Home » » SOMA HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. MCH. PETER SIMON MSIGWA, (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KWA MWAKA WA FEDHA 2014-2015

SOMA HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. MCH. PETER SIMON MSIGWA, (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KWA MWAKA WA FEDHA 2014-2015

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Mheshimiwa Peter Msigwa
--  
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. MCH. PETER SIMON MSIGWA, (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
1.0  UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,  Frank Herbert aliwahi kusema
 “Utawala bora, kamwe hautegemei Sheria bali sifa binafsi za wale wanaotawala. Vyombo vya Serikali mara zote vipo chini ya wale wanaowaongoza. Kwa hiyo sifa muhimu ya Serikali ni namna ya kuteua/kuchagua viongozi” 
Serikali ya awamu ya nne, imeshindwa kuwajenga viongozi wake katika misingi bora na ndio maana pamoja na matatizo ya kimfumo, wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kubadilisha viongozi na matokeo ya ufanisi wake yamekua ni kioja na dhihaka katika utendaji. 

2.0       UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO 16 YA BUNGE
Mheshimiwa Spika, kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilileta Bungeni taarifa yake tarehe 20 Disemba 2013 liyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Mhe. James Lembeli kuhusu uchunguzi wa matatizo katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyokua na maazimio kumi na sita (16). Taarifa hiyo ndiyo iliyomuondoa aliyekua Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na mawaziri wengine. 
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya maazimio ya Bunge, yaliyoongezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni pamoja kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi wa Kimahakama. Aidha, ni takribani miezi zaidi ya mitano kupita tangu Serikali iahidi Desemba mwaka jana, kuahidi, kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuunda tume maalumu ya kuchunguza kilichotokea wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Katika makujukumu yake, Tume hiyo imepewa kazi zifuatazo;
a)  Kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa;
b)  Kuchunguza na kubaini iwapo sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza operesheni hiyo.
c)   Kuchunguza na kubaini kama kuna mtu aliyekiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea wakati wa operesheni;
d)  Kuchunguza na kubaini kama kuna watu ambao walikiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki;
e)   Kupendekeza hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu ambaye itabainika alikiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea pamoja na kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuundwa kwa Tume hii lakini Serikali haikupaswa tena kuipa tume kazi mpya katika maeneo yote bali  yale yaliyohitaji  ushahidi wa ziada wa kijinai, hii ni kwa sababu makosa mengine yako wazi ambayo Serikali ilipaswa iwe imeshachukua hatua badala ya kusingizia inasubiri taarifa ya tume. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, sasa inaitaka Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge wakati wa Majumuisho ya Bajeti ya Wizara ili maazimio ya Bunge hili yasiishie kabatini kama ilivyokuwa kwa mengine ya miaka ya nyuma na ilivyozoeleka sasa.
2.1       Uwajibishwaji Wa Watendaji Kutokana Na Maazimio Ya Bunge
Mheshimiwa Spika, aidha katika azimio namba Saba (7), Bunge liliazimia pia kumwajibisha Mkurugenzi wa Wanyamapori Prof. Alexander Songorwa kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kwenye vyombo vya habari na kuudanganya umma kuhusu mazingira na kifo cha Emiliana Marrow wa Babati.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kushangaza Waziri wa Maliasili na Utalii wa sasa, Mhe. Lazaro Nyalandu ambaye akiwa katika nafasi yake ya unaibu waziri, kipindi kifupi tu kabla ya uteuzi wake, kwa kasi ya ajabu aliandaa mikutano mingi na ziara mbalimbali huku akiandamana na lundo la vyombo vya habari kama kumbikumbi,na kutoa matamko makali dhidi ya ujangili na watumishi wasio waaminifu. Akiwa katika ziara hizo, aliwahi kuikandia sana Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili iliyoongozwa na Mhe. James Lembeli, huku akidai kuwa ilikuwa ya uwongo mtupu. Lakini baada ya kubanwa zaidi, alikana kutoa kauli za kuikosoa ripoti hiyo ya kamati. Sababu za kwanini akanushe maneno aliyoyasema zaidi ya mara nne, inabakia kuwa siri yake mwenyewe. 
Mheshimiwa Spika, Waziri Nyalandu alitoa taarifa za kuwavua nyadhifa zao Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori na  Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori nyadhifa zao. Nyalandu anadai kuwa moja ya sababu za kuwaondoa, ni kutekeleza maazimio ya Kamati ya Lembeli kutokana na kutowajibika wakati wa Operesheni Tokomeza. 
Jambo la kujiuliza, kama aliwahi kusema kuwa taarifa ya kamati ni uongo mtupu, je ni lini amethibitisha kuwa kile alichodai kwamba ni uwongo, ulikuwa ukweli? Cha ajabu, aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi, Paul Sarakikya aliyekuwa kiongozi wa utekelezaji wa operesheni tokomeza na aliyehusika moja kwa moja na kinachodaiwa kuwa uvunjifu wa haki za binadamu, ndiye amepewa nafasi ya kukaimu ukurugenzi! Wote tunafahamu ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na ukatili uliofanywa katika operesheni tokomeza kiasi cha kusababisha mawaziri wanne kuwajibishwa kwa kutenguliwa nafasi zao.
Mheshimiwa Spika, aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ilitumia vigezo gani kumteua Sarakikya kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa Wanyamapori huku ikijua alivyoshindwa kutokomeza ujangili hapa nchini na jinsi aliyoendesha operesheni tokomeza ujangili iliyokuwa imejaa dhuluma, uporaji, utesaji na udhalilishaji dhini ya wananchi. Jambo ambalo liliishangaza zaidi Kambi Rasmi ya Upinzani ni kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Ndugu Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori huku akijua kuwa Sarakikya alifanya makosa mengi katika utendaji wake wa  kazi katika idara hiyo ya Wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe pia kuwa Ndg. Sarakikya ndiye aliyeongoza kikosi cha kuzuia ujangili hata kabla ya operesheni tokomeza. Katika kipindi hicho, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza kati ya nchi nane duniani zilizoongoza kwa matukio ya ujangili. Aidha, ili kuonyesha kwamba Serikali hii haizingatii weledi katika utendaji, alietuliwa tena kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili. 
2.2 Kauli Tata Za Serikali Juu ya Kufukuzwa Kazi kwa Wakurugenzi
Mheshimiwa Spika, mara baada ya waziri kutangaza kuwavua nyadhifa zao wakurugenzi hao tarehe 24 Februari 2014, Katibu Mkuu wa wizara hii Bi. Maimuna Tarishi aliwarudisha kazini wakurugenzi hao huku Serikali nayo kwa kupitia kurugenzi ya habari maelezo,ikitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa taarifa za kufukuzwa kwa wakurugenzi hao si sahihi. Pia, Ikulu kwa kupitia Katibu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, ilitoa tamko la kuitaka Wizara kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma za kumfukuza mtumishi kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002, Kifungu cha IV (23) (2) inayozungumzia mamlaka ya Rais kumwondoa mtumishi aliyemteua kazini, amri ya kumfukuza mtumishi wa umma itatekelezwa iwapo;
(a)hati ya mashtaka imeandikwa dhidi yake (b)mtumishi wa umma amepewa nafasi ya kujibu mashtaka hayo
(c)Maombi yametolewa kwenye hati ya mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizo chini ya kifungu namba 34.
Swali la kumuuliza Waziri Nyalandu, je, hatua hizi zilifuatwa katika kuwasimamisha kazi wakurugenzi hawa? Na je, maamuzi yake ya kumfukuza Prof. Songoro katika vikao vya kamati na kumdhalilisha hata baada ya Ikulu kutoa maagizo ya Wizara kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za kufukuza watumishi kazi ni utawala bora?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali na Wizara kuhakikisha kuwa, uamuzi wowote uliofanywa na kuendelea kufanywa katika kutekeleza maazimio ya Bunge katika kuwawajibisha watumishi hao uzingatie sheria, taratibu na kanuni kwa kuwa Sheria na Kanuni hizo zinaeleza wazi hatua zinazopaswa kuchukuliwa. Vilevile, tunasikitishwa na mvutano baina ya waziri na katibu mkuu wa wizara, hali ambayo inaonesha kuwa kuna mgongano aidha wa kimaslahi na hivyo kuthibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa, Waziri na Katibu Mkuu wa wizara moja wanafanya kazi bila kushirikiana na kila mmoja akionekana kumvizia mwenzake hadharani badala ya kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge lako tukufu.
Aidha, mvutano huu pia ni ishara kuwa, maazimio ya Bunge yanaendelea kupuuzwa na Serikali kwa kigezo cha kuzingatia sheria na kanuni huku zikiwaacha watumishi wenye tuhuma wakihamishwa vitengo na idara na kuendelezea urasimu uleule hata uko wanapohamishwa.
Mheshimiwa Spika, ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi mnafiki na debe tupu haliachi kutika (si maneno yangu, bali ya wahenga). Si mara ya kwanza, kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhoji juu ya usafi wa Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii, na mara kadhaa tumeonesha kwa kiasi kikubwa udhaifu wake na kutoa vielelezo mbalimbali  vinavyotilia shaka utendaji wake kabla na hata baada ya kukabidhiwa wizara hii nyeti!
3.0 TASWIRA YA TAIFA KATIKA JUMUIA ZA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani imeendelea kutoa taarifa kwa Serikali juu ya mtandao wa kimataifa wa ujangili ambao pia unahusisha viongozi waandamizi wa Serikali, maafisa usalama wa taifa, wanajeshi wafanyabiashara wakubwa, polisi, wanasiasa, Ikulu na watumishi wa umma. Serikali ya CCM imekua ikitoa kauli za kubeza pamoja na majibu mepesi ya tuhuma hizi huku tatizo la ujangili likiendelea kulichafua taifa katika jumuia ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kushangaza baada ya gazeti la Mail on Sunday la nchini Uingereza kutoa taarifa kuwa biashara ya ujangili inahusisha watu wa karibu na Rais wakiwemo  wanasiasa, maafisa wa Serikali na wafanya biashara wakubwa, Serikali ilitoa matamko mbalimbali pamoja na kulaani taarifa ya gazeti hilo na hatimaye Waziri Nyalandu, alimwalika mwandishi wa gazeti hilo kujionea mwenyewe shughuli za Serikali za kupambana na ujangili ikiwemo kutembembelea ghala ya kuhifadhia pembe za ndovu zilizokamatwa. Mwaliko huo ilikua ni katika kuthibitisha kuwa Serikali ya CCM haina la kuficha.
Lakini katika hali ya kushangaza, uchunguzi na taarifa zaidi umeonesha kuwa ndani ya miaka minane (8) Serikali ya CCM, imekua ikiomba kibali bila mafanikio kutoka CITES (Convention on International Trade on Endangered Species) cha kuuza shehena ya pembe za ndovu takribani 34,000 zenye uzito wa tani 125 zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 150 sawa na shilingi Bilioni 244.5 za kitanzania (kwa wastani wa sh.1630 kwa dola 1).
Mheshimiwa Spika, jumuia ya kimataifa imeshangazwa na kitendo cha Tanzania kuomba kibali cha kuuza shehena iliyokamatwa ya pembe za ndovu kwa kuwa ni biashara haramu na kitendo cha Serikali kuomba kuyauza ni sawa na kuchochea ujangili zaidi kwa kuwa hali hii itaongeza uhitaji wa pembe za ndovu kwenye soko haramu nchini China.  Jambo hili ni aibu kubwa kwa taifa kuomba kufanya biashara haramu kwa kuwa imelidhalilisha taifa. Hii ni sawa na Serikali ikamate madawa ya kulevya, halafu iamue kuyauza ili kupata fedha.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha waziri wa maliasili na utalii kumwalika nchini mwandishi aliyesemwa kuwa ametoa taarifa za uongo na kulichafua taifa, ili ajithibitishie kuwa Tanzania ni safi katika matukio ya ujangili, Bwana Martin Fletcher, na kumtembeza katika sehemu mbalimbali nchini ikiwa na nia ya kumfunga mdomo(damage control), haikusaidia bali ilivumbua uchafu mwingi na huu wote umewekwa wazi katika vyombo vya habari vya kimataifa na kuendelea kuonesha uozo wa Serikali katika kushughulikia tatizo la ujangili nchini.
Mheshimiwa Spika, imeelezwa kuwa Raisi ameshindwa kusimamia suala hili vizuri kwa kuwa wanaohusika na ujangili ni watu wake wa karibu ama rafiki zake. Aidha, taarifa hizo zimeendelea kubana kauli za Waziri Nyalandu za kuwa anawafahamu majangili kwa majina na kuwataka majangili hao kuacha ujangili ama watawachukulia hatua za kisheria. Maswali yanayoulizwa, je, ni kwa nini waziri hawataji watu wanahousika na ujangili? Pili, inakuaje waziri anawajua kwa majina na hata sehemu wanazokaa, lakini anashindwa kuwachukulia hatua? Inakuaje waziri, awabembeleze watuhumiwa wakati kuna sheria, kanuni na taratibu za kuwachukulia hatua wahalifu? Ni nini kipo nyuma ya pazia katika kuwalinda na kuwaficha watuhumiwa wa ujangili?
3.1 Kukosekana kwa maafisa utalii katika balozi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kuna taarifa kuwa katika balozi zetu mbalimbali na muhimu  ulimwenguni kumekuwa hakuna maafisa utalii ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa wanaweza kuhakikisha kuwa tunapata watalii wa kutosha kwa ajili ya kuinua pato la taifa letu.
Mheshimiwa Spika, katika ubalozi wa Tanzania –Berlin ni kati ya balozi kubwa ulimwenguni ambao hauna afisa utalii pamoja na ukweli kuwa ubalozi huu unahudumia nchi nyingine za Poland,Austria,Hungary,Frankfut,Uswis,Romania,Bulgaria ,Slovakia na Jamhuri ya Czech , kwa kipindi kirefu sana ubalozi huu umeomba kupatiwa afisa utalii kutoka wizara ya mambo ya nje lakini mpaka leo hawajaweza kupelekewa maafisa hao kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya uchumi ambayo ndio msingi wetu wa diplomasia ya kimataifa .
Kambi ya Upinzani, inataka kupata majibu ni lini serikali itawapeleka wataalamu hao katika ubalozi huu kwa ajili ya kuimarisha sekta ya utalii kwenye nchi zote muhimu ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika sekta ya utalii katika taifa letu. 
4.0       BIASHARA HARAMU YA NYARA ZITOKANAZO NA WANYAMAPORI NA KUKITHIRI KWA TATIZO LA UJANGILI NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kumekuwa na ongezeko kubwa na watu wanaojishughulisha na uwindaji na biashara ya nyara za Serikali bila bila kuwa na kibali au leseni toka mamlaka zilizowekwa kisheria.  Kwa mujibu wa sheria ya wanyapori kifungu cha 80(1) sehemu ya 10 “mtu yeyote haruhusiwi kujihusisha na biashara ya nyara (trophies) bila kuwa na leseni ya biashara ya nyara (trophy dealer license). Na kifungu cha 80(2) kinampa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori mamlaka ya kutoa leseni  ya biashara ya nyara kwa mtu yeyote  ambaye ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupokea maombi kwenye fomu maalum na kutimiza masharti yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kulipa ada zilizopangwa.
Mheshimiwa Spika, leseni ya biashara ya nyara inayotolewa katika Kifungu hiki haimruhusu mhusika kuwinda, kuua au kupiga picha mnyama yoyote, badala yake inamruhusu kukamata, kutengeneza bidhaa inayotokana na nyara, kununua au kuuza nyara – 80(3)”[2].
Mheshimiwa Spika, licha ya kuwepo kwa sheria hiyo, bado wanyama wetu wanaendelea kuuwawa kwa kasi ya ajabu. Aidha, kumekuwepo kwa taarifa zinazoonyesha kuwepo kwa mtandao mpana wa wahusika wa biashara ya wanyama pori na bidhaa za wanyamapori kutoka katika nchi kadhaa kama vile, Kenya, Msumbiji, DRC, Namibia na Afrika ya Kusini.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu aliyoyatoa mbele ya Waandishi wa Habari  wakati akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii  katika Hoteli ya Mount Meru – Arusha mwaka jana, ni kwamba; kwa kipindi cha miaka mitatu, iliyopita tembo 31348 sawa  na asilimia 42 walitoweka katika hifadhi ya Selous na Mikumi  na kwamba kuna mtandao wa kijangili  wa kimataifa (Sophisticated International Syndicate)  unaofanya kazi hapa nchini. Aidha alitoa agizo kwa bodi ya wadhamini ya mamlaka ya hifadhi za taifa (TANAPA) itoe maelezo ya kina kuhusu kuwepo watumishi wa ndani ya mamlaka ya hifadhi wanaosadikiwa kushirikiana na majangili hao kuendesha ujangili ambao unahatarisha hifadhi zetu na sifa ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,  Waziri Nyalandu aliirudia kauli hiyo  mkoani Iringa, mwezi  Juni, 2013  wakati wa kikao cha siku mbili cha wadau wa ulinzi wa maliasili juu ya ujangili wa tembo katika mikoa ya Nyanda za juu na  kuahidi kwamba majina ya majangili  yakiwemo ya vigogo wanaojihusisha na ujangili wa tembo yatatangazwa hadharani, lakini mpaka sasa hakuna majina yoyote yaliyotangazwa hadharani.
Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa na Tanzania Wildlife Research Institute-TAWIRI katika mbuga ya hifadhi ya Selou na Mikumi inaonyesha kuwa idadi ya Tembo imeshuka kutoka 74,900 mwaka 2006 hadi kufikia 43,552 mwaka 2009. Hii ikiwa na maana kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu takribani asilimia 42 ambayo ni Tembo 31,348 katika hifadhi mbili tu waliuawa na majangili[3]. Hii ni hatari kubwa sana na kwa kutilia maanani kuwa Tembo mmoja anapatikana baada ya miaka miwili (yaani Tembo hubeba mimba kwa kipindi cha miaka miwili ndipo azae)
Mheshimiwa Spika, biashara haramu ya nyara zitokanzao na wanyamapori hususan tembo imechangia sana ujangili wa kutisha wa tembo kiasi kwamba idadi ya tembo imepungua mno kiasi cha kuwafanya tembo wawe miongoni mwa jamii ya viiumbe waliopo hatarini kutoweka kabisa (endangered species). Nasema hivi kwa sababu idadi ya tembo  kwa uchache,  waliokuwepo katika nchi za Kiafrika kwa miaka ya sabini walikuwa ni takribani  milioni moja na laki mbili  (1,200,000) lakini kwa sasa wamebakia wasiozidi laki tano[4]
Mheshimiwa Spika, hali ya ujangili nchini imefika pabaya na ina kiasharia kibaya kwa miaka michache ijayo. Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010, jumla ya tembo 10,000 waliuwawa Tanzania, ikiwa ni sawa na wastani wa tembo 27 kwa siku. Mwaka 2012 pekee, tembo takribani 23,000 wameuwawa kwa mwaka ambayo ni sawa na tembo 63 kwa siku. Hii ni sawa na ongezeko la 57% kwa kipindi cha miaka 2. Kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na tembo kati ya 150,000 na 170,000.  Kutokana na takwimu hizi, ikiwa Tembo 63 wanauwawa kwa siku, ni dhahiri kwamba  kwa kipindi cha miaka 7 ijayo  Tembo hawa watakuwa wameuawa wote.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kupamba na madawa ya kulevya na uhalifu (United Nation’s Office on Drugs and Crime- UNODC-), inaonyesha kuwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara  na nchi za Kusini Mashariki mwa Asia  ni wasambazaji wakubwa wa bidhaa haramu za wanyamapori kwenye soko la China, Marekani na baadhi ya nchi katika bara la  Ulaya. Bidhaa hizo za wanyamapori ni pamoja na pembe za ndovu, pembe za faru, ngozi za chui na simba na viungo mbalimbali vya wanyamapori. Kwa mujibu wa utafiti huo ni kwamba mununuzi hulipa kiasi cha dolla za kimarekani 2,500 kwa kila pembe moja ya faru.
Mheshimiwa Spika, tatizo la Ujangili limekuwa gumu kumalizwa kabisa kwa kuna taarifa zinazohusisha askari wa Jeshi la  Polisi na Jeshi la Wananchi katika matukio ya ujangili na biashara haramu ya nyara na taarifa hizo zimeripotiwa sana na vyombo vya habari, lakini cha kusikitisha ni kwamba hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari wa majeshi hayo (yaani jeshi la polisi na jeshi la wananchi wa Tanzania). Mpaka sasa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania hawajakanusha taarifa hizo jambo linaloashiria kwamba pengine taarifa hizo ni za kweli.
Mheshimiwa Spika, taarifa za baadhi ya askari walioripotiwa na vyombo vya habari kuhusika na ujangili ni kama ifuatavyo:
  1. Mnamo Tarehe 7 January 2013, Gazeti la habari leo lilitoa taarifa za askari wawili kujihusisha na biashara ya meno ya tembo na kuhusishwa na mauaji ya faru katika mbuga ya Serengeti na mpaka sasa hakuna taarifa rasmi kutoka Serikalini juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari hao.
  1.  Mnamo Januari 20, 2013 Sajenti wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Azizi Athuman Yusufu alikamatwa mkoani Arusha akiwa na pembe mbili za ndovu na bunduki aina ya Riffle yenye namba 458 huku akitumia gari ya mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe anayefundisha nchini.
  1. Tarehe 23 Julai, mwaka 2013, walikamatwa watu saba wanaodhaniwa kuwa ni majangili , wakiwamo askari watatu wa Magereza Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wakiwa na  gari la Magereza  aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili STK 4394 lililokuwa limepakia   nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55. Nyara hizo zilikuwa ni pamoja na Twiga wawili, Pundamilia wawili, Swala, Palapala majike wawili na Mbuni wawili.
Mheshimiwa Spika, Biashara haramu ya pembe za ndovu imevuka mipaka ya nchi na imeanza kushamiri katika ukanda wa Afrika ya Mashariki jambo ambalo linatishia kutoweka kabisa kwa wanyama hao ambao ni kivutio kikubwa cha utalii. Taarifa katika mtandao wa habari wa “Annamiticus” (www.annamiticus.com) zinasema kwamba mwaka 2012, makontena mawili kutoka Kenya na Tanzania yalikamatwa huko HongKong yakiwa yamebeba tani 4 (Kilo 4,000) za pembe za ndovu. 
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kontena lililotoka Tanzania lilikuwa limeandikwa “plastic scrap” ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya plastiki lakini baada ya kufunguliwa kulikuwa na vipande 972 vya pembe halisi za ndovu zenye uzito wa kilogramu 1,927 pamoja na kilo moja na nusu ya unga wa pembe za ndovu zilizosagwa. Kontena lililotoka Kenya lilikuwa limeandikwa “roscoco beans” yaani maharage aina ya roscoco, lakini lilipofunguliwa kulikuwa na vipande 237 vya pembe za ndovu sawa na kilogramu 1,884.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo, wingi wa pembe hizi za ndovu zilizokamatwa, unadhihirisha kwamba tembo takriban 600 kwa uchache waliuwawa.
Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili,2013   kontena lingine lilikamatwa likiwa limesheheni pembe za ndovu 113 huko China zenye thamani ya Dola za Kimarekani 400,000.Kontena hili liliandikwa kwamba limebeba vipuri (spareparts) toka Burundi. Kwa kuwa Burundi haina bandari, kuna uwezekano mkubwa kwamba kontena hilo lilipitia bandari ya Tanzania, na hivyo kuna uwezekano pia kwamba pembe hizo zinatokana na tembo waliouwawa Tanzania.
5.0       MAENDELEO YA SEKTA YA WA WANYAMAPORI NCHINI
Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta ya wanyamapori katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu ni mkubwa sana. Takwimu[5] zinaonyesha kuwa uwindaji wa kitalii kwa miaka mitatu kati ya 2009 na 2012 uliingiza shilingi bilioni 91. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia idara yake ya Wanyamapori inatakiwa kuilinda na kuiendeleza sekta hii ili iendelee kuchangia zaidi katika uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, katika muktadha wa kuilinda na kuiendeleza sekta ya wanyamapori, Bunge lilitunga Sheria ya Uhifadhi ya 2009, ambayo inatumika pamoja   na sera ya wanyamapori ya mwaka 2007 ili kuratibu na kudhibiti shughuli za uwindaji wa wanyamapori kwa namna ambayo sekta ya wanyampaori inakuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, ulinzi wa Sekta ya wanyamapori ni muhumu kwa kuwa sekta inachangia ukuaji wa uchumi katika Nyanja mbalimbali. Kwa mfano wanyamapori ni kivutio kikubwa cha watalii ambao hutoa fedha nyingi za kigeni wajapo kutalii hapa nchini kwa ajili ya kutazama na kuwapiga picha wanyama hao. Aidha sekta ya wanyama pori inachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutoa ajira kwa wananchi na pia kukuza soko la bidhaa za ndani. 
Mheshimiwa Spika, licha ya umuhimu wa sekta hii, Serikali imekuwa haifuatilii makampuni ya uwindaji yenye leseni kuona kama wanafuata sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya 2009. Matokeo ya udhaifu wa Serikali katika ufuatiliaji, kumekuwa na uvunjaji mkubwa wa sheria jambo ambalo limesababisha uwindaji ufanyike kiholela. Kwa mfano, Kampuni ya Uwindaji ya Green Miles Safaris Limited imekuwa ikiwakimbiza na kuwakamata watoto wa wanyamapori pindi wanapozaliwa kinyume na kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Wanyamapori ya 2009. Aidha Sheria hiyo inapendekeza adhabu ya kifungo cha miaka mitano gerezani na au faini kati ya shilingi 500,000/= hadi shilingi 2,000,000/=
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataarifa kwamba Kampuni hii ya Green Miles Safaris Limited ilishapewa zuio na Mahakama la kufanya uwindaji kutokana na uwindaji usiozingatia sheria lakini Kampuni hiyo ilipita mlango wa nyuma na kuomba kilbali cha uwindaji kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori na Mkurugenzi  akatoa kibali na hivyo wote wawili wakapuuza uamuzi wa Mahakama.
Mheshimiwa Spika, Kampuni hii ya Green Miles Safaris Limited, pamoja na uhalifu mwingi inaoufanya katika mbuga zetu wakati wa uwindaji, imekuwa ikilindwa na Serikali ndio maana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Upinzani Bungeni inashawishika kuamini kwamba Serikali ndio chimbuko la tatizo la Ujangili na uwindaji haramu wa wanyamapori hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo mbele ya bunge hili ni kwa nini haijaichukulia Kampuni ya Uwindaji Green Miles kwa kufanya uwindaji haramu hapa nchini?
Mheshimiwa Spika, Tatizo kubwa la Maendeleo ya Sekta ya Wanyapori ni kwamba Serikali huwa haifuati hata mapendekezo yanayotolewa na Kamati za zinazoudwa na Serikali yenyewe. Kwa mfano, mwaka 2006, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa wakati huo Mheshimiwa Anthony Mwandu Diallo (Mb), aliunda Kamati ya Wataalam ambayo aliitaka ifanye uchambuzi wa kina wa shughuli za uwindaji wa kitalii nchini. Uchambuzi huo ulitakiwa uzingatie utendaji kazi katika shughuli za uwindaji wa kitalii, mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa na matatizo yanayoikabili tasnia hiyo. Hatimaye, Kamati ilitakiwa kumshauri Mheshimiwa Waziri namna ya kuleta mabadiliko ndani ya sekta hiyo kwa minajili ya kulinda uhifadhi, kuwawezesha wananchi kushiriki katika uwindaji wa kitalii kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuondoa umaskini na kuongeza Pato la Taifa. 
Mheshimiwa Spika, Hadidu za rejea kamati hiyo ilizopewa ziliitaka Kamati:[6]
(i)  Ipitie utaratibu wa sasa wa uombaji na ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii pamoja na chombo chake cha ugawaji kuona kama havibagui wala havisababishi malalamiko kwa wadau mbalimbali;
(ii)                                     Ichambue kwa makini vigezo na masharti yaliyopo yanayohusu ukaguzi wa uwezo wa Kampuni za Uwindaji zinazowasilisha maombi kwa ajili ya Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama yanafaa kwa mazingira ya sasa;
(iii)                                   Ichambue Mikataba mbalimbali ya kampuni za uwindaji; ya zamani na inayoendelea kwa lengo la kujiridhisha kama inafaa au ina upungufu unaohitaji marekebisho ili kulinda uhifadhi na maslahi ya umma.
(iv)                                  Iangalie Kanuni za Uwindaji wa Kitalii na zile za Utalii wa picha pamoja na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974 na kushauri namna ya kuondoa migongano ambayo imejitokeza baada ya kuruhusu utalii wa picha kwenye maeneo ya uwindaji wa kitalii.
(v)                                    Ichambue Sera na Sheria zinazohusiana na Wanyamapori na Utalii, na Kanuni za Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama Wananchi wanafaidika na uwindaji huo wa kitalii.
(vi)                                  Ichambue utaratibu wa ukusanyaji mapato, kubaini njia ambazo zitaongeza maduhuli ya Serikali, na kutathmini utaratibu wa ugawaji vitalu kwa njia ya zabuni.
(vii)                                Mwisho, Kamati iangalie uwezekano wa Serikali kuwawezesha Wananchi kushiriki kikamilifu katika tasnia hii ya uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Kamati hiyo yalikuwa ni kama ifuatavyo:
  1. Kuboresha utaratibu wa ugawaji wa vitalu kwa kuipa Kamati ya Ugawaji Vitalu nguvu za kisheria na kwa kupanua uwakilishi wake.
  2. Kuunda Wakala wa Serikali wa kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii badala ya Idara ya Wanyamapori.
  1. Kuangalia upya umiliki wa vitalu ili kuwawezesha wananchi kushiriki zaidi katika uwindaji wa kitalii kwa njia ya ubia na baadaye kumilikishwa vitalu wakati wageni na wananchi watafanya kazi ya kuwindisha.
  1. Serikali iwawezeshe Wawindaji Bingwa wa Kitanzania ili waweze kumiliki vitalu na kutumia ujuzi na uzoefu walionao. Serikali inaweza kuwawezesha wananchi kwa kuzungumza na mabenki ili wapunguze riba ya kukopa fedha benki na kuruhusu matumizi ya vitalu kama dhamana. Pia wawindaji bingwa waanzishe bodi yao ya kitaalam.
  1. Kuthamini vitalu vya uwindaji wa kitalii na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato ya Serikali.
  1. Kuweka ukomo wa umiliki wa kitalu wa vipindi viwili vya miaka mitano ili ili kuruhusu waombaji wapya.
  1. Kuboresha taarifa za sekta ya Wanyamapori kwa kuweka taarifa zote muhimu zinazohusu shughuli za uwindaji wa kitalii kwenye Tovuti ya Idara.
  1. Idara iimarishe ufuatiliaji na tathmini ya vitalu kwa kuanzisha chombo huru cha kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni  kwa kiwango gani mapendekezo ya Kamati hiyo yametekelezwa  na ni mangapi ambayo bado kutekelezwa na ni kwanini?

6.0       UTALII NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA
Mheshimiwa Spika,
Kwa eneo kubwa la ardhi lililofunikwa na wingi wa misitu pamoja na aina mbalimbali za maua na viumbe, Tanzania  ni mojawapo ya vivutio vikubwa vya utalii barani Afrika. Nchi yetu ina raslimali nyingi asilia ikiwemo pamoja na maeneo mengi ya nyika za mapori yenye aina nyingi za banoai.
Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa vivutio vya utalii ni pamoja na Mbuga za wanyama , hifadhi za taifa, hifadhi zilizozuiliwa na  maeneo ya kihistoria. Hata hivyo kwa sababu ya ongezeko la joto, baadhi ya hivi vivutio ikiwemo theluji katika kilele cha mlima Kilimanjaro iko katika hatari ya kupotea. Na baadhi ya wanyama katika mbunga zenye ukame mkubwa wameanza kupungua na kuathirika.
Mheshimiwa Spika, Licha ya kuwa na neema ya kuwa na vivutio vingi vya utalii, bado sekta ya utalii inakabiliwa na chamgamoto kadhaa, zikiwa ni;
(i)   Uendelezaji wa kazi zitakazohakikisha kuendelea kuwepo kwa vivutio mbalimbali vya utalii kwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi;
(ii) Ukarabati wa miundombinu kama vile barabara, madaraja, kambi za watalii na upatikanaji wa umeme kwa ajili ya watalii wa mbugani;
(iii)                       Uwezo mdogo wa idara zinazohusika kusimamia, kulinda vivutio vya utalii, kama vile kuendesha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, inaamini kabisa tatizo la umeme katika vivutio vya utalii vilivyopo mbugani, suluhisho ni kutumia umeme wa jua (solar energy), hili ni rahisi katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nitaonyesha hapo baadae makusanyo yanayopatikana kutoka sekta ya utalii hayana uwiano wa moja kwa moja na uwekezaji katika sekta hiii. Ndiyo sababu kubwa ya mapato ya sekta kutokuakisi vivutio tulivyonavyo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika Sekta ya Utalii ni suala lenye tija kubwa katika uchumi wetu kwa kuwa sekta hiyo imekuwa ikichangia katika uchumi wa Taifa licha ya uwekezaji mdogo uliofanyika katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonyesha  kuwa katika maeneo yote  ya hifadhi zetu kwa sasa kuna  kuna hoteli zenye uwezo wa kutoa huduma za malazi (carrying capacity)  kwa watu 6,681 ambapo kwa miaka mitano ijayo idadi hii itafikia uwezo wa kulaza watu 8,421. Hiki ni kwango kidogo sana cha huduma za malazi kiasi kwamba tunapoteza fursa ya kunufaika katika sekta ya utalii. 
Mheshimiwa Spika, japokuwa uwekezaji katika sekta ya utalii ni mdogo lakini sekta imeendelea kuwa nguzo muhimu katika uchumi wetu. Kwa mwaka 2011 utalii na usafiri wa kitalii ulichangia asilimia 13 kwenye pato la taifa na kuchangia takriban asilimia 25 ya fedha za kigeni. Aidha, Mpango unaeleza kuwa lengo ni kuongeza wageni kwa asilimia 40 kutoka   wageni 671,886 kwa sasa hadi 940,640 ifikap June 2016. Aidha Mpango unalenga pia kuzidisha siku za mtalii kutembelea maeneo yenye vivutio vya kitalii nchini kutoka siku wastani wa siku 11 za sasa hadi wastani wa siku 18[7].
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa tathmini ya mpango huo ili wananchi wajue tumefanikiwa kwa kiwango gani katiaka kuboresha sekta ya wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ya ndani ya nchi, uwekezaji katika ujenzi wa hotel kwenye maeneo muhimu ya utalii kama vile kwenye hifadhi, mikoa inayozunguka mlima Kilimanjaro kutasaidia sana kuvutia watalii. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuboresha miundo mbinu ya usafiri hasa wa anga ili na kujenga hoteli za viwango vya Kimataifa katika maeneo yenye vivutio vya watalii ili kuvutia mashirika ya mengi ya ndege toka nje kuja hapa.
Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Serikali kwamba ifufue shirika letu la Ndege la Taifa ili tuweze kumudu ushindani katika usafiri wa anga na hapohapo kuongeza idadi ya watalii katika nchi yetu. Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na ule wa Julius Nyerere Dar es Salaam vikiboreshwa vinaweza kuwa ni kitovu cha mashirika mengi ya kimataifa kubadilishia wasafiri kama kuna mkakati makini.
Mheshimiwa Spika, watalii toka nje wanapenda sana kupanda ndege za nchi wanazotembelea zaidi kuliko kupanda ndege za kuunganisha. Kwa njia moja au nyingine usafiri huo unawapunguzia gharama. Mfano mzuri ni miaka ya themanini wakati Air-Tanzania ilipokuwa inafanya safari zake nchi za Ulaya, watalii wengi walikuwa wanakuja kwa ndege zetu. Hoja ni kwamba Serikali ina mkakati gani wa kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATC) Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza Serikali kuingia ubia na makampuni binafsi kupitia mpango wa Private Public Pertnership – ( PPP) ili kuboresha huduma za usafiri wa anga hapa nchini ambao unachoche watalii wengi kuja kwa kuwa kuna usafiri wa moja kwa moja.
7.0       SEKTA YA MISITU
Mheshimiwa Spika, misitu ina nafasi muhimu ya kumeza hewa ukaa duniani wakati ikizuia uharibifu wa udongo/ardhi. Ukataji miti na uondoaji misitu uliokithiri unachangia katika ongezeko la uzalishaji wa hewa ukaa Tanzania. Kupitia misitu mingi tuliyonayo Tanzania imeendelea kutoa huduma ya kumeza hewa ukaa duniani, bila ya kuwepo utaratibu wowote wa kimataifa kutoa fidia yoyote.
Mheshimiwa Spika, mbali ya kuwa na misitu mingi, kumekuwepo na changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya misitu, nazo ni:
a)  Kufanya uendelezaji wa misitu kama raslimali ya kumeza hewa ukaa na kuinufaisha jamii inayoizunguka;
b)  Kuthibiti ubora na uendelevu wa misitu
c)   Jamii inayoizunguka misitu kunufaika na biashara ya hewa ukaa duniani;
d)  Ujenzi wa uwezo wa kufanya tafiti za uendelezaji misitu nchini;
e)   Uendelezaji wa njia bora zinazowezesha jamii inayozunguka misitu kunufaika na raslimali hiyo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hizo, zinazoikabili sekta hii ya misitu, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka kuhakikisha kwa kadri misitu ya Tanzania inavyoendelea kutoa huduma ya kimataifa ya kumeza hewa ukaa duniani, hivyo ni lazima nchi na wananchi wetu tunufaike kwa kupata kazi na teknolojia zinazochangia maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni kwamba, ni muhimu Serikali kuhakikisha unajengwa uelewa kwa jamii na wadau wa misitu juu ya uwepo wa fursa za kutumia uwezo wa misitu kumeza kumeza hewa ukaa kama chanzo cha kunufaika na biashara ya hewa ukaa duniani. Kuhamasisha ongezeko la matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati ya kupikia na kuchemshia na kupunguza msongo kwenye misitu yetu kwa hitaji hilo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa katika kuhamasisha hilo, ni muhimu kuwepo kwa misitu mfano na miradi mfano katika ngazi za wilaya na vijiji ili wananchi waone jinsi misitu inavyoweza kuwanufaisha wananchi wanaozunguka misitu mfano hiyo. Hili linawezekana kama mipango na umakini katika utekelezaji wake utakuwepo. 
Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika kilimo cha miti ni mojawapo ya kilimo ambacho kwa muda mrefu kinaweza kuleta tija kubwa kwa wananchi hasa hapa nchini, uwekezaji huu unakabiliwa na chamgamoto kubwa ya kukosekana kwa mikopo ya muda mrefu na ambayo inaweza kuwa-accommodate wakulima ambao hawana dhamana ya kuweka zaidi ya umiliki wa kimira wa ardhi husika, jjambo ambalo halikubaliwi na taasisi za fedha.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huu wa kilimo cha miti ni maarufu sana katika mikoa ya Iringa na Njombe, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni utaratibu gani hadi sasa ambao wakulima wadogo hasa wa miti wanasaidiwa kupata mikopo ya muda mrefu katika kukabiliana na tatizo hili la uwepo wa hewa ukaa na kuongeza kipato.
8.0       MAPITIO YA BAJETI KWA IDARA NA VITENGO VYA WIZARA
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14 wizara ilitarajia kukusanya maduhuli ya jumla ya shilingi bilioni 148.97 kutoka katika Idara na taasisi zilizo chini yake. Mwaka huu wa fedha wizara inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 144.6, ambayo ni pungufu ya shilingi bilioni 4.37 kwa kulinganisha na makadirio ya mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika, randama inaonyesha kuwa Idara ya wanyamapori kwa kipindi cha mwaka 2013/14 ili kadiriwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.65,  Lakini hadi mwezi Machi, 2014 ilikuwa imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 8.92 ambayo ni sawa na asilimia 31.13 ya malengo. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2014/15 Idara ya Wanyamapori imepanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 15.55 kutoka kwenye vyanzo vyake vilivyo chini ya idara. Makadirio haya ni pungufu ya shilingi bilioni 13.1 kwa kulinganisha na mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo ni kwamba Sekta  ya Maliasili na Utalii inashuka kimapato. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza sababu zilizofanya mapato yatokanayo na makusanya ya maduhuli kwa shuka kwa kiasi kikubwa namna hiyo. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na taarifa ya uchunguzi maalum ni kwamba kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2012 Idara ilikusanya shilingi bilioni 91 na hali halisi ni kwamba uwezekano kukusanya zaidi ni mkubwa zaidi. 
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya kawaida, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 19.163 kwa ajili ya matumizi ya Idara hiyo, ambayo ni sawa na asilimia 22.7 ya makusanyo yake. Lakini hadi mwezi machi 2014, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 9.161 tu. Swali hapa ni kwamba idara itawezaje kujiendesha ikiwa fedha iliyotolewa ni kidogo namna hiyo? Ikumbukwe kwamba Idara hii inasimamia taasisi/vyuo na wakala zipatazo sita ambazo ni TANAPA, NCAA, TAWIRI,CAWM-Mweka, PWTI na CBCTC ambazo zinahitaji fedha za kutosha kuziendesha.
 Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwenye sekta ya wanyamapori, ni kwa miradi miwili tu ambayo ni mradi wa KILORWEMP unaotekelezwa kwa ushirika kati ya Tanzania na Serikali ya Ubelgiji. Mwaka 2013/14 zilitengwa jumla ya shilingi bilioni 1.82, lakini hadi Machi 2014 shilingi milioni 310 ambazo zilitoka Serikali ya Ubelgiji.
Mheshimiwa Spika, mradi wa pili ni ule wa Kulinda ushoroba wa Selous-Niassa, ambao unatekelezwa kwenye wilaya za Namtumbo na Tunduru kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani. Kwa mwaka jana hakuna fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14 Idara ya Utalii ilikadiriwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 16.896 lakini hadi mwezi mach, 2014 ilikuwa imekusanya shilingi bilioni 3.25 ambayo ni sawa na asilimia 19 tu ya matarajio kwa mwaka. Aidha, fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida kwa idara na Taasisi zilizo chini yake ni shilingi bilioni 12.1, lakini hadi Machi, zilikuwa zimetolewa shilingi bilioni 3.36.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2014/15 idara hii ya Utalii inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 16.91. Aidha, kwa maendeleo Iadara hii imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.2. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza inakuwaje Idara inakusanya shilingi bilioni 16.91 lakini uwekezaji unakuwa wa shilingi bilioni 1.2, aidha uwekezaji huo hauna matokeo ya moja kwa moja na ukuaji wa utalii. Je ni kwa vipi katika Dunia hii ya ushindani katika sekta ya utalii inaweza kuleta tija na kuinua uchumi?
9.0       HITIMISHO
Kambi Rasmi ya Upinzani, haitochoka kuikosoa Serikali kwa kuwa, kwa muda mrefu sasa katika Wizara hii tumekua tunatoa mapendekezo ambayo yanabezwa. Na kwa kuwa ni wajibu wetu kuisimamia ipasavyo Serikali ya CCM, tunazidi kusisitiza kuwa ili sekta ya maliasili na utalii iendelee kuna haja nzima ya kubadilisha mfumo wa usimamizi, uendeshaji na utekelezaji wa Wizara, ambao utatoa fursa kwa viongozi waandamizi wa Wizara pamoja na watumishi kutimiza na kutekeleza majukumu yake bila mashinikizo ya kisiasa.
Ni rai yetu kuwa, Serikali itayafanyia kazi mapungufu yote ambayo tumekua tukiyasema kwa muda mrefu sasa na kuisimamia ipasavyo sekta hii hili iwe mhimili wa uchumi kwa taifa kwa kuongeza mapato pamoja na kutoa nafasi za ajira kwa wananchi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
…………………………………………..
Mch. Peter S. Msigwa (MB)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Maliasili na Utalii.
13.05.2014

[1] ripoti ya CAG 2012/2013 pg 148.
[2] Sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009
[3] www.reuters.com/video/feuters-tv
[4] Haken, J. (2011), “Transnational Crime in the Developing World” in the Global Financial Integrity Journal of February, 2011.
[5] Ripoti ya CAG-ukaguzi wa ufanisi na ukaguzi maalum kwa kipindi kinachoishia tarehe 31 Machi, 2014
[6] Wizara  ya  maliasili  na  utalii- Taarifa  ya  kamati kuhusu  uboreshaji  wa  tasnia  ya uwindaji  wa  kitalii  Tanzania, JUNI, 2006
[7] Mpango wa Taifa  wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011 – 2016

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa