Home » » MENO YA TEMBO YAIBWA KATIKA KITUO CHA POLISI

MENO YA TEMBO YAIBWA KATIKA KITUO CHA POLISI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Polisi akilinda sehemu ya shehena ya meno ya tembo iliyokamatwa Dar es Salaam hivi karibuni.

Meno ya tembo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya vielelezo mahakamani yalitoweka katika Kituo cha Polisi cha Kilwa mkoani Lindi.
Tukio hilo limenukuliwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikisema meno makubwa 108 ya tembo na kilo 20 za meno mengine ya tembo yaliyokuwa yamehifadhiwa kama kielelezo cha kesi za uhujumu uchumi, yamebainika kutoweka kinyemela.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni juzi, imebainisha kuwa meno mengine makubwa ya tembo yaliyokuwa na uzito wa kilo 498.3 yamebadilishwa kinyemela na meno madogo, hivyo kusababisha hasara ya kilo 203.66 za meno ya tembo ambazo thamani yake haikufahamika.
CAG Ludovick Utouh katika ripoti hiyo ya mwaka ulioishia Juni 30, 2013, amebainisha kuwa kumbukumbu katika Pori Tengefu la Miguruwe zilionyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Juni 5 hadi Juni 8, 2012 meno makubwa 108 yalikuwa miongoni mwa vielelezo kituoni hapo.
Kati ya meno hayo 108 yaliyokamatwa katika matukio ya ujangili, 74 yalitoweka katika kituo cha polisi wakati 34 yalibadilishwa na meno madogo, tofauti na yale yaliyokuwa yamekamatwa yakihusishwa na kesi ya ujangili Na. 3/2009 na kesi nyingine ya uhujumu uchumi Na. 2/2010 ambazo zilikuwa zikiendelea mahakamani mkoani Lindi.
Pia ilibainika kuwa kilo 20 za meno ya tembo ambayo yalikamatwa na kuhifadhiwa kama kielelezo cha majalada KLM/IR/184/2009, KLM/IR/235/2009 na KLM/IR/567/2010 yalitoweka.
Gari la ujangili latoweka
Ukaguzi huo pia ulibaini kuwa gari lililokamatwa likiwa kielelezo baada ya kukutwa na kilo 26 za meno ya tembo yenye thamani ya Sh135 milioni liliondolewa kinyemela katika Kituo cha Polisi Kilwa.
CAG katika ukaguzi huo alibaini upungufu katika usimamizi wa meno ya tembo na nyara nyingine za taifa katika chumba cha meno hayo Dar es Salaam na vituo vya mikoani.
CAG katika taarifa yake hiyo amesema kutokana na kukosekana kwa kumbukumbu sahihi, meno ya tembo yanaweza kuibwa au kupotea bila menejimenti kuwa na taarifa yoyote, hivyo ameishauri Serikali kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa kutosha katika usimamizi wa nyara za Serikali nchi nzima.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa