Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Serikali imetangaza utaratibu mpya kwa usajili wa namba za
pikipiki kutoka ‘T’ na sasa zitasomeka ‘TZ’ lengo likiwa ni kudhibiti
vitendo vya uhalifu.
Hatua hiyo ilitangazwa bungeni mjini Dodoma jana
na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali
kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Uagizaji magari waongezwa makali
Waziri Mkuya alisema, Serikali inatarajia kuongeza
kodi kwa magari yatakayoingizwa nchini yakiwa yametumika kwa zaidi ya
miaka minane baada ya kubadilisha ukomo wa umri wa magari yasiyo ya
uzalishaji (non-utility vehicles) na magari ya uzalishaji na yasiyobeba
abiria (non-passanger utility vehicles), kutoka miaka 10 hadi minane.
Alisema hatua hiyo ina lengo la kulinda mazingira
na kupunguza wimbi la uigizaji wa magari chakavu ambayo yanasababisha
ajali, vifo na kuongeza gharama kwa kutumia fedha za kigeni kuagiza
vipuri mara kwa mara.
Pendekezo hilo pia liliwasilishwa katika Bajeti
inayomalizika lakini liliondolewa baada ya kuibua mvutano mkubwa bungeni
na kusababisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuingilia kati.
Waziri wa Fedha wakati huo, marehemu William
Mgimwa alisema Serikali iliwasilisha pendekezo hilo ili kupunguza muda
wa magari yaliyotumika kuingia nchini kwa lengo la kudhibiti magari
chakavu, kutunza mazingira na kuwapunguzia wananchi mzigo wa kununua
mafuta kwa kuwa yanatumia nishati hiyo kwa wingi.
Alisema Serikali inatekeleza hoja hiyo kwa kuwa hata Kenya na Uganda wameanza kufanya hivyo na kwamba ni mpango wa nchi nyingi.
Baada ya kuwasilisha muswada huo, Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Fedha na Uchumi, iliwasilisha maoni yake na kupinga
pendekezo hilo la Serikali kwa kueleza kwamba uwezo wa wananchi wengi
kununua magari mapya ni mdogo.
Akiwasilisha maoni ya Kamati, aliyekuwa mwenyekiti
wake, Andrew Chenge alisema Serikali haikuwa na nia ya kuyaondoa
barabarani magari yenye umri zaidi ya miaka 10, hivyo pendekezo hilo
halikuwa na manufaa kwa taifa.
“Kamati inaamini kwamba sababu zilizofanya
Serikali kuleta mapendekezo bungeni mwaka 2006 ya kutoza ushuru wa
bidhaa za magari yenye umri zaidi ya miaka 10 bado zina nguvu hadi leo…
Kamati inashauri umri wa magari yanayostahili msamaha uwe miaka 10 na
siyo minane inayopendekezwa,” alisema.
Msimamo huo wa Kamati uliungwa mkono na Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambayo ilisema hoja ya Serikali katika eneo
hilo ni dhaifu kwa kuwa wananchi wengi hata wabunge hawana uwezo wa
kununua magari mapya na wala umri wa gari si kigezo pekee cha ubora.
Mvutano huo ulimlazimu Waziri Mkuu Pinda kuingilia kati na kueleza kwamba Serikali imekubaliana na maoni ya wabunge na kukubali umri wa magari yanayoingia nchini kubaki kuwa miaka 10.
Chanzo:Mwananchi
Mvutano huo ulimlazimu Waziri Mkuu Pinda kuingilia kati na kueleza kwamba Serikali imekubaliana na maoni ya wabunge na kukubali umri wa magari yanayoingia nchini kubaki kuwa miaka 10.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment