Home » » JAJI BOMANI ATABIRI MGOGORO BUNGE LA KATIBA

JAJI BOMANI ATABIRI MGOGORO BUNGE LA KATIBA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwanasheria Mkuu Mstaafu,Jaji Mark Bomani,akizungumza na waandishi wa habri,Jijini Dar es Salaam.
Wasiwasi wa kutofikiwa mwafaka na kuendelea kwa mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuhusu muundo wa serikali, umezidi kutanda miongoni mwa wananchi, huku Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali akishauri suala hilo liwekwe kando.
Mwanasheria huyo ana mwanasiasa mkongwe nchini, Jaji Mark Bomani, alitoa ushauri huo, huku akisema wajumbe wajikite katika kujadili mambo mengine yaliyomo kwenye rasimu ya katiba badala ya kung’ang’ania muundo wa Muungano.

Mambo hayo, aliyataja kuwa ni kama vile usawa wa uwakilishi wa jinsia, tunu za taifa, mgombea binafsi, mawaziri kutokuwa wabunge na kuwaomba wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni kujadili mambo hayo, ambayo alisema hayawezi kuleta ubishi, malumbano wala mgawanyiko miongoni mwao.

Jaji Bomani alitoa ushauri huo, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kutoa maoni yake juu ya mchakato wa katiba mpya na mustakabali wa nchi.

Alisema haoni uwezekano wa mwafaka kufikiwa baina pande mbili ambazo zimekuwa zikilumbana, kwa kuwa majadiliano yaliyokwishafanyika katika Bunge hilo kuhusu suala hilo yamekuwa yakifanyika kwa misingi ya kiitikadi na maslahi binafsi zaidi.

“Nina wasiwasi kama mwafaka au maridhiano yatapatikana Agosti, mwaka huu, Bunge Maalumu litakapokutana. Zimejitokeza tofauti kubwa za kimtizamo au kiitikadi bila kusahau maslahi binafsi,” alisema Jaji Bomani.

Alisema tofauti hizo hazimpi matumaini kwamba, mwafaka au maridhiano yatapatikana, hasa juu ya suala muhimu la idadi ya serikali, kwa kuwa bado zipo palepale.

“Nina shaka pia kama pana utashi wa kutosha toka kwa baadhi ya viongozi wa nchi,” alisema Jaji Bomani.

Alisema pia ana mashaka kama kura za kutosha theluthi mbili za wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili za wajumbe kutoka Zanzibar zitapatikana mwisho wa mjadala.

Jaji Bomani alisema katiba ni kitu, ambacho lazima kwanza upatikane mwafaka wa wengi, vinginevyo kukiwa na kundi linalopinga ni hatari, kwani malumbano yaliyojitokeza yalifikia kutishia hata Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema haoni kuwa ni sawa mchakato wote wa katiba ukwamishwe na suala la idadi ya serikali.

“Yale, ambayo yanaweza yakaafikiwa yangeweza kuingizwa ndani ya katiba tuliyonayo, tena bila ya kuhitaji kura ya maoni, kwa maoni yangu, hatua kama hii ingeiboresha kwa kiwango kikubwa katiba tuliyonayo,” alisema Jaji Bomani.

Aliongeza: “Kwa mfano, kuna suala muhimu la uwakilishi sawa wa jinsia, yaani asilimia 50 wanaume na asilimia 50 wanawake kwenye vyombo vya uwakilishi kama vile kwenye Bunge, kwenye halmashauri za wilaya nakadhalika. Suala la mawaziri kutokuwa wabunge nalo pia nafikiri lingeweza likajadilika na mwafaka kupatikana. Ndiyo mtindo wa Marekani, Ufaransa na Kenya jirani zetu.”

Alisema pia muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi nao ungeweza kujadiliwa na kupatiwa mwafaka, vilevile suala la mgombea huru linajadilika na lile la tunu za taifa nalo pia lingeweza likajadiliwa na kupatiwa muafaka ili nchi iwe na dira inayoeleweka.

Jaji Bomani alisema hayo ni baadhi tu ya masuala, ambayo yangeweza kujadiliwa na kupatiwa muafaka na kuingizwa kwenye katiba iliyopo bila ya kukwamishwa na suala la idadi ya serikali.

Alisema kama uwezekano wa kukubaliana juu ya idadi ya serikali haupo siyo sawa kukwamisha masuala mengine yote.

“Kama suala la idadi ya serikali haliwezekani kwa sasa kwanini tusiliweke kiporo mpaka wakati muafaka?...Liliwachukua wenzetu wa Kenya miaka 10 kukubaliana juu ya katiba mpya. Mimi binafsi na kitaaluma ningependa sana tupate katiba mpya, tena mshabiki wa serikali tatu, lakini siyo kwa gharama yoyote,” alisema Jaji Bomani.

Aliongeza: “Napendekeza kwamba Bunge Maalumu likikutana mwezi ujao liweke kando kwanza suala la idadi ya serikali ili liyaangalie yale masuala mengine, tuseme kwa wiki mbili hivi.

Halafu liamue kuahirisha suala la idadi ya serikali mpaka wakati muafaka. Labda hata baada ya uchaguzi wa 2015. Tuna katiba inayofanyan kazi, ingawa ina dosari. Tunaweza endenelea nayo hadi wakati mwafaka.”
“Kusema kweli suala la idadi ya serikali lingekuwa suala zuri sana kulitia kwenye ilani za uchaguzi za vyama mbalimbali. Kwa sababu hii ningewasihi wenzetu wa Ukawa warudi bungeni, angalau kwa haya mengine.”

Alisema anaamini kama italazimishwa uamuzi juu ya suala la idadi ya serikali, nchi itaingizwa kwenye tafrani kubwa, ambayo matokeo yake yanaweza kuvuruga amani, kudumaza maendeleo ya nchi na wananchi nap engine kusababisha kuvunjika kwa Muungano.

Jaji Bomani alisema haiwezekani kuendelea na mjadala usio na matumaini ya mafanikio, kwani tayari zaidi ya Sh. bilioni 60 zimekwishatumika kulipa wajumbe wa Bunge hilo, mbali na mabilioni mengine, ambayo yametumika kuwalipa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Fedha hizi zinahitajika kwa maendeleo ya wananchi. Lazima sote tuwe na uchungu nazo,” alisema Jaji Bomani.
UKAWA WAJIBU
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, alipotakiwa kuzungumzia maoni hayo ya Jaji Bomani, hasa ombi lake la kuwataka warejee bungeni, alisema: “Tunamshukuru kwa ushauri wake. Tutautafakari.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa