Home » » CHENGE :SERIKALI IMEKOSA UBUNIFU

CHENGE :SERIKALI IMEKOSA UBUNIFU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Yaelezwa kukataa kupokea ushauri
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge,Andrew Chenge
Serikali imekosa ubunifu ndiyo maana inawasilisha bajeti inayoainisha vyanzo vya mapato vile vile mwaka baada ya mwaka, hali inayoifanya mipango ya serikali kuwa vigumu kutekelezwa.
Hayo yalielezwa bungeni jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya  Bunge, Andrew Chenge, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu bajeti ya serikali ya mwaka 2014/15 ya Sh. trilioni 19.8 53 iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita na Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya.

“Serikali imekosa ubunifu na haitaki kupokea ushauri kuhusiana na vyanzo vipya vya mapato kwa kuwa imekuja na vyanzo vile vile vya kitamaduni vilivyozoeleka wakati kuna vyanzo vingine vingi,” alisema.

Chenge alisema ongezeko la bajeti kwa Sh. trilioni 1.605 ikilinganishwa na iliyomalizika ya mwaka 2013/14 inatia shaka iwapo malengo ya ukusanyaji na matumizi yatafanikiwa.

Alisema uchambuzi wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/15 uliofanywa na Kamati umeonyesha kwamba mzigo wa matumizi ni mkubwa ikilinganishwa na vyanzo vya mapato vilivyopendekezwa.

Alisema mapendekezo ya maabara ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na Kamati ya Chenge 1 pamoja na mapendekeo ya Kamati ya Bajeti inaendelea kuhimiza serikali kufanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa ili kupunguza nakisi ya bajeti na mzigo wa walipa kodi wale wale.

BAJETI YA SERIKALI 2014/15
Chenge alisema katika uchambuzi wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/15 Kamati imebaini kuwa lipo tatizo la kimsingi tokea siku ya kwanza bajeti hiyo inapoanza kutekelezwa.

 Alitaja tatizo hilo kuwa ni mapato yote ya ndani ni Sh. trilioni 12.44, matumizi yote ya kawaida ni Sh. trilioni 13.408, mapato ambayo serikali itakusanya ni asilimia 63.3 tu ya bajeti yake, kwa hiyo nakisi ya bajeti ya matumizi ya kawaida ni Sh. bilioni 968 kiasi cha kuhitaji mikopo na misaada ya kibajeti  ili kulipia sehemu ya matumizi ya kawaida.

Kadhalika alisema bajeti ya maendeleo ni Sh. trilioni 6.445, ikiwa pia na nakisi itayozibwa na mikopo ya ndani, mikopo ya nje na misaada ya miradi ya maendeleo.

Chenge alisema matatizo ya mwaka wa fedha unaokuja ni haya haya yalidhihirika kwa mwaka wa fedha unalizika Juni 30, mwaka huu.

Aliyachambua kuwa ni mzigo mkubwa wa serikali katika vyanzo duni, ambao alisema kuna tatizo la kimsingi tangu siku ya kwanza ilipoanza kutekelezwa kwenye upande wa matumizi.
Alitaja mizigo hiyo kuwa ni matumizi makubwa kama deni la taifa kubwa la Sh. trilioni 4.354, mishahara Sh. trilioni 5.317, matumizi mengineyo Sh. trilioni 3.735 na jumla ya matumizi ya kawaida kuwa Sh. trilioni 13.408.

Tatizo lingine ni misaada na mikopo ya kimaendeleo ni Sh. bilioni 2.019.4, misaada na mikopo ya kibajeti Sh. bilioni 922.2, mikopo ya miradi ya maendeleo ni Sh. bilioni 1.745, mifuko ya pamoja ya kisekta ni Sh. bilioni 274.1 na miradi ya maendeleo imetengewa Sh. trilioni 6.445.

Alisema ukifuatilia kwa makini sura ya bajeti, utaona kwamba makadirio ya makusanyo ya ndani ya Sh. trilioni 12.44 hayatoshi kugharimia mahitaji ya mishahara (Sh. trilioni 5.317), deni la taifa (Sh. trilioni 4.354) na matumizi yasiyoepukika (Sh. trilioni 3.063) ambayo kwa ujumla ni kiasi cha Sh. trilioni 12.734.

Kamati hiyo ilipendekeza kodi ya zuio la asilimia 15 kwenye ada wanayolipwa wakurugenzi wa bodi kila mwisho wa mwaka iangaliwe upya kwa kuwa Kodi ya zuio (WHT) kwa washauri binafsi ni asilimia tano kwa kila mwisho wa mwaka.

Chenge alisema pamoja na serikali kupunguza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 13 hadi asilimia 12, Kamati haijaridhika na punguzo hilo na imeishauri kupunguzwa hadi kufikia tarakimu moja kwa mwaka ujao wa fedha.

Mapendekezo mengine yaliyotolewa na Kamati hiyo ni kubadilisha ukomo wa umri wa magari yasiyo ya uzalishaji yanayotozwa ushuru wa uchakavu wa asilimia 25 hivi sasa kutoka miaka kumi na zaidi kwenda miaka minane.

“Kamati inashauri Serikali kuwa na sera mahususi ya kodi itakayohamasisha wananchi kununua magari mapya badala ya chakuavu kwa kupunguza ushuru wa bidhaa kwa magari mapya,” alisema.

Kuhusu kurekebisha viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa zisizokuwa za mafuta kwa asilimia 10; vinywaji baridi, mvinyo, pombe, na vinywaji vikali, alisema Kamati inashauri kuwa pendekezo la ongezeko la bidhaa hizo liondolewe.

DENI LA TAIFA
Alisema katika mwaka wa fedha 2012/13 jumla ya Sh. trilioni 2.735 zilitengwa kwa ajili ya kugharimia deni la taifa, hata hivyo, Sh. trilioni 3.341 zilitumika katika mwaka huo kugharimia deni hilo ambalo halikuwa kwenye bajeti.

Alisema ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), imebaini kuwa uhakiki wa mseto wa deni la taifa umebaini akaunti saba za wafadhili wanaodai serikali zenye thamani ya Sh. trilioni 1.247 ambazo hazikufanyiwa malipo yoyote tokea mwaka 1998.

“Maelezo yaliyotolewa kuhusu akaunti hizo ni kwamba, malipo yake yamesimama kwa sababu mazungumzo kati ya serikali na wafadhili yanaendelea kwa nia ya kulipatia serikali nafuu ya madeni na hata pengine kuyafuta kabisa,” alisema.

Alisema deni la taifa hadi kufikia Machi 2014 ilikuwa imefikia Sh. trilioni 30.563 ikilinganishwa na Sh. trilioni 23.67 Machi 2013.

MWENENDO WA MATUMIZI
Alisema bado manunuzi mengi yamekuwa yakifanyika bila tija na kutoa mfano wa manunuzi ya dharura yaliyofanywa na Mamlaka ya Bandari Tanzania ambayo hayakupata kibali cha Mlipaji Mkuu wa Serikali, yaliyokuwa na gharama ya Dola za Marekani 810,000.

Alisema tatizo la kutosimamia kwa umakini matumizi ya serikali ulisababisha bajetiya mwaka 2013/14 kuanza na deni la Sh. bilioni 611.4 ambayo ni matumizi ya mwaka wa fedha 2012/13, lakini hayakulipwa mwaka huo na deni hilo halikuingizwa kwenye bajeti ya 2013/14.

“Hali hii inatarajiwa pia kujitokeza tena kwa kiwango kikubwa ziadi kwenye bajeti ijayo ya mwaka 2014/15. Malimbikizo ya madai hayo hadi Desemba 2013 yalikuwa yamefikia Sh trilioi 2.09, tatizo hili ni lazima litafutiwe dawa haraka,” alisema.

Chenge alisema katika mwaka wa fedha 2013/14 utekelezaji wa bajeti katika baadhi ya mafungu ulifanyika kinyume cha matarajio ya serikali, hali iliyosababisha baadhi ya mafungu ambayo yalikuwa yametengewa fedha kutopelekewa kwa waliopangiwa.

Mafungu ambayo yalipokea fedha nje ya bajeti za mafungu hayo aliyataja kuwa ni Wizara ya Mambo ya Ndani (Polisi), Ofisi ya Makamu wa Rasi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mfuko wa Bunge, Tamisemi, Wizara ya Mawasiliano, Utamaduni na Michezo na Wizara ya Ujenzi.

 Alisema mafungu hayo yalitumia ziada ya Sh. bilioni 115.81  na kiasi hicho kilitumika ndani ya miezi tisa ya utekelezaji wa bajeti.

UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2013/14
Alisema mwenendo unaonyesha kuwa hadi kufikia Aprili  2014, serikali imekusanya Sh. bilioni 12,882 na kwamba kiwango hicho cha ukusanyaji wa mapato siyo cha kuridhisha na Kamati inaona kwamba sera za mapato kwa mwaka 2013/14 zimeshindwa kuleta mapato kama ilivyokusudiwa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa