Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAUGUZI wa Zahanati ya Izava, iliyopo Kata ya Segala, Wilaya ya
Chamwino mkoani Dodoma, wamelalamikiwa kwa kitendo cha kuwatoza sh
6,000 kwa kila mzazi anayejifungulia nyumbani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima Jumapili, wajawazito
hao walisema kuwa wauguzi wa zahanati hiyo wamekuwa na tabia ya
kuwatoza fedha hizo wanapojifungua nyumbani na kuwapeleka watoto
hospitalini.
Mmoja wa wajawazito hao, Mwanaidi Bakari, alisema miongoni mwa sababu
zinazowafanya wajifungulie nyumbani ni wauguzi hao kuwataka waende
zahanati wakiwa na wakunga wao wa jadi ili wawasaidie.
Alisema kutokana na hali hiyo, wajawazito waliamua kujifungua
nyumbani kwa kuona kwamba wauguzi wenye taaluma wanashindwa kuwasaidia
bila kuwategemea wakunga.
“Tunashangaa, kwa kitendo hicho wengi wetu tumeamua kujifungulia
nyumbani na wakunga wa jadi, lakini cha ajabu tunatozwa kiasi cha fedha
sh. 6,000,” alisema Mwanaidi.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, James Charles, alisema si
utaratibu wa serikali kutoza fedha hizo na kueleza kuwa ni kinyume na
taratibu na kuwataka wananchi kutoa taarifa ili hatua za kisheria
zifuatwe.
“Hatuwezi kuvumilia kitendo hicho, wanalipwa mishahara na serikali
kwa ajili ya kuwahudumia wanajamii pindi wanapohitaji huduma za
kiafya,” alisema Charles.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment