Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kinamama walio karibu na familia ya marehemu Isabela Andrew aliyebakwa
hadi kufa wakiangua kilio baada ya kushuhudia mahali mwili wake
ulipokutwa huko Area C mjini Dodoma jana.
Mfanyakazi wa ndani, Isabella Andrew (18), amefariki dunia na
kifo chake kikidaiwa kusababishwa na kubakwa na watu wasiojulikana.
Mwili wa msichana huyo ulikutwa ukiwa umeharibika
katika moja ya pagale, lililopo Area C, Dodoma Mjini na mwandishi wetu
alishuhudia ukitolewa hapo kwa machela huku polisi wakiwahoji mashuhuda
wa tukio hilo.
Mkazi wa Mtaa wa Kiwanja cha Ndege, Jackson Coy
aliyekuwa akiishi na binti huyo alisema msichana huyo alipotea tangu
Jumamosi iliyopita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime,
alisema mwili huo uliokotwa jana saa mbili asubuhi na kwamba polisi
wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake.
Mwili huo ulibainika baada ya mama mmoja, Rehema
Msambile kufika katika pagale hilo alipokuwa akifuatilia nyendo za mtoto
wake ambaye juzi alipigwa kwa tabia ya utoro shuleni.
“Niliamua leo (jana) kumfuatilia, nikaanza katika mapagale.
Nilipofika hapa ndipo nikaona mwili wa marehemu ikabidi nimuite jirani hapo aje aone,” alisema.
Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Henry
Kandenga alisema mazingira yanaonyesha kuwa binti huyo alibakwa kwa
sababu walikuta nguo za ndani zikiwa pembeni.
“Hakuna yowe iliyosikika kwamba kuna mtu anauawa
ukizingatia kwamba nyumba ziko jirani na hata nyumba aliyokuwa akiishi
ni jirani na mahali alipokutwa,” alisema.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment