Home » » TAARIFA: 3 WATIWA MBARONI KWA KULIMA BHANGI HEKARI SITA NA NUSU,NA WENGINE 34 MBARONI KWA KUFANYA FUJO NA KUHARIBU MALI KIBAIGWA

TAARIFA: 3 WATIWA MBARONI KWA KULIMA BHANGI HEKARI SITA NA NUSU,NA WENGINE 34 MBARONI KWA KUFANYA FUJO NA KUHARIBU MALI KIBAIGWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME - SACP
Na: Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu 34 wakazi wa Mji mdogo wa Kibaigwa Kata ya Kibaigwa Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma kwa makosa ya kufanya fujo na kuharibu mali tukio lililotokea tarehe 05/05/2014 majira ya saa 13:30Hrs.

Kamanada wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema Vijana wanaokadiriwa kuwa zaidi ya miatatu wakishirikiana na Wabeba mizigo wa Soko Kuu la Mazao la Kibaigwa, walifanya maandamano bila kibali na kung’oa bango la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa lenya tangazo la kutoruhusu wafanyabiashara kuingiza mazao sokoni bila kulipa ushuru uliowekwa kwa mujibu wa sheria. Viwango vya ushuru vinavyotozwa vilipanda tangu tarehe 01.07.2013 ambapo gunia la Kg. 100 za karanga zilipanda kutoka Tshs. 1000/= hadi Tshs 3000/=, guina la mahindi lilipanda kutoka Tshs. 500/= hadi Tshs. 1000/=, dumu la mafuta ya alizeti lilianza kutozwa Tshs. 500/=, gunia la mashudu lilianza kutozwa Tshs. 1000/=, gunia la alizeti lilianza kutozwa Tshs. 1000/= ushuru ambao unapingwa na wabeba mizigo.

Vijana  hao wabeba mizigo walifanya fujo kwa kufunga barabara kuu ya Dodoma – Morogoro kwa mawe na kuchoma mataili, pia walivamia maduka na bar za jirani na kupora vinywaji na kuvunja majokofu.

Kamanda MISIME amesema katika vurugu hizo walisababisha uhalibifu wa mali kwa kushambulia magari kwa mawe likiwemo gari la Mbunge wa Tanga Mh. OMARI NUNDU lenye namba za usajili T.419 CWC Land Cruiser Prado ambaye aliyekuwa akienda Bungeni Dodoma, pia gari la Polisi namba PT. 0960 Land Rover lilivunjwa kioo cha mlango wa mbele kulia na basi la Kampuni ya Shabaha lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam lilivunjwa kioo cha mbele.

Kamanda MISIME amesema chanzo cha vurugu hizo ni wabeba mizigo wa soko la mazao kibaigwa kupinga kitendo cha Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuweka tangazo la kutoza ushuru wa mazao sokoni hapo wakidai kwamba linawakosesha kufanya kazi zao kwani wateja wanashindwa kuingiza mazao sokoni na wao kukosa kazi.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu kwa makosa ya kupatikana na Mashamba ya Bangi. LEONARD S/O RAMADHANI MTWANGU, miaka 53, kabila Mgogo, Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Ilolo Wilaya ya Mpawapwa alikamatwa akimiliki ekari tatu (3) za shamba la bangi kinyume cha sheria. Mtu wa pili ni MATONYA S/O MPARE mwenye miaka 24, kabila Mgogo mkazi wa Kijiji cha Matumbulu Manispaa ya Dodoma alikamatwa akimiliki nusu ekari ya shamba la bangi kinyume cha sheria na mtu mwingine ni EMMANUEL S/O LUHANGA mwenye miaka 45, kabila Mkaguru, Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Nguji Wilaya ya Kongwa ambaye alikamatwa akimiliki ekari tatu (3) za shamba la bangi kinyume cha sheria. Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika na msako unaendelea.

Kamanda MISIEME ametoa wito kwa wananchi wakazi wa Kibaigwa waache kujichukulia sheria mkononi, wafuate taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria. Kutokana na ushahidi uliopo wote waliohusika watakamatwa popote walipo na watafikishwa Mahakamani kwa makosa ya Kufanya mkusanyiko bila halali, Kuandamana bila kibali, kufunga barabara na kuharibu mali ambayo ni makosa kisheria.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa