Home » » NI BAJETI YA MACHUNGU

NI BAJETI YA MACHUNGU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WAZIRI wa Fedha, Bi. Saada Mkuya Salum, jana aliwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali bungeni Mjini Dodoma, kwa mwaka wa fedha 2014/15 ambayo ni zaidi ya sh. trilioni 19.8 ikiongeza makali ya kodi kwenye bia na sigara.

Katika bajeti hiyo, watumiaji pombe kali na juisi za matunda ambayo yanazalishwa nchini, wameguswa na makali hayo pamoja na kudaili ukomo wa umri wa magari yanayopaswa kuingizwa nchini kutoka miaka 10, hivi sasa yataanzia miaka minane kushuka chini.

Bi. Salum alisema lengo la Serikali ni kulinda mazingira, kupunguza wimbi la uagizaji magari chakavu ambayo yanasababisha ajali, vifo na kuongeza gharama kwa kutumia fedha za kigeni kuagiza vipuri mara kwa mara.

Alisema Serikali imebadilisha ukomo wa umri wa magari ya uzalishaji na yasiyobeba abiria yanayotozwa ushuru wa uchakavu asilimia tano kutoka miaka 10 na zaidi hadi minane kushuka chini.

Upande wa matrekta, alisema hayatatozwa kodi na wale wanaoingiza mabasi ya kubeba abiria, watatozwa kodi ya asilimia 10 tofauti na awali ambapo walitozwa asilimia 25. Lengo la hatua hiyo ni kurahisisha usafiri wa abiria na kuwawezesha wananchi kupata unafuu.

Hatua zingine zilizochukuliwa na Serikali ni kurekebisha viwango maalum vya ushuru wa bidhaa zisizokuwa za mafuta kwa asilimia 10 ambazo ni vinywaji baridi, mvinyo, pombe na vinywaji vikali.

Alisema bidhaa za sigara zitatozwa ushuru wa bidhaa asilimia 25 ili kutekeleza matakwa ya Mkataba wa Udhibiti wa Matumizi ya Tumbaku wa Shirika la Afya Duniani ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mkataba huo.

Ushuru wa vinywaji baridi, Bi. Salum alisema umeongezeka kutoka sh. 91 kwa lita hadi sh. 100 kwa lita ikiwa ni ongezeko la sh. 9 kwa lita ambapo ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) ambayo imetengenezwa kwa matunda yanayozalishwa nchini, umepanda kutoka sh. 9 kwa lita hadi sh. 10 kwa lita.

Upande wa bia, ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka za Tanzania ambayo haijaoteshwa kama vile Kibuku, umepanda kutoka sh. 341 kwa lita hadi sh. 375.

Ushuru wa bia nyingine zote umeongezeka kutoka sh. 578 kwa lita hadi sh. 635 kwa lita ambapo ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, umeongezeka kutoka sh. 160 kwa lita hadi sh. 176.

Alisema ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, umeongezeka kutoka sh. 1,775 kwa lita hadi sh. 1,953 kwa lita ikiwa ni ongezeko la sh. 178 kwa lita na ushuru wa vinywaji vikali, umepanda kutoka sh. 2,631 kwa lita hadi sh. 2,894 kwa lita.

Ushuru wa Mafuta

Akizungumzia Sheria ya Ushuru wa Mafuta, Sura 220, Bi. Salum alisema anapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria hiyo, ili kuondoa mamlaka ya Waziri wa Fedha kutoa msamaha wa Ushuru wa Mafuta, isipokuwa misamaha inayotolewa kwenye mikataba iliyosainiwa baina ya Serikali na washirika wa maendeleo ili kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile miundombinu ya barabara, maji na mingine.

Mikopo

Kuhusu mikopo ya kibiashara ndani na nje, alisema kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu nchini, Serikali itaendelea kukopa mikopo yenye masharti ya kibiashara kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo.

Alisema mwaka 2014/15, Serikali inategemea kukopa katika soko la ndani sh. bilioni 2,955.2 kati ya hizo, sh. bilioni 689.56 sawa na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na sh. bilioni 2,265.7 kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva kwa utaratibu.

Bi. Salum alisema Serikali inatarajia kukopa sh. bilioni 1,320.0 kutoka masoko ya fedha ya nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Alisema uamuzi wa kuendelea kukopa kwa masharti nafuu na ya kibiashara umezingatia tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa pamoja na umuhimu wa kuendeleza miradi ya kipaumbele hususan miundombinu ambayo itafungua fursa za kiuchumi na kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi.

Misamaha ya Kodi

Bi. Salum alisema kila baada ya robo mwaka, kila misamaha ya kodi itakuwa inawekwa hadharani kwa kuhusisha kila taasisi, Wizara, kampuni na kuonesha jinsi taasisi zilizopata misamaha jinsi zilivyofaidika.

Alisema lengo la hatua hiyo ni kuongeza wigo wa uwazi kwa jamii kuelewa kinachoendelea pamoja na kujua waliopewa misamaha.

Walimu

Alisema Serikali inaendelea na utaratibu wa ujenzi wa nyumba za walimu kwa awamu. Mwaka 2013/14, halmashauri 40 kila moja ilipewa sh. milioni 500 ili zianze ujenzi wa nyumba za walimu na kiasi kama hicho kitatolewa kwa halmashauri hizo kwa mwaka 2014/15.

Aliongeza kuwa, sh. milioni 500 zitatolewa kwa halmashauri 80 zaidi, hivyo kufanya jumla ya halmashauri 120 kunufaika na utaratibu huo.

Kuhusu malipo ya madai ya walimu, alisema Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa madai ya walimu yaliyohakikiwa, ambapo mwaka 2013/14, kiasi cha sh. bilioni 5.6 kimelipwa na mwaka 2014/15, madai ya walimu ambayo yatakuwa yamehakikiwa yataendelea kulipwa.

Wanafunzi

Bi. Salum alisema mwaka 2014/15, Serikali itaendelea kuboresha huduma kwa wanafunzi katika shule na vyuo mbalimbali ili kuhakikisha vijana wanasoma katika mazingira tulivu na bora.

Hatua hiyo itaenda sambamba na kujenga maabara katika shule, vyuo na kuzipatia vifaa muhimu, pamoja na kutumia maabara zinazotembea ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi, kutenga fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi walio vyuoni na watakaojiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Alisema pia Serikali itajenga maktaba mpya, kukarabati na kuimarisha zilizopo kwa kuzipatia vitabu zaidi vya kiada na ziada.

Nafuu kwa watumishi

Katika hotuba hiyo, alisema mwaka 2014/15 Serikali imepunguza kodi kwa watumishi kutoka asilimia 15 hadi 13 ambapo mkakati huo ni endelevu hadi kuhakikisha msamaha huo unafikia tarakimu moja ili kuwapunguzia mzigo wafanyakazi.

Bajeti ya Kisekta

Bajeti ya Nishati na Madini, imetengewa sh. bilioni 1,090.6, miundombinu ya usafirishaji sh. bilioni 2,109.0, kilimo sh. bilioni 1,084.7, elimu sh. bilioni 3,465.1, maji sh. bilioni 665.1, afya sh. bilioni 1,588.2, utawala bora sh. bilioni 579.4.

Alisema mwaka 2014/15 kwa kuzingatia sera za uchumi, misingi na shabaha ya bajeti, sura ya bajeti itakuwa kama ifuatavyo; Serikali imepanga kukusanya jumla ya sh. bilioni 19,853.3 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje.

Mapato ya kodi na mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia sh. bilioni 12,178.0 sawa na asilimia 19.2 ya Pato la Taifa. Mapato kutokana na vyanzo vya halmashauri yanatarajiwa kufikia sh. bilioni 458.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.

Maoni ya Bajeti

Wakati huo huo, Serikali imeombwa kuangalia maeneo muhimu hususan sekta ya madini na riba katika benki ili kusaidia wananchi wa kawaida badala ya kukimbilia kupandisha kodi katika maeneo ambayo wananchi wengi hupata mahitaji yao.

Waziri Mkuu mstaafu, Bw. John Samwel Malecela, aliyasema hayo jana wakati akitoa maoni yake baada yake bajeti hiyo kusomwa bungeni na kuongeza kuwa, bajeti ni nzuri kwani imekuwa tofauti na miaka iliyopita ikiwa imeondoa baadhi ya kero zinazokuwa zikilalamikiwa na wananchi.

"Bajeti ya mwaka huu ni tofauti na ya miaka ya nyuma, kama mlivyosikia baadhi ya kodi zimeondolewa hivyo italeta unafuu kwa mwananchi wa kawaida, " alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema bado matatizo ya msingi ambayo yapo pale pale kwa kuwa Serikali haikuweza kubainisha sekta ya madini imeingiza kiasi gani na itaingiza kiasi gani ambapo fedha za ndani haziwezi kukidhi mahitaji ya kawaida.

Alisema kasi ya ongezeko la deni la Taifa linamtisha pamoja na ukopaji umeongezeka kwa kasi tangu mwaka 2007 hadi sasa.

"Kwanza nampongeza kwa jambo zuri moja ambalo ni kutoa taarifa za misamaha ya kodi ili watu kufahamu...awali kulikuwa na utaratibu huo lakini sasa umerudishwa hivyo ni jambo zuri pamoja na Waziri kujitoa katika kuidhinisha misamaha ya kodi.

Aliongeza kuwa, Bi. Salum ameshindwa kueleza sekta ya madini imechangia kwa kiasi gani lakini deni ya Taifa limekuwa kubwa tangu 2007 na haioneshi jinsi litakavyoweza kupungua.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, alisema bajeti hiyo ni ya maumivu kwa wananchi kwani imeongeza kodi katika maeneo muhimu kama vinywaji baridi ambavyo wananchi wengi hutumia.

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani, alisema bajeti hiyo ni nzuri lakini haiwasaidii wananchi wa hali ya chini kutokana na riba kubwa kwenye benki ambazo huchukua mikopo.

"Kama bajeti ingekuwa kweli ina nia ya kuwasaidia wananchi, riba ingekuwa ndogo katika benki zote ambazo wakulima huenda kukopa, katika jimbo langu baadhi ya wananchi wamekimbia nyumba zao kwa kuogopa kudaiwa na benki baada ya kukopa wakiamini wangepata mazao lakini haikuwa hivyo matokeo yake benki zinachukua nyumba zao," alisema.

Mwananchi wa kawaida, Bi. Justina Saimon, mkazi wa Dar es Salaam,alisema bajeti hiyo ni nzuri kwani imebana misamaha ya kodi lakini bado haijamsaidia mwananchi wa hali ya chini.

Alisema Serikali imeacha sekta ya madini ambayo ndiyo inayoingiza fedha nyingi za kigeni lakini kodi kubwa imepandishwa kwa mahitaji muhimu ya wananchi wa kawaida.

"Bajeti ya Serikali tumeizoea kwani kila mara inaacha kupandisha kodi kwenye sekta muhimu inakimbilia maeneo ambayo wananchi wengi wanayatumia hivyo ni sawa na kuendelea kuwaumiza," alisema.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa