Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Betty Mkwasa,
amemlalamikia Mbunge wa Bahi, Omar Badwel (CCM), kwa kuwahamasisha
wananchi kuharibu mazingira ikiwa ni pamoja na kufyeka msitu wa hifadhi
ya taifa wa Chenene.
Akizungumza na vyombo vya habari juu ya uharibifu wa mazingira katika
msitu huo, Mkwasa, alisema kuwa wapo wakulima ambao ni wahamiaji
wanaokingiwa kifua na mbunge huyo kwa misingi ya kuangalia jinsi ya
kulinda kura katika uchaguzi mkuu mwakani, bila kuangalia athari za
mazingira.
Mkwasa, aliyasema hayo baada ya kuulizwa swali ni kwanini wananchi wa
wilaya hiyo hususani wakulima, wamevamia msitu huo na kuanza kufyeka
miti wakati msitu huo ni hifadhi.
Alikiri kuwepo kwa wananchi ambao ni wakulima waliovamia msitu huo na
kuanza kufyeka miti kwa malengo ya kuendeleza kilimo, japo walishapewa
tahadhari na kutakiwa kuondoka katika msitu huo.
“Wapo wakulima ambao walivamia hifadhi hiyo kwa lengo la kulima,
lakini serikali imekuwa ikizuia, baada ya kuona hilo, watu wa hifadhi
walilazimika kwenda kuweka mipaka kwa lengo la kuwataka wakulima hao
kuondoka katika hifadhi hiyo…
“Kutokana na hali hiyo, wakulima walikuja ofisini kwangu kwa lengo
la kuomba wasiondoke hadi hapo watakapokuwa wamevuna mazao yao,
kutokana na hali ya ubinadamu, niliwashauri wavune kwanza mazao yao na
baadaye wakimaliza kuvuna wasirudie tena kulima na badala yake waondoke
katika msitu huo…
“Cha kushangaza, mbunge wa jimbo alikwenda katika msitu huo na
kuwaambia kuwa wasiondoke na waendelee kulima, jambo ambalo
limesababisha kuendeleza uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa,
kwani kwa sasa wameanza kufyeka miti na kudai kuwa hawawezi kuhama
kutokana na kauli ya mbunge wao,” alisema Mkwasa.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa misingi ya sheria ya utunzaji wa
mazingira, yeye na timu yake watahakikisha wakulima hao wanaondoka
katika msitu huo mara watakapomaliza kuvuna mazao yao.
Kwa upande wake, mbunge Badwel alipoulizwa kuhusu hilo, alisema ni
kweli wakulima hao ni wa siku nyingi wakiendeleza shughuli zao za
kilimo na wakati wote serikali ilikuwa imelala.
“Haiwezekani watu ambao walianza kulima zaidi ya miaka 50 ukawaambia
waondoke, kwani siku zote walikuwa wapi? Huwezi kuwaondoa watu kama kuku
au bata, mimi nimewaambia hakuna sababu ya wao kuondoka hadi hapo
serikali itakapokaa na wananchi na kutatua mgogoro huo,” alisema
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment