Home » » MKAGUZI AZINYOSHEA KIDOLE TDFA,TBS

MKAGUZI AZINYOSHEA KIDOLE TDFA,TBS

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amezinyooshea kidole mamlaka mbili za Serikali kwa kushindwa kudhibiti uingizaji wa bidhaa zisizo na ubora nchini.
Taarifa ya CAG kuhusu ukaguzi wa ufanisi na ukaguzi maalumu kwa kipindi kinachoishia Machi 31, 2014, imezitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), akisema zilipwaya katika ukaguzi wa ubora wa chakula kinachoingizwa na kuzalishwa nchini.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa ufuatiliaji ulishindwa kuzuia viwanda vya usindikaji chakula kuvunja sheria mara kwa mara.
Kwa mujibu wa CAG, asilimia 80 ya viwanda vilivyokuwa vimekiuka sheria havikuchukuliwa hatua, huku kukiwapo makosa ya kujirudiarudia kwa wasindikaji na waagizaji chakula nje ya nchi.
Taarifa hiyo imesema kwa hali inavyoonekana, idadi ya bidhaa hafifu nchini imekuwa ikiongezeka kwa miaka mitatu kwa kati ya asilimia 30 na 40 kutoka mwaka wa fedha wa 2010/2011.
Bidhaa hizo nyingi hupita katika bandari na mipaka ya Tanzania ambayo wakaguzi wa TBS walitakiwa kuzikagua, lakini kutokana na upungufu wa ukaguzi, zimekuwa zikiingia nchini.
Katika taarifa hiyo, CAG alisema ukaguzi wa ubora wa bidhaa zinazoingia nchini haukufanyika vizuri na vya kutosha na ukaguzi wa bidhaa kutoka nje haukufanywa kwa kuzingatia viashiria hatarishi.
“Bidhaa zote zilipewa kipaumbele sawa wakati wa ukaguzi licha ya ukweli kwamba baadhi ya bidhaa zinajulikana kuwa na athari kubwa kwa afya na mazingira ya walaji nchini,” imesema taarifa hiyo.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa