Home » » BUNGE LA KATIBA LAITISHWA,UKAWA NGANGARI

BUNGE LA KATIBA LAITISHWA,UKAWA NGANGARI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe
Bunge Maalumu la Katiba limeitishwa Agosti 5, mwaka huu, huku wajumbe wake wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiendelea na msimamo wao wa kutorejea bungeni hadi yatakapopatikana maridhiano ya msingi.
Kwa mujibu wa taarifa ya kuwaita wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba iliyotolewa jana na Ofisi ya Katibu wa Bunge hilo, wajumbe wote wanatakiwa kuwasili mjini Dodoma kuanzia Agosti 3, mwaka huu, kwa ajili ya kuanza mkutano huo kama ilivyopangwa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Agosti 4, mwaka huu, itakuwa siku maalumu kwa ajili ya mambo ya kiutawala na kwamba, wajumbe wote wanapaswa kufika ofisi za Bunge, majira ya saa 4:00 asubuhi

MBOWE: MSIMAMO WETU ULEULE
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, akizungumza na NIPASHE jana, alisema kitakachowarudisha ndani ya Bunge hilo ni maridhiano ya msingi yatakayorejesha maoni ya wananchi kujadiliwa.

Mbowe alizungumzia msimamo huo wa Ukawa kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) alioutuma kwa mwandishi baada ya kutakiwa kueleza msimamo wa umoja huo kufuatia Bunge hilo kuitishwa.

“Hadi hatua ya sasa ninapoandika sms (ujumbe) hii, msimamo wetu Ukawa uko palepale. Hatutarejea Bunge la Katiba…Labda yawepo maridhiano ya msingi yatakayorejesha maoni ya wananchi kuheshimiwa kupitia Rasimu ya Katiba ya Tume ya Warioba na siyo vinginevyo,” alisema Mbowe.

DK. BANA: WANASIASA HAWAELEWI MARIDHIANO

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema vyama vyote vya siasa vimeshindwa kufahamu maana halisi ya maridhiano na kuyatekeleza kwa vitendo.

“Neno maridhiano ni pana mno. Linahitaji moyo wa ushujaa, uzalendo na kuachia kile unachoamini ni sahihi na kuthamini hoja inayotolewa na mwingine,” alisema Dk. Bana.

Alisema kwa bahati mbaya viongozi vyama vya siasa hawana elimu ya maridhiano na lengo la maridhiano na kwamba, wangejua maana yake kwa mapana na kanuni zake wangeridhiana na Bunge Maalumu la Katiba kuendelea.

“Mathalani, alisema CCM hawajawahi kuwa na maridhiano ndiyo mana hadi leo wanavutana, Chadema wana mgogoro mkubwa hawajaweza kufikia maridhiano, NCCR Mageuzi na CUF hivyo hivyo…vyama vyote vinavyounda Ukawa na wanaoendelea kwenye Bunge wameshakumbwa na migogoro, lakini hawakutumia maridhiano kumaliza,” alisema Dk. Bana.

Alisema dhana ya maridhiano inatamkwa lakini kama haitajitokeza katika dhana ya kisiasa haiwezi kuwa ndani ya Bunge la Katiba na kwamba haiwezi kufanikiwa kufikia maridhiano kwa wanasiasa kuzunguza maridhiano mdomoni na hawajawahi kutumia ndani ya taasisi (vyama) zao za kisiasa.

Dk. Bana alisema kama Ukawa wangekuwa na dhamira ya kweli wangerejea na watafute maridhiano, lakini wameendelea kutoa visingizio jambo ambalo halitasaidia.

“Tuliopo nje tunaona Ukawa wana ajenda yao nje ya Katiba, walivyotoka walizungumza yote yaliyowakera na tuliwaunga mkono, tulijua yatatokea kwa kuwa siyo Bunge jepesi,  lazima Bunge libadilike na kurudi kwenye mstari... lakini walivyotoka wakaanza kuzungumzia uchaguzi mkuu mwaka 2015 na kuweka kando Katiba,” alisema Dk. Bana.

BUNGE LA KATIBA LIENDELEE
Dk. Bana alisema Bunge hilo ni vyema likaendelea kwa mujibu wa sheria na kanuni kwa kuwa hakuna sheria iliyotamka kuwa kundi moja likitoka au watu fulani wakitoka Bunge lisiendelee.

Alisema wajumbe wa Ukawa ni asilimia 22 ya wajumbe wa Bunge hilo, hivyo hawawezi kuathiri matakwa ya asilimia 78 ya wajumbe waliobaki ndani ya Bunge hilo,” alisema Dk. Bana.

Alisema ni vyema Ukawa wakatanguliza maslahi ya Taifa mbele na kuungana na wenzao katika kujadili rasimu ya Katiba na kwamba, kwenda kuitafuta Katiba nje ya Bunge ni sawa na kufanya vurugu zisizo za msingi.

“Tunawapenda sana, walitumia busara kutoka, ujumbe tumeshaupata nasi hatukutarajia mteremko kwenye Bunge hilo, walichukizwa na yaliyokuwa yanaendelea kama lugha za matusi na kutoka nje ya mstari, sasa warudi bungeni kujadili rasimu,” alisema Dk. Bana.

Bunge hilo linaloundwa na wajumbe 639, wakiwamo 201 wa kuteuliwa na Rais na wengine wakiwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar awali lilipewa siku 70 na nyongeza ya siku 20 kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Bunge hilo lililoanza Februari 18, mwaka huu, lilitumia takriban siku 21 za mwanzo kujadili na kupitisha kanuni za kuliongoza, ikiwamo kuunda kamati 16, kati ya hizo, 12 za kujadili sura za Rasimu ya Katiba.

Kamati hizo zilijichimbia katika kumbi mbalimbali mjini Dodoma na kujadili sura ya kwanza na ya sita, huku mjadala mzito uliosababisha Bunge kuingia kwenye mvutano mkubwa ni sura ya sita inayozungumzia muundo wa Muungano.

Kundi la wajumbe wengi, wakiongozwa na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatetea muundo wa sasa wa serikali mbili uendelee kwa maelezo kuwa ndio utakaodumisha Muungano.

Kundi la Ukawa linaloundwa na vyama vya upinzani, vikiwamo Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na baadhi ya vyama vidogo lilisimamia serikali tatu kwa hoja kwamba, rasimu ilipendekeza serikali tatu kutokana na maoni ya wananchi.

Aidha, baada ya kamati hizo kumaliza kazi na kurudi kama Bunge Maalumu, wenyeviti wa kamati hizo waliwasilisha taarifa ya wengi, huku wengine wakiwasilisha ya wachache.

Hata hivyo, mjadala huo ulijikita katika kurushiana vijembe, maneno yasiyo na staha, matusi, kudhihaki waasisi, kumshambulia Jaji Warioba kwamba alichakachua takwimu na kupendekeza serikali tatu kwa maslahi yake binafsi.

Hata hivyo, wakati mjadala wa sura hizo ukiwa katikati, kundi la wajumbe wanaounda Ukawa walitoka nje ya ukumbi Aprili 16, mwaka huu, kususia mchakato huo kwa madai kwamba, CCM imeliteka Bunge na mjadala huo kutokana na kufuta mapendekezo ya tume ya sura hizo mbili na kupenyeza rasimu yake.

Hadi Bunge hilo linaahirishwa, ngwe yake ya kwanza Aprili 25, mwaka huu, wajumbe wa Ukawa walikuwa nje ya Bunge kwa takriban siku tisa, huku wakianza kuzunguka maeneo kadhaa ya nchi kuwaeleza wananchi juu ya mwenendo wa Bunge kupitia mikutano ya hadhara.

Bunge hilo liliahirishwa kupisha Bunge la Bajeti, Mei, mwaka huu na litaendelea tena Agosti 5, mwaka huu kwa siku 60 zilizoongezwa na Rais Kikwete.

Rais Kikwete aliliongeza Bunge hilo kufanyika siku 60, baada ya kuombwa na Mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
Sitta alifikia hatua hiyo, baada ya kuona kwamba siku 70 zimeemalizika kwa kujadili sura mbili tu bila hata kufikia makubaliano.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa