BARAZA la Vyama vya
Siasa nchini, jana limetoa msimamo wake likitaka Bunge Maalumu la
Katiba, liendelee na mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya ambao upo kwa
mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Mwenyekiti wa baraza
hilo, Bw. Peter Mziray, alisema shinikizo linalotaka Rais Jakaya Kikwete
alivunje Bunge hilo haliwezekani kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria
zilizopo.
Alisema wananchi
wanapaswa kufahamu kuwa, suala la Katiba ni jambo nyeti na marais wengi
duniani wanaogopa kuliweka suala hilo mezani ili lizungumzwe.
"Kikao kilichoitishwa
na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), Agosti 2 mwaka huu, kilikutanisha
viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na hakikuwa rasmi hivyo waliosema
tulikubaliana mchakato huu usimame watoe ushahidi wa maandishi au
kupeleka suala hilo mahakamani," alisema.
Aliongeza kuwa, katika
kikao hicho walikubaliana mambo mengi na jambo moja lililobaki lipo
kisheria kwani unapoamua kufanya maridhiano lazima uweke silaha chini.
Wakati huo huo, Bw.
Mziray alitoa taarifa za kuahirishwa kwa kongamano lililopangwa
kufanyika mjini Dodoma Agosti 23-24 mwaka huu, ambalo lilikuwa na lengo
la kujadili mchakato huo pamoja na changamoto zake.
Alisema kongamano hilo
lililenga kuwashirikisha viongozi wastaafu wa awamu zilizopita, viongozi
mbalimbali wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, viongozi wa
dini, wazee wastaafu na wakuu wa usalama nchini.
"Tumeahirisha kongamano
hili kutokana na kiongozi mmoja kuwa na udhuru; hivyo tumeona ni bora
tuliahirishe kutokana na unyeti wa jambo hili kuwa na umuhimu mkubwa
katika nchi yetu," alisema Bw. Mziray.
Bw. Mziray alisema
uamuzi wa kuandaa kongamano hilo ulitokana na Kikao cha baraza hilo
pamoja na vyama vya siasa kilichofanyika Agosti 2 mwaka huu na kutoa
pole kwa familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
nchini (NEC), Jaji mstaafu Lewis Makame, aliyefariki juzi, jijini Dar es
Salaam.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment