Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
ameitaka Serikali kueleza jinsi ilivyopata fedha za kuendesha Bunge
Maalumu la Katiba kwa kuwa Bunge la Muungano halikuwahi kuziidhinisha.
“Hadi sasa Bunge (la Muungano), halijui bajeti
yote ya Bunge Maalumu la Katiba. Halijui fedha kiasi gani zimetumika kwa
ajili ya matengenezo mbalimbali ya miundombinu ya Bunge la Katiba,”
alisema katika hotuba yake ya maneno 10, 910.
Fedha alizokuwa akihoji Mbowe ni zilizotumika
kulipa posho, mishahara na stahiki mbalimbali za wajumbe na watumishi wa
Bunge Maalumu hadi lilipoahirishwa Aprili 25, mwaka huu na hata
litakaporejea Agosti 5, mwaka huu.
Wasiwasi wa Mbowe unalenga kupata majibu ili
kuliepusha Taifa na balaa la ufisadi na wizi wa fedha za umma kama
ilivyotokea mwaka 2005.
Mbowe alisema mwaka huo mabilioni ya fedha za umma
yaliibwa kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA), ya Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), kwa ajili ya kugharimia kampeni za Uchaguzi Mkuu wa CCM
na mgombea wake wa urais.
Alisema Serikali haijawahi kutoa makadirio ya
matumizi kwa ajili ya shughuli za Bunge la Katiba licha ya kutakiwa
kufanya hivyo mwaka jana na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati
wa mjadala wa makadirio na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria mwaka
2013/14.
Alisema fedha za Bunge la Katiba zilitakiwa
kuidhinishwa kisheria kama inavyosema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
kwamba fedha hizo zitatoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.
Alisema zilitakiwa kuidhinishwa na ama na Sheria
ya Matumizi ya Serikali iliyotungwa mahsusi na Bunge au sheria
iliyotungwa kwa mujibu wa Ibara ya 140 ya Katiba inayohusu mfuko wa
matumizi ya dharura unaoanzishwa kwa ajili ya mambo ya haraka na
dharura.
“Hata kama fedha za matumizi ya Bunge la Katiba
zingeainishwa kama inavyotakiwa na Katiba, bado matumizi hayo yalitakiwa
kuidhinishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),”
alisema Mbowe.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment