Home » » Sheria kutungwa kuwalinda watoa siri za uhalifu

Sheria kutungwa kuwalinda watoa siri za uhalifu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro
 
Wizara ya Katiba na Sheria inatarajia kuwasilisha bungeni miswada mbalimbali ikiwamo wa upatikanaji wa msaada wa kisheria katika kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha hotuba ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2014/15.

Alisema miswada hiyo itahusu kulinda mashahidi na waathirika wa vitendo vya jinai, kulinda watu wanaotoa taarifa kwa siri kuhusu vitendo vya uhalifu au vya ukiukwaji wa maadili.

Alisema mswada mwingine ni marekebisho ya sheria au usajili wa vizazi na vifo, sheria ya ufilisi.

Sambamba na hilo, Dk. Migiro alibainisha kuwa katika kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria, Wizara inakusudia kueneza mfumo wa usajili wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga.

Alisema pia ni kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa taasisi za mafunzo za Wizara sambamba na kusimamia na kufuatilia utoaji haki kwa kusimamia shughuli za uendeshaji na usikilizaji wa mashauri.

Pia, alisema ni kuziimarisha kamati za maadili za Mahakama katika ngazi ya mikoa na wilaya kwa kuzipa mafunzo na kuzifanyia ukaguzi na kwamba kazi hiyo itaanza katika mikoa ya Dodoma, Katavi, Shinyanga, Mara, Mwanza, Rukwa, Singida na Tabora.

Dk. Migiro alisema mipango mingine ni kuimarisha utekelezaji wa mpango wa kutenganisha shughuli za upelelezi na mashtaka.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa