Home » » WATANZANIA WAHIMIZWA KUPIMA AFYA

WATANZANIA WAHIMIZWA KUPIMA AFYA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen Kebwe amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao ili kuzuia kasi ya ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell).
Alisema ugonjwa huo unapaswa kupigwa vita kwa nguvu kwani asilimia 13 hadi 18 ya Watanzania, wanaugua ugonjwa huo ulioenea kwenye mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa na Pwani.
Dk Kebwe ameiagiza wizara yake kutenga fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ugonjwa huo na kusema kuwa bila jitihada za makusudi, taifa litazidi kupoteza nguvukazi kutokana na ugonjwa huo.
Aliyasema hayo jana wakati akizundua kampeni ya kuhamasisha mapambano dhidi ugonjwa huo iliyofanyika kwenye Viwanja vya Nyerere Squire mjini Dodoma.
“Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ni nchi ya tano duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa ugonjwa huu wa ‘Sickle Cell’”, alisema Dk Kebwe
Alisema kuwa kutokana na ugonjwa huo kuwa tishio amezitaka pia hospitali zote nchini kufungua kliniki maalumu kwa ajili ya kupima ugonjwa huo, kwani hivi sasa ni Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee ndiyo inayotoa matibabu ya ugonjwa huo.
“Kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya ugonjwa huu, baadhi yao wamekuwa wakihusisha matukio ya vifo hivyo na imani ya kishirikina,” alisema Kebwe na kuongeza: “Mtu akifa watu wanasema kalogwa, mara kuna mkono wa mtu, kumbe kifo hicho kimetokana na ugonjwa wa ‘Sickle Cell’. Tuachane na imani hizo potofu twende hospitali tukapime ili tuweze kuzuia maambukizi.”
Aliongeza: “Ugonjwa huu ni wa kurithi, kama baba na mama wana vinasaba hivyo, mtoto akizaliwa naye atakuwa na ugonjwa huu. Nchi za wenzetu wamefanikiwa kupambana nao kwa njia ya kupima, kwani ukipima unajitambua.”
Mkurugenzi wa Asasi ya Motion Art Production (MAP), Honeymoon Aljabry alisema ugonjwa huo umesambaa kwa kasi nchini na kuiomba Serikali kufanya jitihada za dhati kuokoa maisha ya watu.
Asasi ya MAP kwa kushirikiana na Taasisi ya Fight Sickle Cell out of Afrika ya nchini Marekani ndiyo walioandaa kampeni hiyo inayosaidia vifaa vya tiba kwa wagonjwa.
 Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa