Home » » BAJETI:MACHO,MASIKIO DODOMA

BAJETI:MACHO,MASIKIO DODOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
Watanzania watajua hatma ya maisha yao kwa mwaka mmoja ujao, baada ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, leo kusoma bungeni Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/15.
Mabalozi wa nchi mbalimbali duniani wanaowakilisha nchi zao nchini pamoja na wahisani ni miongoni mwa wageni mashuhuri wengi waliopewa mwaliko na Bunge la Jamhuri ya Muungano, kuja kusikiliza hotuba hiyo.

Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema jana kuwa ametoa mwaliko kwa mabalozi,wahisani na wageni wengine wengi.

Pamoja na mabalozi, wahisani, hotuba hiyo itakayosomwa kuanzia saa 10:00 jioni itakuwa ikifuatiliwa na mamilioni ya Watanzania ndani na nje ya nchi wakiwamo wasomi, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na wavuvi, viongozi wa dini na wanasiasa.

Spika Makinda, alitangaza kuwa leo asubuhi, Bunge litakuwa na kipindi cha maswali na majibu kama kawaida.

Alisema baada ya kipindi hicho itasomwa hotuba ya Waziri wa Nchi anayehusika na Mipango. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, ndiye atasoma hotuba hiyo).

Aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Marehemu Dk. William Mgimwa, aliwasilisha makadirio ya Bajeti Kuu ya Serikali ya Sh. trilioni 18.2 kwa mwaka wa fedha 2013/14 sawa na ongezeko la asilimia 17 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2012/13.

Pamoja na kiasi hicho cha fedha, katika mkutano wa bajeti unaoendelea, wabunge waliilaumu serikali kwa kushindwa kupeleka fedha zilizopitishwa na Bunge kwa baadhi ya wizara ikiwa sasa imebakia takriban, wiki mbili tu kabla ya mwaka huo wa fedha kumalizika Juni 30.

Hata hivyo, akimwakilisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda bungeni mwishoni mwa wiki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, asiye na Wizara Maalum, Profesa Mark Mwandosya, alisema fedha nyingi zimeshindwa kupelekwa maeneo husika kwa sababu wahisani walikuwa bado hawajatekeleza ahadi zao.

Serikali ikiwa imebanwa kwa ‘kupiga panga’ Sh. bilioni 100.3 kwa bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo makadirio yake kwa mwaka huu ni Sh. 622, 952, 923,000.00 ikilinganishwa na Sh. bilioni 700 zilizotolewa mwaka jana kwa, wabunge waliitaka Serikali kufuatia ahadi za wahisani.

Walisema kwa kuwa siku hizi dunia ni kijiji kutokana na mawasiliano kuwa rahisi zaidi, ingekuwa jambo la busara kwa serikali kuwasiliana na wahisani ambao bado hawajatekeleza ahadi zao ili waweze kufanya hivyo kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Profesa Mwandosya alikubali kwamba serikali itafanya mawasiliano na wahisani hao ili deni lao lilipwe kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Katika bajeti hiyo (2013/14), marehemu Dk. Mgimwa, alielezea misingi ya bajeti hiyo ya Sh. trilioni 19.6 ni kuendelea kuimarisha na kudumisha amani na usalama, kudumisha viashiria vya uchumi na kuimarisha sera za fedha ili ziendane na sera za bajeti husika. 

Alitaka vipaumbele katika bajeti hiyo kuwa ni kuimarisha miundombinu, kilimo, viwanda, utalii pamoja na huduma za jamii.

Spika Makinda alisema baada ya kusomwa kwa bajeti ya mwaka huu, Bunge litaahirishwa hadi Juni 16, mwaka huu, ili kutoa nafasi kwa wabunge kujadili kwa kina baada ya kupata muda wa kuisoma.

Aliwataka wabunge wanaotaka kujadili bajeti hiyo na bado hawajajiorodhesha kufanya hivyo kutekeleza wajibu wao kwa kujaza fomu maalum.Fomu hizo zilikuwa zikisambazwa bungeni kwa wabunge wanaotaka kujadili hotuba hiyo.

Alisema kwa mujibu wa utaratibu waliojiwekea kila mbunge atakayechangia atatumia muda wa dakika saba ili wabunge wengi wapate nafasi ya kuchangia.

Alisema siku tano za kujadili bajeti hiyo zitatosha na wabunge wengi watapata nafasi.Kwa mwaka wa fedha 2014/15, Serikali imepanga kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Sh. trilioni 19.6.

KAULI YA SERIKALI
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, alitaja mambo manne ambayo bajeti ya 2014/15 itakuwa imejikita zaidi.

Mosi kukusanya mapato zaidi ya ndani  ili taifa liweze kujitegemea, na katika kufanya hivyo usimamizi ni wa kwao, lakini utekelezaji unashirikisha pia taasisi nyingine.

Alisema ukusanyaji wa mapato unatokana na kupungua kwa fedha za misaada kila mwaka na hata zile zinazopatikana masharti yake yanakuwa magumu.

Pili, ni kupeleka fedha maeneo yenye mahitaji muhimu.“Sote tumeona madhara ya kukimbizana na fedha dakika za mwisho wa bajeti, miradi mingi ya maendeleo inashindwa kutekelezwa kwa wakati.

“Kila wizara inayoomba fedha, tutakata mahitaji yasiyokuwa ya lazima…kama wapo wananchi wanakula mlo mmoja tu kwa siku, kwa nini na sisi tupate chai maofisini,” alisema.

Pia alitaja bajeti hiyo italenga kuweka usimamizi wa fedha zinazopatikana kwa kudhibiti maeneo yanayovuja.Alisema hiyo itawezekana baada ya kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Bajeti, mwaka huu.

Tatu, ni kusimamia fedha isiyotokana na kodi, akitoa mfano wa fedha wanazochangishwa wananchi kwa shughuli za maendeleo kama vile ujenzi wa zahanati au madarasa kupotea bure.

Alisema siyo sahihi kwa fedha za wananchi kupotea baada ya ujenzi wa jengo kama zahanati, lakini likifikia hatua ya kupaua mthamini anasema halina viwango.

Nne, bajeti hiyo itajikita pia kuziba mianya ya kukwepa kodi na kusimamia watu wanalipa kodi badala ya kuliachia kundi moja tu la wafanyakazi kulipa kodi kuliko wengine.

Hata hivyo, alisema bajeti hiyo itawapunguzia wafanyakazi mzigo wa kodi.Kuhusu misamaha ya kodi, Nchemba alisema, hatakuwa mwoga kuwachukulia hatua watu watakaokwepa kodi au kutumia vibaya misamaha ya kodi.

Alidai atafanya hivyo bila kujali ukubwa wa kampuni au umaarufu wake.“Hakuna mtu atakayetumia fedha za umma kwa kukwepa kodi au kutumia vibaya misamaha ya kodi,” alisema. Alisema kila msamaha utakaotolewa utatakiwa uwekwe wazi na itumike kama ilivyokusudiwa.

Alisema kwa mfano, misamaha inayotolewa hospitalini inatakiwa itumike hospitalini na siyo vinginevyo.

Aidha alisema wataimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa kodi na kuweka nidhamu ya matumizi mazuri ya fedha za wananchi.Hata hivyo, kama ilivyokuwa 2013/14 kwa bajeti ya serikali kutegemea wahisani kwa shughuli zake za maendeleo, hali haitakuwa tofauti pia kwa mwaka wa fedha 2014/15.

HALI ILIKUWA NGUMU 2013/14

Kwa mwaka wa fedha 2013/14 hali ilikuwa ngumu zaidi kwa baadhi ya wizara hasa za Afya, Maji, Nishati na Madini, Elimu, Uchukuzi kiasi cha kuifanya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuwa na wakati mgumu kwa kuibana serikali juu ya bajeti finyu ya maendeleo na hasa kutotimizwa kwa bajeti yake.

Ili kunusuru hali hiyo, Kamati ya Bajeti ya Bunge ambayo mwenyekiti wake ni Andrew Chenge, ilikutana kwa zaidi ya siku sita na wenyekiti wa kamati mbalimbali za Bunge kupanga namna ya kutunusuru hali tete ya bajeti kwa kuiongezea fedha.

Hata hivyo, maridhiano ya vikao hivyo yalikuwa siyo kuiongezea fedha bajeti bali kupunguza maeneo ambayo hayakuwa muhimu zaidi na kupeleka kwenye maeneo muhimu yaliyotengewa fedha kidogo.

Matokeo ya vikao hivyo, wajumbe baada ya kuibana serikali walifanikiwa kufyeka zaidi ya Sh. bilioni 200 katika Bajeti kuu ikiwamo matumizi yasiyo muhimu.

Moja ya maeneo ambayo yamefyekwa ni fungu la safari za Rais ambapo kwa mwaka 2013/14 alipangiwa bajeti ya Sh. bilioni 15, lakini akatumia Sh. bilioni 50.

Imeelezwa kuwa wajumbe wamepambana na kufanikiwa kupunguza kiasi hicho hadi kufikia Sh. bilioni 11.Kuna uwezekano mkubwa wa kuwapo ugumu katika utekelezaji wa bajeti ya 2014/15 kutokana na kiasi kikubwa cha fedha za bajeti ya maendeleo kutopelekwa katika wizara karibu zote, licha ya Waziri Mkuya kuwaeleza wabunge kabla ya mkutano wa bajeti kwamba mwaka umaomalizika serikali ilikusanya mapato yake kwa asilimia 93 hadi ilipofika Aprili mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa