Home » » LISSU AWATAJA MAWAZIRI,ABUNGE WALIOOMBA FEDHA

LISSU AWATAJA MAWAZIRI,ABUNGE WALIOOMBA FEDHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amewataja kwa majina mawaziri na wabunge aliosema bungeni kuwa wamekuwa ombaomba katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Baadhi ya waliotajwa ni pamoja na Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Naibu Spika, Job Ndugai; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi; Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana na wabunge Betty Machangu (Viti Maalumu), Livingstone Lusinde (Mtera), John Komba (Mbinga Magharibi), Eugen Mwaiposa (Ukonga) na Gudluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi).
Hata hivyo, gazeti hili halijawataja majina mawaziri na wabunge wengine waliomo kwenye orodha hiyo ya Lissu kwa kuwa hawakupatikana jana kujibu tuhuma hizo.
Mbali na kuwataja kwa majina, Lissu pia ametoa vielelezo vinavyoonyesha jinsi walivyokuwa wakiidhinishiwa malipo kwa nyakati tofauti na Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF), kwa sababu mbalimbali.
Lissu alimwambia mwandishi wetu jana kuwa licha ya kiwango cha fedha kutokuwa kikubwa, lakini kinaweza kusababisha mgongano wa kimasilahi kati ya wajibu wa wabunge kwa umma na masilahi yao binafsi.
“Hali hii inaweza kusababisha Bunge likashindwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia Serikali na taasisi zake,” alisema Lissu huku akisisitiza azimio lake la kuwasilisha hoja binafsi kwa Spika wa Bunge ili iundwe tume kuchunguza suala hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga jana alikiri kuwa shirika hilo liliidhinisha malipo kwa mawaziri na wabunge hao kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo, alisema shirika hilo halitoi fedha taslimu, bali hununua vitu ambavyo viliombwa na viongozi hao kwa ajili ya kusaidia wananchi na si kufanya biashara.
Sakata lenyewe
Akizungumzia jinsi mawaziri na wabunge hao walivyosaidiwa, Lissu alisema LAPF ilitoa Sh2.5 milioni kwa ajili ya mradi wa madarasa Jimbo la Kongwa linaloongozwa na Ndugai.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Ndugai alisema hakuna tatizo lolote kwa mbunge kupewa msaada na mfuko wa kijamii.
“Huyo Lissu ana upungufu mkubwa. Hivi LAPF ikisaidia Sh2 milioni kwa ujenzi wa darasa unaogharimu Sh10 milioni ni tatizo hilo? Nchi hii inakwenda wapi jamani, siyo kila kitu wanachozungumza wapinzani ni hoja, kama LAPF wangekuwa wanatoa fedha lingekuwa tatizo lakini wanasaidia vifaa tu.”
Lissu alisema nyaraka alizonazo zinaonyesha kuwa Agosti, 2013 LAPF iliidhinisha fedha za kununulia pikipiki mbili kwa ajili ya vituo vya afya vya Jimbo la Mtera linaloongozwa na Lusinde.
Kama ilivyokuwa kwa Mwaiposa, Lusinde naye alisema kuomba si kosa na kwamba amekuwa akiomba misaada sehemu mbalimbali kwa ajili ya kulisaidia jimbo lake.
“Fedha hizo tumeshapata na pia tuliomba nyingine katika Kiwanda cha Saruji cha Wazo bado hatujapata,” alisema Lusinde na kusisitiza kuwa mbunge hawezi kuona mambo hayaendi katika jimbo lake kisha akakaa kimya.
Lissu pia alisema LAPF ililipa Sh1.5 milioni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ajili ya Mfuko wa Nyasa Foundation uliopo katika eneo la jimbo linaloongozwa na Komba ambaye pia ni mlezi wa mfuko huo.
Komba alifafanua kuhusu fedha hizo na kusema: “Zilikuwa za Harambee na tuliomba sehemu nyingi lakini mimi siyo niliyeomba. Wao ndiyo waliomba na hata hundi walichukua wao.”
Lissu pia alisema LAPF iliidhinisha Sh1.5 milioni kwa ajili ya mradi wa maabara wa Jimbo la Arumeru Magharibi la Medeye madai ambayo mbunge huyo aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema ili ayajibu anataka mwandishi awe pamoja na Lissu na wakae wote watatu kwa pamoja.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa