Home » » TIKETI ZA NDEGE ZILIWEKEWA 'CHA JUU ' MARA 16 SERIKALINI

TIKETI ZA NDEGE ZILIWEKEWA 'CHA JUU ' MARA 16 SERIKALINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Ndege kubwa inavyoonekana kwa ndani.

Tuhuma nzito za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka zimezidi kuibuliwa katika ofisi nyeti za Serikali, ikiwamo ya tiketi za ndege kuuzwa kwa bei kubwa mara 16 zaidi ya nauli halisi.
Hayo yamo katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyotokana na ukaguzi maalumu wa hesabu za Serikali kwa kipindi kinachoishia Machi 31, 2014 iliyowasilishwa bungeni juzi.
Katika ukaguzi wake, sampuli 72 za tiketi za safari za nje zilichukuliwa katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Maliasili na Utalii na zilipofanyiwa uchunguzi, ilibainika kuwa 56 sawa na asilimia 72 zililipiwa zaidi na hivyo kupoteza Sh273.6 milioni za walipakodi.
Badala ya Serikali kulipa Sh700.9 milioni kwa mawakala wa usafiri wa anga, ililipa Sh974.5 milioni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, mawakala walitakiwa kutoza gharama ya huduma kama ilivyo katika mikataba ya Wakala wa Huduma za Ununuzi (GPSA), lakini walitoza viwango ambavyo ni zaidi ya vile vilivyoko kwenye mikataba na hivyo Serikali kulipa zaidi.
Sampuli ya tiketi 22 zilizochukuliwa kati ya safari 239 za maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zilionyesha pia kuwa, zilitozwa zaidi ya kiwango kilichokubaliwa.
Matokeo yake, taasisi za ununuzi zililipa Sh44 milioni badala ya Sh23.5 milioni na hivyo kusababisha malipo ya ziada ya Sh20.5 milioni ambayo ni karibu mara mbili ya gharama zilizotakiwa.
Ripoti hiyo inasema uchunguzi wa sampuli ya safari 229 kutoka kwa wakala mwingine kwenye wizara hiyo, unaonyesha kuwa pia zilitozwa zaidi ya kiwango kilichokubaliwa. “Baadhi ya tiketi zilitozwa zaidi ya mara 16 ikilinganishwa na bei iliyowekwa kwenye mkataba na GPSA… Nusu ya tiketi zilitozwa zaidi ya mara tatu ya bei iliyokubaliwa,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Matokeo yake, wizara hiyo ililipa Sh70.8
 milioni badala ya Sh18.8 milioni ikiwa ni ongezeko la Sh52.3 milioni, ambazo ni mara tatu zaidi ya kiwango kilichokuwa kwenye mikataba.
Ripoti hiyo ya CAG imebainisha kuwa kwenye sampuli ya tiketi 45 za safari za nje, kulikuwapo fursa ambayo ingemwezesha wakala kuchagua bei kati ya Sh488,250 hadi Sh46.3 milioni.
Hata hivyo, bei iliyochukuliwa na mawakala ilikuwa ya kati ya Sh919,150 hadi Sh40.3 milioni na kusababisha wizara kulipa kiasi cha Sh611.9 milioni ingawa ingeweza kulipa Sh366.6 milioni.
“Serikali ingeweza kuokoa Sh162.3 milioni… Kwa wastani nusu ya tiketi zilizonunuliwa kwa safari za nje ziligharimu Sh2 milioni kila moja zaidi ya kiwango cha chini kilichokuwapo,” inasema taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo, CAG Ludovick Utouh katika taarifa yake alisema Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), haikuwa ikitimiza wajibu wake wa kisheria wa kusimamia viwango vya nauli za usafiri wa anga.
“TCAA hawakutambua majukumu yao ya kusimamia viwango vya nauli za ndege na hivyo kusababisha mawakala kukosa msimamizi na hivyo kutoza nauli kadri wanavyoona inafaa,” alisema.
CAG amependekeza Serikali kuimarisha uwezo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili iweze kufanya uchunguzi na kubaini vitendo vya rushwa katika ununuzi wa umma.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa