Home » » Makomandoo kulinda tembo

Makomandoo kulinda tembo

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (kushoto), akimsikiliza Naibu wake, Mahmoud Mgimwa, wakati wabunge wakichangia hotuba ya bajeti ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 bungeni mjini Dodoma jana.
 
Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza kiama kwa majangili baada ya kuunda  kikosi maalum cha makamandoo waliofuzu mafunzo ya kijeshi watakaotumia ndege moja na helkopta tatu kwa ajili ya kupambana na majangili katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba zikiwa jitihada za kulinda tembo na faru.
Mpango huo ulitangazwa na Waziri wa Malisili na Utalii, Lazaro Nyalandu,  wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2014/15 juzi jioni.

Nyalandu alisema kikosi hicho kitakuwa na uwezo wa kushuka kutoka kwenye helkopta hizo na kuwakamata majangili katika maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba baada ya ndege hiyo ya kisasa kufanya doria.

Pia alisema kuwa kikosi hicho kitakwenda kwenye mafunzo mwezi ujao Afrika Kusini.

Nyalandu alisema kikosi hicho kikiwa na helkopta kitafanya doria katika pori la akiba la Selous, Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi za Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kupambana na majangili.

Alisema kuwa kikosi hicho kitakuwa na magari zaidi ya 20 yenye askari waliopata mafunzo maalum yatakuwa na kazi ya kuwasiliana na makomandoo watakaotumia helkopta.

Waziri Nyalandu alisema magari, ndege na helikopta moja vimetolewa kama msaada kutoka kwa wahisani wa kimataifa wakati helkopta mbili zitanunuliwa kwa fedha za serikali.

Akizungumzia kuhusu ndege hiyo iliyoletwa kama msaada mwezi huu na Serikali ya Ujerumani, alisema itakuwa na uwezo wa kufanya doria usiku na mchana ambayo ikipita katika hifadhi ina uwezo wa kutambua joto la binadamu na mnyama pamoja na kupiga picha na kutuma taarifa katika ofisi ya utambuzi.

“Baada ya kutoa taarifa linaangaliwa eneo kama ni la barabara na baada ya hapo yanatumwa magari, lakini kama hakuna tunapeleka helkopta yenye makomandoo kwa ajili ya kuwakamata,” alisema Waziri Nyalandu.

Alisema kuwa wafadhili hao wameshatoa Dola za Marekani milioni tano (sawa na Sh. bilioni 8.2) ambazo zimeanza kutumika kwa ajili ya matayarisho ya askari hao kwa kuwajengea mabweni, kununua magari, kununua mitambo ya mawasiliano na helkopta.

Alisema Hifadhi ya Ngorongoro na zile za Tanapa licha ya kununua helkopta hizo mbili kwa ujumla zitachangia Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kupambana na vitendo vya ujangili.

Waziri Nyalandu alisema kuwa wanatarajia kufanya mazungumzo na Mtandao wa mawasiliano wa Google kwa ajili ya kuongeza jitihada za kupambana na majangili.

Aliongeza kuwa wamekubaliana na mashirika ya kimataifa kwa ajili ya kuanzisha mfuko maalum wa uchangiaji kwa lengo la kulinda wanyama katika maeneo ya mapori ya akiba na hifadhi.

Wakati Waziri Nyalandu akitangaza mpango huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilisema kutohukumiwa na kuharibiwa kwa kesi za ujangili, upungufu wa rasilimali watu hasa askari wanyamapori na kukosekana kwa silaha za kisasa kwa ajili ya kukabiliana na majangili, kumechangia kuongezeka kwa ujangili nchini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli, aliyasema hayo juzi katika hotuba yake kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2013/14 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara.

Alisema kamati inasikitika kuona bado ujangili umeendelea kuwa changamoto kubwa katika mapori yote ya akiba na hakuna dalili yoyote inaonyesha kupungua kwake kutokana na sababu hizo.

Lembeli alisema ujangili wa tembo umekuwa ni janga la kitaifa kwa kuwa wanateketezwa. “Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Taasisi za Utafiti wa wanyamapori za serikali na mashirika nchini na kimataifa, tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku, 850 kwa mwezi na 10,000 kila mwaka,” alisema.

Alisema Shirika la Tawiri limeonyesha taarifa za kitaalam zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka 2009 na kufikia 70,000 mwaka 2012.

Lembeli alisema iwapo kasi hiyo haitadhibitiwa na kuachwa kuendelea bila kudhibitiwa mara moja ni wazi kuwa tembo watakuwa wametoweka nchini katika miaka saba ijayo.

“Hali hii ni hatari na aibu kwa nchi yetu ambayo ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo...tunampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa jitihada zake binafsi za kudhibiti ujangili wa tembo na kuwezesha kupewa msaada wa helkopta na ndege zitakazosaidia kupambana na ujangili,” alisema.

Kadhalika, kamati imehoji kuhusu mgongano kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Maliasili na Utalii katika utozaji wa kodi kwa silaha na faru wanaoletwa na wahisani.

Lembeli alisema ni jambo la kusikitisha kwamba pamoja na Tanzania kuwa na hazina kubwa ya wanyamapori, bado serikali haijalipa kipaumbele na umuhimu unaostahili.

Alisema ingawa Wizara imeonyesha nia ya wazi ya kukabiliana na ujangili, hivyo kununua silaha za kukabiliana na hali hiyo, lakini TRA ilizuia silaha hizo bandarini ikidai kodi kwa zaidi ya mwaka mmoja.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa