Home » » SAIDI MJULIZI:MGUNDUZI WA RANGI ZISIZOTUMIA KEMIKALI ZA ASILI

SAIDI MJULIZI:MGUNDUZI WA RANGI ZISIZOTUMIA KEMIKALI ZA ASILI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Saidi Mjulizi akiwa katika mchakato wa kutengeneza rangi alizogundua kwa kutumia miti.
Wengi tumezoea kusikia kuwa mchakato wa utengenezaji wa rangi, hauwezi kukwepa matumizi ya kemikali. Huo siyo ukweli, Mtanzania Saidi Mjulishi amepewa tuzo na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ikimtambua kama mgunduzi wa rangi maalumu za asili zisizotumia kemikali.
Sifa moja kubwa ya bidhaa nyingi anazotumia mwanadamu ama zinatokana na kemikali au mchakato wa utengenezaji wake unahusisha matumizi ya kemikali.
Hivi ndivyo ilivyo kwa bidhaa mbalimbali muhimu kwa mwanadamu, vikiwamo vyakula, vinywaji na vinginevyo.
Hapa nchini wakati sayansi na teknolojia vikielezwa kushika kasi, Mtanzania aitwaye Said Mjulishi ameingia katika orodha ya wagunduzi kwa kubuni  rangi maalumu za asili anazosema hazina mchanganyiko wowote na kemikali kama ilivyo kwa rangi nyingine za viwandani.
Katika mahojiano na mwandishi wetu, Maimuna Kubegeya, Mjulizi ambaye ni kitaaluma ni mhandisi, anaelezea kwa kirefu ugunduzi wa rangi hizo anazosema zina uwezo mkubwa wa kuboresha mazingira.
Swali: Tueleze historia yako kwa kifupi
Jibu: Mimi ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera. Baada ya kumaliza elimu yangu ya msingi nilijiunga na kilichokuwa Chuo cha Ufundi cha  Dar es Salaam, sasa kinafahamika kwa jina la Dar es Salaam Insititute of Technology (DIT).
Nikiwa chuoni nilisomea kozi ya uhandisi. Baada ya kumaliza niliajiriwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa na kufanya kazi katika kitengo cha mashine za kusaga.
Swali: Ilikuwaje ukaangukia kwenye ugunduzi hasa huu wa rangi za asili?
Jibu:  Ni historia ndefu, lakini kwa kifupi ni kwamba ule ujuzi wangu nilionao katika masuala ya uhandisi, umekuwa ni chanzo cha kuniongezea udadisi. Unajua  unapokuwa na kiu ya kutaka kujua jambo, inakuwa ni rahisi kupata suluhisho.  Kwa muda mrefu nimekuwa nikishuhudia watu wakipata athari wanapotumia rangi zenye kemikali.
Wako watu wangu wa karibu walioathiriwa na hata kupata matatizo kadhaa yakiwamo ya ngozi na hata mzio kutokana na matumizi ya rangi zenye kemikali.
Baada ya kufikiria kwa kina nikapata wazo la kufanya utafiti kupitia miti ili nione kama naweza kugundua rangi zisizokuwa na athari kiafya.
Swali: Nini kikafuata baada ya kuamua kufanya utafiti huo?
Jibu:  mwaka 2006 nikaanza mradi wa kwanza wa utafiti kwa kutumia miti kadhaa na baadaye  nikafanikiwa kugundua miti aina mbili  ambayo ni  mfumbo na mtuntu. Mwaka 2012, baada ya kushuhudia kazi zangu, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ilinitangaza rasmi kama mgunduzi wa rangi.
Swali: Rangi za aina gani ulizogundua kupitia utafiti huo?
Jibu: Kwa sasa nimegundua rangi za aina mbili na bado  naendelea na utafiti wa rangi nyingine. Rangi zilizopo sasa ni  zambarau na hudhurungi. Rangi  hizi zinaweza kutumika kwenye nguo, lakini hii ya hudhurungi pia inaweza kutumika kwenye mbao kama dawa ya kuulia wadudu au rangi tu ya kawaida hasa kwa mbao nyeupe.
Sifa ya rangi hizi ni kuwa  zina uwezo wa kupambana na wadudu wanaobungua mbao, hivyo ni suluhisho tosha kwa wale wanaohitaji kupaka rangi kwenye mbao za kujengea.
Swali: Ukoje mwitikio wa jamii kuhusu matumizi ya rangi ulizogundua?
Jibu: Kwa sasa tuko katika kampeni ya kuhakikisha watu wengi wanaelewa umuhimu  kutumia rangi hizi. Kwa kushirikiana na wadau kama Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), tumekuwa tukiendesha mafunzo kuhusu matumizi yake.
Kwa mfano, tayari tumeshaangaza kutoa mafunzo ya utengenezaji wa batiki kwa kutumia rangi hizi. Kimsingi, rangi hizi hazina athari yoyote kiafya tofauti na zile zilizozoeleka. Hadi sasa tumeshawafundisha watu zaidi ya 60 katika  awamu ya kwanza ya mafunzo, mipango yetu ni kuwafikia watu wengi zaidi.
Kwa upande wa rangi za mbao, tayari tumeanza kusambaza katika maduka kadhaa ya Dar es Salaam. Aidha,  tuna mpango wa kwenda mbele zaidi na kuwafikia Watanzania wengi.
Swali:  Huoni kuwa ni uharibifu wa mazingira kutumia miti kutengeneza rangi?
Jibu: Miti hii tunayotumia kwa kawaida huwa na tabia ya kujivua magamba na hii ndiyo sifa ya pekee ya miti hii. Tunachotumia ni magamba yake hivyo  hatuna haja ya kukata miti, tunachokitumia kama malighafi yetu kubwa ni yale magamba. Halafu hata mabaki bado ni  rafiki wa mazingira, kwani yanaweza kutumika kama kuni au hata  mbolea.
Swali: Una  wito gani  kwa Serikali na jamii kwa jumla
Jibu: Serikali itoe msaada kwa wagunduzi kwani kwa kufanya hivyo tutaweza kukuza teknolojia yetu. Kwa upande wa wananchi, nawasihi wahamasike kutumia vitu vinavyogunduliwa na watafiti  wa ndani. Hii itasaidia kuwapa hamasa  ya kugundua mambo mengi zaidi.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa