Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, ametoa wiki moja kwa
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (Duwasa),
kung’oa mara moja mifumo ya maji isiyotakiwa katika visima vilivyopo
ndani ya viwanja vya maonyesho ya wakulima ya Nane Nane eneo la Nzuguni
ili kuondoa mzozo uliopo.
Dk. Nchimbi, alitoa agizo hilo mjini hapa juzi, wakati wa mkutano wa
maandalizi ya sherehe hizo za wakulima (Nanenane), Kanda ya Kati
zinazotarajiwa kuzinduliwa Agosti Mosi, ulioshirikisha wadau
mbalimbali.
Alisema ni suala la upuuzi na aibu kwa Duwasa na Umoja wa Wakulima
Kanda ya Kati (Taso), ambazo zote ni taasisi za serikali, kuleta mzozo
unaozorotesha utendaji kazi katika eneo hilo na maonyesho ya Nanenane
ambayo hufanyika kila mwaka.
“Nimeshagazwa sana kuona kunatokea jambo kama hili, hapa kuna vitu
ambavyo vinapingana, maana nichojiuliza ni kwanini Duwasa waingilie na
kuingiza mifumo yao na kuondoa kasi ya huduma wakati ilipaswa
kuhakikisha huduma ya maji inaboreshwa Nanenane?” alihoji Dk. Nchimbi.
Alifafanua kuwa mamlaka hiyo imeweka mfumo wake wa maji katika visima
pamoja na matenki ya Taso na watu waliopo katika eneo hilo, lakini cha
kushangaza maji hakuna na hivyo kukwamisha maonyesho.
Alisema itaonekana haina maana kama watakuwa wanawahamasisha wananchi
kuchimba visima halafu wanakwamishwa na Duwasa, kutokana na wao kuweka
mfumo ambao hauna maji na kwamba, masuala hayo ni ya kipuuzi na
hawawezi kuendelea na malumbano wakati kuna mambo yanaharibika, ndio
maana yeye kama rais wa mkoa, ameamua kutoa agizo mara moja na kuwapa
wiki moja tu kulitekeleza.
Alisema haipendezi kwa mamlaka hiyo kuingia kimaslahi katika eneo
hilo na kudhoofisha maonyesho hayo, badala yake waingie kwa kuboresha
kwa pamoja na kuhakikisha ufanisi unapatikana.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Katibu Tawala Mkoa ambaye ni Mjumbe wa
Bodi ya Duwasa, Rehema Madenge, alisema kuwa mamlaka hiyo inafanya
kazi kwa mujibu wa sheria ya mamlaka za maji mijini, hivyo eneo la
maonyesho Nzuguni wanahusika.
Sambamba na hilo, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Dodoma na maeneo
jirani, kushiriki kikamilifu katika maonyesho hayo licha ya kuwa
kitaifa yanafanyikia Mkoa wa Lindi na kuondokana na dhana ya
kutoyathamini kwa kuwa yanafanyika kikanda
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment