Home » » AJALI YA BASI YAUA 17,YAJERUHI 56

AJALI YA BASI YAUA 17,YAJERUHI 56

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Wananchi wakiangalia basi la Morobest lilipopata ajali ya kugongana uso kwa uso na lori jana na kuua watu 17 katika eneo la Pandambili, wilayani Kongwa, mkoa wa Dodoma. PICHA: IBRAHIM JOSEPH
Watu 17 wamefariki dunia na wengine 56 wamejeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Moro Best kugongana uso kwa uso na lori la mizigo, katika eneo la Pandambili, wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.
Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio jana zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, David Misime, zilieleza kuwa, kati ya waliokufa, 13 walifariki dunia papo hapo.

Kamanda Misime alisema wengine wawili walifariki wakiwa njiani wakati wakikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na wawili walifia kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Alitaja chanzo cha ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 2.30 asubuhi kuwa ni dereva wa lori  lenye namba za usajili T820 CKU na tela namba T 390 CKT, kujaribu kulipita lori lingine, ambalo halijafahamika na kugongana na basi hilo.

Basi hilo lilitajwa na Kamanda Misime kuwa ni lenye namba za usajili T 258 AHU, lililokuwa likitokea Mpwawa kuelekea jijini Dar es Salaam, huku lori hilo likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma.

“Wakati dereva wa lori akijaribu kulipita lori lingine, akakutana ana kwa ana na basi, hali iliyosababisha ajali, ambayo imegharimu maisha ya wenzetu,” alisema Kamanda Misime.

MMILIKI WA LORI AZUNGUMZA
Akizungumza kwenye eneo la tukio, mmiliki wa lori hilo aliyejitambulisha kwa jina la Felix Maneno, alimtaja dereva wa lori  kuwa ni Gilbert Lemanya na utingo wa gari hilo, Mikidadi Zuberi Omar, ambao alisema wote walikufa papo hapo.

Maneno alisema lori hilo lilikuwa likisafirisha mabomba makubwa ya maji, ambayo ni mali ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka mkoani Dodoma (Duwasa).

HOSPITALI YA RUFAA MKOA DODOMA
Gari ya kubeba wagonjwa la kwanza ilifika hospitali majira ya saa 4:00 asubuhi, likiwa na majeruhi 18, mmoja kati yao akiwa ni mtoto, Darina Dickson (2).

Gari lingine la wagonjwa lilifika hospitali hapo majira ya saa 5:00 asubuhi, likiwa na majeruhi wawili; mmoja wa kike na mwingine wa kiume.Hata hivyo, taarifa iliyotolewa muda mfupi baadaye na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Ezekiel Mpuya, ilieleza kuwa mtoto huyo alifariki dunia muda mfupi baada ya kupokelewa wodini.

“Mwingine aliyefariki baada ya kufikishwa hapa ni Magreth Njanji, mkazi wa Mwananyamala, Dar es Salaam,” alisema Dk. Mpuya.

Dk. Mpuya alisema hali ya Mfamasia wa Hospitali ya Mpwapwa, Getrude Kombe ni mbaya na kwamba ni mmoja kati ya wagonjwa wawili ambao wapo kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Alisema Kombe amejeruhiwa pamoja na mumewe wakiwa safarini kikazi.Mumewe ambaye ni daktari katika Hospitali ya Wilaya Mpwapwa, George Mjelwa, amelazwa katika wodi namba 11 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Dk. Mpuya alisema waliagiza uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa kuhamishia mkoani wagonjwa ambao hali zao zilikuwa mbaya ili kunusuru maisha yao.

Pia alisema aliagiza Bohari ya Dawa (MSD) mkoani Dodoma kupeleka dawa za dharura mapema iwezekanavyo ili kukidhi mahitaji yaliyotokana na tukio hilo.

MAJERUHI ANENA
Tofauti na taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kuhusu chanzo cha ajali hiyo, mmoja wa majeruhi, Nicholus Loga, alilieleza NIPASHE kuwa, dereva wa basi ndiye aliyejaribu kushindana na basi la Al-Saedy kabla ya ajali hiyo kutokea.

“Jamaa alitaka ku-over take (kumpita) Al- Saedy. Mimi nilikuwa nimekaa ‘siti’ ya pili kabla ya ‘siti’ ya mwisho kabisa upande wa kushoto. Ndipo akajikuta uso kwa uso na lori lililokuwa na mabomba, wakagongana,” alisema Loga.

Loga alikuwa majeruhi pekee aliyefikishwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoani Dodoma, akiwa na uwezo wa kuzungumza tofauti na wenzake na alitibiwa na kuruhusiwa jana muda mfupi baada ya kuchunguzwa afya yake.

“Nilikuwa na ndugu yangu amevunjika mguu na mgongo anasema unauma. Yumo wodini. Tulikuwa tunatoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam,” alisema.

PANDAMBILI NA AJALI KUBWA
Ajali zilizowahi kutokea eneo hilo ni pamoja na iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime (Chadema), Chacha Wangwe, wakati akitokea mjini Dodoma mwaka 2008.

Hivi karibuni muasisi wa Chama cha ACT-Tanzania, Samson Mwigamba akiwa na Ludovick Joseph walipata ajali katika eneo hilo wakisafiri kwenda Dodoma, gali lao liliharibika.

Mwigamba alifukuzwa uanachama Chadema akiwa na wadhifa wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za usaliti.

NDUGAI AZUNGUMZA
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, akizungumzia ajali hiyo, alisema anasikitishwa na ajali zinazotokea mara kwa mara katika eneo la Pandambili.

“Sijui kwa nini Pandambili. Maana ukipaangalia utaamini ni mahala salama kwa kuwa pamenyooka. Lakini mara kwa mara ajali zinatokea eneo hili. Nafikiria kuomba serikali kupitia mamlaka za barabarani paangaliwe kubaini kuna tatizo gani,” alisema Ndugai

Ndugai, ambaye pia ni Mbunge Kongwa (CCM), alisema anashawishika kuamini kuwapo tatizo la kitaalamu katika eneo hilo na kwamba, anafanya mpango kuomba wataalamu wa barabara kufanyia uchunguzi eneo hilo.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa