Home » » PINDA:TUNAJIPANGA KUPAMBANA NA MATUKIO YA TINDIKALI

PINDA:TUNAJIPANGA KUPAMBANA NA MATUKIO YA TINDIKALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Licha ya matukio ya umwagiaji tindikali kuendelea na wahusika kushindwa kukamatwa, serikali imesema imejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vya nje kubaini wahusika wa vitendo hivyo, vyanzo na sababu zake ili kuwachukulia hatua stahiki.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (pichani), wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge, bungeni jana.

Alikuwa akijibu swali la Betty Machangu (Viti Maalum-CCM), aliyetaka kujua serikali imechukua hatua gani kuhusu matukio ya mauaji na umwagiaji wa tindikali kwa mapadri, masheikh, watalii na walimu wa kujitolea yaliyotokea Zanzibar.

Pinda alisema serikali imekuwa ikishirikiana na vyombo vya nje kukabiliana na vitendo hivyo na kutokana na hali hiyo baadhi ya vitendo vimeweza kudhibitiwa kabla havijatokea na kuzima njama hizo.

“Hali ni shwari na serikali imechukua hatua stahiki na imekuwa macho kukabiliana na vitendo hivyo,” alisema Pinda.

Pinda alisema mara nyingi linapotokea suala kama hilo, serikali huchukua hatua za haraka kwa vyombo vya dola kuingilia kati.
Alisema kwa sasa hali ni shwari baada ya vitendo hivyo kudhibitiwa.

Hata hivyo, aliwataka Watanzania kujiepusha na kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuwaingiza katika mgongano na vyombo vya dola.

Hadi sasa, tayari kuna orodha ya matukio kadhaa ya kuogofya kuhusiana na umwagiaji tindikali; ambayo sifa yake kubwa ni kumuunguza vibaya mtu anayemwagiwa, kumuachia maumivu makali yatokanayo na majeraha makubwa, kumbadili mtu haiba yake daima milele kwa namna ya kusikitisha na pia kuwapofusha wale wanaoingiwa machoni na kimiminika hicho cha aina tofauti.

Miongoni mwa waliokwishatajwa na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi kukumbwa na vitendo hivyo, ni mwananchi aitwaye Masoud Mohamed Shambi, ambaye ni mkazi wa kisiwa cha Pemba, aliyekumbwa na mkasa huo mwaka 2000.

Mwingine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Rashid Ali Juma (45), ambaye aliunganishwa katika orodha ya waathirika wa tindikali baada ya kumwagiwa na mtu asiyejulikana na kuhudhuriwa kwa takriban asilimia 25 ya mwili wake.

Juma alikumbwa na mkasa huo Februari 18, 2011, saa 2:30 usiku, nje ya Msikiti wa Amaan, ambako alikuwa amekaa baada ya kumaliza ibada ya swala ya isha.

Pia Novemba 5, 2012, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, alikumbwa pia na mkasa huo, baada ya kumwagiwa tindikali na mtu asiyefahamika wakati akifanya mazoezi ya viungo kwenye Uwanja wa Mwanakwerekwe.

Tukio jingine la tindikali Zanzibar lilitokea mwaka 2012 na kumhusisha mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia, Chandurali Chunilai Asawala.
Alimwagiwa na watu waliomvamia akiwa njiani, akaporwa Sh. 700,000 na kuachwa akiwa na majeraha tele mwilini.

Mei 23, 2013, saa 2.00 usiku, Sheha wa Shehia ya Tomondo, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Said Omar, maarufu kwa jina la Kidevu, alikumbwa pia na mkasa huo wa kutisha wa kumwagiwa tindikali.

Agosti 7, 2013, saa 1:15 usiku, watu wawili waliokuwa katika pikipiki kwenye eneo la Mji Mkongwe, Mtaa wa Shangani, Zanzibar, waliwamwagia tindikali mabinti wawili, raia wa Uingereza Katie Gee (18) na Kirstie Trup (18) waliokuwa Zanzibar wakifanya kazi ya ualimu kwa kujitolea.
 
Vilevile, Septemba 14, 2013, unyama utokanao na mashambulizi ya tindikali visiwani Zanzibar ulimkuta Padri Ancelmo Mwang’amba wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Cheju.

Tukio hilo lilijiri Pemba, eneo la Mtemani Maghorofani, saa 2:00 usiku. Mtu asiyejulikana alimmwagia tindikali Msuko na kumuunguza vibaya kifuani na maeneo ya tumboni.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa