Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI imepokea gawio la sh bilioni 1. 275 kutoka Kampuni ya
Mafuta ya Tanzania Petroleum Reserves Limited (Tiper), baada ya kampuni
hiyo kupata faida baada ya kodi ya sh bilioni 6.06 kwa mwaka wa fedha
2013.
Akizungumza muda mfupi baada ya kupokea hundi kwa niaba ya Serikali
katika Ofisi ya Hazina jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha, Dk Servarcius Likwelile, alisema fedha hizo
zitasaidia kujazia kwenye mapungufu yaliyojitokeza katika bajeti ya
mwaka 2013/2014.
"Gawio hili kutoka Tiper litaisaidia Serikali kuziba mapengo
yaliyobaki katika bajeti kutokana na ukweli kwamba hatukuweza kufikia
malengo yetu katika ukusanyaji wa mapato. Tutazielekeza fedha hizi
katika sekta zinazozihitaji zaidi. Usambazaji wake utategemea na
mgawanyo wa bajeti ya mwaka 2013/2014 jinsi ilivyo,” alisema.
Aliupongeza uongozi wa kampuni ya Tiper kwa utendaji bora ambao
umeifanya kampuni huyo kuendelea kupata faida nzuri, kutengeneza ajira,
kuhakikisha nchi ina kiasi cha kutosha cha akiba ya mafuta ya petroli
na kuhakikisha kwamba wanahisa wote wawili wanapata magawio yao jinsi
inavyotakiwa.
Akizungumuza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi hiyo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Tiper, Daniel Belair, alisema mchango wa kampuni yake
utasaidia katika kuchochea jitihada mbalimbali za maendeleo ya kijamii
na kiuchumi nchini.
"Mwaka 2013 ulikuwa ni mwaka bora kwa kampuni ya Tiper hususani
katika utendaji wake ambapo kampuni iliweza kupata faida ya sh bilioni
8.8 kabla ya kodi na kuweza kulipa kodi ya mapato ya sh bilioni 2.74
kwa serikali.
"Tiper imejidhatiti katika kuwekeza nyenzo za kisasa za kuhifadhia
mafuta na itahakikisha kwamba mafuta ya petroli yanapatikana kwa
urahisi kwa watumiaji wote wadogo na kubwa," alisema Beilar.
Alisema kampuni hiyo imewekeza zaidi ya dola milioni 10 za Marekani
kwa ajili ya kuongeza uwezo wake wa sasa wa kuhifadhi mafuta ya mita za
ujazo 141,000 hadi kufikia mita za ujazo 290,000 ifikapo mwaka 2015.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tiper, Profesa Abdulkarim
Mruma, alisema kampuni hiyo inayomilikiwa kwa pamoja na Serikali ya
Tanzania na kampuni ya Oryx Oil & Gas (OOG), kila mmoja akiwa na
hisa za asilimia 50 imekuwa ikilipa gawio kwa serikali tangu 2009
kutokana na uwekezaji mkubwa wa sh bilioni 8.3.
chanzo :Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment