Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Omar Nundu
Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Omar Nundu jana aliikalia kooni
Serikali kwa kuwakumbatia wageni na kuibua madai kuwa baadhi ya vigogo
wa Serikali walipewa nyumba wakati wa kubinafsisha viwanda nchini.
Nundu ambaye ni Mbunge wa Tanga Mjini (CCM),
alitoa kauli hiyo jana jioni alipokuwa akichangia bajeti ya Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda kwa mwaka 2014/15. “Hizi tax
holiday (kipindi maalumu cha kusamehewa kodi) ziondolewe maana siyo
tunasema maneno tu, umefika wakati sasa maneno yakae kando vitendo
vifanye kazi, watu wamechukua viwanda kwa ajili ya kuvidhoofisha tu,”
alisema.
“Tanga kule vimejaa chungu nzima (viwanda) na
tunapoongelea mbolea, tena tunakuwa kama tunaongelea maji tu… Tunayajua
mliyoyafanya. Vipo mlivyopewa kutoa viwanda vile. Ondoeni mawazo hayo
msitupeleke mpaka tukasema mambo haya humu ndani,” alisema Nundu na
kuongeza:
“Mnapewa vijijumba, watu wazima ovyoo, unapewa
kijijumba halafu unadhalilisha nchi hapa! Mmeyafanya! Twende viwanda
virudi tufanye kazi,” alisema Nundu bila kuwataja kwa majina waliopewa
nyumba.
Nundu alisema uchumi duniani kote unategemea
viwanda na kwamba pamoja na wizara kueleza mambo mengi ukweli ni kwamba
hayatoshi na kuna mengi ya kufanya.
Utajiri wa magadi
Awali, akiwasilisha bajeti yake, Waziri wa Viwanda
na Biashara, Dk Abdallah Kigoda alisema uzalishaji wa magadi soda
utaanza kuliingizia taifa Dola 320 milioni za Marekani (Sh520 bilioni)
kwa mwaka kuanzia mwaka 2016/17.
Alisema mradi huo unaoendeshwa na Shirika la
Maendeleo ya Taifa (NDC), unatarajia kuzalisha tani milioni moja za
madini hayo na bidhaa nyingine za chumvi kwa mwaka. Alisema tafiti
kuhusu wingi na ubora wa rasilimali ya magadi soda zilikamilika mwaka
2013/14 na kiasi cha tani bilioni 4.68 za magadi ambazo huongezeka kwa
mita za ujazo milioni 1.86 ziligunduliwa.
Dk Kigoda alisema kiasi hicho kiligunduliwa katika Bonde la Engaruka na jitihada za kumtafuta mtaalamu mshauri zimeanza.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment