiliko ya Katiba na
kuwapongeza wajumbe waliobaki bungeni akisema wameonyesha uzalendo na
kutanguliza masilahi ya nchi na waliosusia Bunge hilo wameonyesha kuwa
hawana nia wala dhamira ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wanapata
Katiba bora kwa wakati.
Ukawa unaundwa na wajumbe kutoka vyama vya
NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la 201
ambao waliteuliwa na Rais Kikwete.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment