Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi akizungumza bungeni,
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola amesema iwapo Muswada wa
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), hautapelekwa bungeni, atakusanya
saini za wabunge ili kumwondoa madarakani Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Lugola aliyasema hayo jana alipokuwa akiomba
mwongozo wa Spika ni lini muswada huo unaolenga kufuta misamaha ya kodi
utaletwa bungeni.
Alisema amepata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wake
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ya Mitaa (Laac),
Rajab Mborouk Mohamed ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Uongozi kuwa kamati
hiyo iliiagiza Serikali kuwasilisha haraka Muswada wa VAT.
Alisema lengo la kutaka muswada huo uletwe bungeni ni kupitia na kufuta misamaha yote ya kodi isiyo na tija.
Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2012/2013 inaonyesha kuwa kuna
misamaha ya kodi ya Sh1.5 trilioni nchini.
“Bajeti yetu ya mwaka jana inaonekana ina upungufu
wa Sh1.5 trilioni na kusingekuwa na misamaha ya kodi mwaka jana
tusingekuwa na upungufu huo,” alisema.
“Wabunge tumekuwa tukiilazimisha Serikali iongeze
fedha. Wabunge ndiyo waliomchagua Spika na Spika ameonyesha kuipendelea
Serikali ilhali wananchi wanashindwa kupata maendeleo,” alisema.
Alihoji ni lini muswada huo utaletwa bungeni kwa sababu karibu Bunge la Bajeti linaelekea ukingoni.
“Haya mambo ya wabunge kutishwatishwa kwamba
tukikataa Bajeti ya Serikali Bunge litavunjwa. Mimi niko tayari Bunge
livunjwe nirudi Mwibara nikalime na kuvua dagaa,” alisema.
Alisema kama muswada huo hautaletwa katika Bunge
la Bajeti atakuwa mbunge wa kwanza kuleta hoja ya kumtaka spika afukuzwe
kwenye kiti hicho kwa sababu anaibeba Serikali.
Alipoulizwa baadaye jana jioni sababu ya
kumng’ang’ania Spika, Lugola alisema: “Ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi ambayo hupanga ratiba. Ukitazama ratiba ya mkutano huu, hakuna
mahali panapoonyesha Serikali italeta muswada huo wa VAT badala yake,
Serikali inasema tu kwa mdomo na yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi,” alisema Lugola.
Akijibu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Serikali ndiyo
iliyoomba kuleta Muswada wa VAT katika Bunge hili bajeti... “Hana sababu
ya kumsingizia Spika kuibeba Serikali.
Tunakusudia kuuleta katika Bunge hili ili usomwe mara ya kwanza na tungependa upite katika hatua zote.”
Siku chache kabla ya kuanza kikao hicho cha Bunge,
Lukuvi alisema Serikali itawasilisha bungeni rasimu ya maboresho ya VAT
ambayo itafuta misamaha ya kodi hiyo na kwamba mpango huo unafanyiwa
uchambuzi na Serikali na kwamba utawasilishwa katika wiki ya pili ya
Bunge la Bajeti.
Kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa CUF ambaye pia
ni mtaalamu wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba na wadau mbalimbali wa
uchumi walikuwa wakipigia kelele wingi wa misamaha ya kodi wakisema
imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha mapato ya Serikali.
Profesa Lipumba alisema hivi karibuni kuwa ili
kuondoa kasi ya ukuaji wa nakisi, Serikali inatakiwa kufuta kabisa
misamaha holela ya kodi inayofikia Sh1.8 trilioni ambayo ni sawa na
asilimia tano ya pato la taifa.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya wakati akiwasilisha
mpango wa Bajeti ya mwaka 2014/15 kwa wabunge, alisema Serikali imepanga
kukamilisha utungwaji mpya wa Sheria ya VAT.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na kuongeza
wigo wa kodi kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kuanzisha vyanzo vipya
pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo rasmi wa
kodi.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment