Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MADIWANI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa
Dodoma, wamewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuachana na
siasa za maji taka na wajikite kutatua umasikini wa Watanzania.
Kauli hiyo waliitoa juzi walipokuwa wakizungumza na waandishi wa
habari katika ofisi za gazeti hili baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa
wanapanga kujiengua CHADEMA muda wowote kuanzia sasa baada ya
kununuliwa na CCM.
Diwani wa Kata ya Dodoma Makulu, Ally Bilingi, alisema uzushi huo
unaoenezwa na viongozi wa CCM kwa kushirikiana na wafuasi wao,
unadhihirisha ukomavu wa rushwa na ununuzi wa uongozi unaofanywa na
chama hicho tawala.
“Umefika wakati wa makada wa CCM kuanza kuweweseka, mimi niliingia
CHADEMA kwa mapenzi yangu mwenyewe baada ya kuona CCM hawana sera na
wanaficha ukweli kutokana na kulindana katika ufisadi…
“Lakini najua wazi kuwa CCM ili uweze kushika madaraka ni lazima
uwe mtu wa kutoa rushwa, viongozi wengi wapo katika madaraka kutokana
na vitendo vya kununua nafasi hizo, watafute hoja za kuwaeleza
Watanzania, lakini siyo siasa za maji taka za kuwashawishi watu, eti
sisi madiwani wa Dodoma tunaweza kununuliwa,” alisema.
Diwani wa Kata ya Ipala, Hamisi Nghumba, alisema si mara ya kwanza
viongozi wa CCM kumfuata na kutaka aondoke CHADEMA na kuhamia kwao.
“Wamekuwa wakinifuata na kuniahidi kunipa fedha nyingi, lakini
nimewakatalia siku zote, CCM kwa sasa wanatafuta kila mbinu ya
kusambaratisha CHADEMA Mkoa wa Dodoma, lakini kutokana na chama hiki
kuota mizizi kwa sasa hawawezi,” alisema.
Diwani wa Viti Maalum, Jemima Salali, alisema kuwa kwa misingi ambayo
ameishaiweke katika maeneo mbalimbali ndani ya chama, kamwe hawezi
kuondoka CHADEMA.
Diwani wa Iyumbu, Ezron Kudugwa, alisema CCM kwa kutumia makada wao
wanatafuta njia ya kudhoofisha viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA kwa
kuwapandikizia uongo ili wakate tamaa.
“Kama viongozi wa juu katika chama wakisikia mambo kama hayo
wanashituka, lakini kiukweli mimi pamoja na madiwani wenzangu kamwe
hatuwezi kuondoka CHADEMA,” alisema
Chanzo:Tanzani Daima
0 comments:
Post a Comment