Home » » WANANCHI KUENDESHA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MKOANI DODOMA

WANANCHI KUENDESHA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MKOANI DODOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

IMEELEZWA kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuchimba maji ardhini na kuendesha kilimo cha umwagiliaji licha ya mkoa huo kijiografia kuwa na hali ya ukame.

Hayo yalielezwa jana mkoani hapa na Mkurugenzi wa Utafiti wa Kilimo na Maendeleo Kanda ya Kati, Leon Mroso wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kilimo cha umwagiliaji.

Mroso alisema kuwa Mkoa wa Dodoma ni moja kati ya mikoa ambayo hupata mvua kidogo huku ardhi yake ikiwa na maji mengi ambayo alisema endapo yatachimbwa yanaweza kusaidia kilimo cha umwagiliaji.

“Dodoma inapata mvua milimita 500-600 kwa mwaka ambapo kwa takwimu hizo hiyo ni mvua kidogo sana...

“Kutokana na kuwepo kwa maji mengi ardhini kuna uwezekano mkubwa wa kutumia mashine za kuvuta maji hayo kwa ajili ya umwagiliaji,”alisema Mroso.

Aidha aliitaka jamii nchini kujiunga katika vikundi kwa lengo la kupata mkopo katika taasisi za kifedha nchini ili kuwawezesha kuchimba visima na kununua mashine za kuvutia maji pamoja na kufanikisha kilimo cha umwagiliaji mkoani hapo.

“Kama vikundi vitajiunga mfano pale ambapo hakuna umeme wakanunua vipande vya umeme jua kama 60 hivi wanaweza kuendesha mashine za kuvuta maji na kufanya kilimo cha umwagiliaji kuwa na tija kubwa,” alisema.

Hata hivyo aliwataka watafiti nchini kujenga tabia ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa jamii hasa wakulima ili kuweza kutimiza lengo la kilimo hicho ikiwa ni pamoja na kuvuna maji ya mvua.

Chanzo:Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa