Home » » UZALENDO HAUPIMWI KWA MATAMASHA YA MUZIKI

UZALENDO HAUPIMWI KWA MATAMASHA YA MUZIKI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Hivi karibuni limefanyika tamasha la uzalendo mjini Dodoma lililoshirikisha wasanii wa muziki, hasa wa kizazi kipya na waigiza filamu.
Mgeni rasmi wa tamasha hilo alikuwa ni Rais Jakaya Kikwete, akiwa pia na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri na viongozi wengine wa Serikali.
Rais Kikwete aliyezindua video ya wasanii mbalimbali alisema amependezwa na wimbo wa uzalendo huku akiwataka Watanzania kutimiza wajibu wao wa kuilinda nchi yao kwani inafitiniwa na kuchukiwa na wengi.
Inawezekana ni kutokana na mwaliko huo, ndipo Rais Kikwete akalazimika kutoa maoni kama hayo. Lakini ijulikane kuwa suala la uzalendo linakwenda mbali zaidi ya matamasha kama hayo. Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda nchi yake. Neno hili lilitumika sana miaka ya 1950 na kuendelea wakati nchi za Afrika na kwingineko duniani zikipigania uhuru kutoka kwa wakoloni hasa miaka ya ‘60.
Watu waliungana kwa moyo wote kwa sababu walijua adui yao ni mkoloni. Lakini baada ya uhuru kupatikana, tunaona neno lenyewe likaanza kupoteza uhalisia wake, kwa sababu wale viongozi walioingia madarakani wakajivisha tena madaraka ya ukoloni.
Leo, miaka 52 baada ya uhuru, ukiuliza Watanzania wanaungana ili kupambana na adui gani, haieleweki. Hakuna anayejali tena nchi, kila mtu anajitafutia mtaji wake aondoke.
Kwa hali ilivyo sasa ni nadra kuona Mtanzania mzalendo. Maadili yameshuka tangu uongozi wa juu wa Serikali hadi ngazi za chini. Kila kukicha utasikia kashfa ya wizi wa fedha za Serikali na wezi hawachukuliwi hatua. Leo utasikia kashfa ya EPA, mara wezi wamesamehewa, kesho utasikia kashfa ya IPTL, kila mtu anaruka kimanga na nyinginezo nyingi.
Rais Kikwete ameshakiri mara kadhaa kuwa na orodha ya wala rushwa, majangili 40 wa meno ya tembo, lakini hatuoni wakikamatwa wala kuwajibishwa.
Halafu akitoka hapo, anawataka Watanzania waipende nchi yao! Tutaipendaje nchi wakati wachache wanafaidi matunda ya uhuru na wengi wanalala njaa?
Matokeo yake sasa karibu kila Mtanzania anatafuta upenyo naye aibe siku ziende. Kama ni mfanya usafi ofisini, anaiba sabuni walau akauze mtaani, dereva naye anaiba mafuta akauze, ofisa anabuni miradi na safari hewa ili apate cha juu, waziri anaingia mikataba bandia na wawekezaji ili apate asilimia 10. Mwisho wa yote Rais amekaa kimya!
Rushwa imekithiri, siyo hospitali, shuleni, mahakamani na popote zinapotolewa huduma. Uzalendo haupo tena, kila mtu anachukua chake mapema.
Tatizo hili halitatibika kwa kufanya matamasha ya muziki na kuleta wasanii wa muziki wa Marekani kuja kutumbuiza.
Ni lazima tujenge jamii inayowajika na viongozi wa Serikali wawe wa kwanza katika kuwajibika na wawe mfano, siyo vinginevyo.
 Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa