Home » » WANAFUNZI JELA KWA KUMUUA MWALIMU WAO BILA KUKUSUDIA

WANAFUNZI JELA KWA KUMUUA MWALIMU WAO BILA KUKUSUDIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, imewahukumu wanafunzi wawili waliokuwa kidato cha tatu mwaka 2008 katika Sekondari ya Chemchem, Wilaya ya Mkalama, kutumikia kifungo cha miaka sita jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwalimu wao wa nidhamu bila kukusudia.
Washtakiwa hao Shani Mtua na Mohammed Salimu, ambao wote wakati huo umri wao ulikuwa miaka 18, walihukumiwa kifungo hicho na Jaji Rehema Mkuye katika Mahakama hiyo iliyoanza vikao vyake jana mjini Singida.

Jaji  Mkuye alitoa hukumu hiyo baada ya washitakiwa hao kukiri shitaka dogo la kuua bila kukusudia katika Kijiji cha Mpambala kilichopo Tarafa ya Kirumi Wilaya Iramba (sasa Wilaya Mkalama) mkoani Singida.

Mapema Mwanasheria wa Serikali, Zakaria Elisaria, aliyekuwa akisaidiwa na Karen Mrango alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa walimuua mwalimu huyo Rajabu Idude (49), aliyekuwa  wa nidhamu shuleni hapo, Agosti 21, 2008, saa 1.00 usiku.

Alidai chanzo cha mauaji hayo ni mshitakiwa wa kwanza kupewa barua saa 3.00 asubuhi siku hiyo ya kusimamishwa masomo kwa wiki mbili kwa   utovu wa nidhamu hali iliyomlazimu awashawishi wenzake watatu kumpiga mwalimu huyo.

Zakaria alidai washtakiwa hao walimuua mwalimu huyo kwenye kichaka kilichokuwa jirani na shule hiyo  kwa kumpiga ngumi na mateke kisha kumjeruhi mwilini kwa kuchoma kwa kisu alichokuwa nacho mshitakiwa huyo wa kwanza wakati akirudi nyumbani kutoka kwenye  klabu ya pombe za kienyeji.  

Alidai kuwa kutokana na kipigo hicho, mwalimu huyo alipiga yowe kuomba msaada zilizosababishwa mwanaye, Maye Rajabu kufika haraka kwenye eneo la tukio hilo.

Alidai wakati akifika kwenye eneo hilo, alimkuta baba yake amefariki dunia, huku washitakiwa hao wakiwa wametoweka mahali hapo baada ya kukimbilia  katika nyumba waliyokuwa wamepanga.

Mwanasheria huyo alidai baadaye ulifanyika msako usiku huo na kufanikisha kukamatwa kwa washtakiwa wanne  kisha kuhojiwa kuanzia ngazi ya mlinzi wa amani kwenye kijiji hicho hadi jana mahakamani walikiri, na akaiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwao na kwa wanafunzi wengine wenye tabia kama zao.

Hata hivyo, ilidaiwa  kuwa washitakiwa wengine wawili; Emmanuel Daud na Michael Msengi, walifariki dunia wakiwa mahabusu gerezani, wakisubiri kesi hiyo kusikilizwa na Mahakama Kuu.

Wakili wa washitakiwa hao  kutoka kampuni ya Kim & Company. Advocates, Raymond Joackim, alimwomba Jaji Mkuye kutoa adhabu nafuu dhidi ya wateja wake kutokana na kuonyesha ushirikiano mkubwa tangu siku waliyokamatwa.

Aidha, Joackim alidai washitakiwa hao walifanya kosa hilo kutokana na kusukumwa na umri mdogo (utoto), ni wakosaji wa mara ya kwanza, wanajutia kosa hilo pia tayari wamekaa gerezani kwa muda mrefu wa miaka sita, hivyo tayari wamejifunza kutokana na mauaji hayo.

Akitoa hukumu, Jaji Mkuye alisema hakuna ubishi kwa yote aliyosema wakili wa utetezi, lakini pia anadhani sababu hizo siyo kibali kwa washitakiwa, waliokuwa wanafunzi wakati huo kupanga na kutekeleza mauaji dhidi ya mwalimu wao aliyekuwa anasimamia nidhamu.

“Nadhani kosa walilofanya haliwezi kukubalika kwa jamii hata kidogo…fujo zimekuwa zikitokea kwenye shule na vyuo, hata kusababisha vurugu kiasi cha kuathiri utendaji…, kufuatia kosa hili, kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka sita jela,”alisistiza Jaji Mkuye katika hukumu hiyo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa