Home » » CCM YAJIPA MTIHANI

CCM YAJIPA MTIHANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
 
Kelele ambazo zimepazwa na watu wa kada mbalimbali nchini dhidi ya mchakato wa Katiba mpya zimeifanya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukutana kwa dharura, huku kukiwa na taarifa ndani ya chama hicho kuwa kuna hoja zinazokinzana juu ya kuendelea au kusitishwa kwa muda kwa Bunge Maalum la Katiba.
Kikao hicho kinachokutana mjini hapa leo, inadaiwa kitajadili miito ya wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa kauli za kumtaka Rais Jakaya Kikwete aliahirishe Bunge Maalum la Katiba linaloendelea na vikao vyake hadi hapo maridhiano yatakapopatikana baina ya CCM na wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Bunge hilo lililorejea katika ngwe ya pili Agosti 5, mwaka huu baada ya kuahirishwa Aprili 25, mwaka huu kupisha mkutano wa bajeti sasa linahudhuriwa na wajumbe wengi kutoka CCM, wachache kutoka kundi la 201 na wachache zaidi kutoka vyama vidogo vya siasa.

Wajumbe wengi wa vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walitoka nje ya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu wakilalamikia mambo mbalimbali ikiwamo Bunge hilo kuweka kando Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti  Jaji Mstaafu Joseph Warioba na kujadili rasimu mbadala ya CCM.

Wadau hao wanapendekeza kwamba Bunge hilo liahirishwe hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kumalizika.

Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya chama hicho, kimeeleza kuwa kikao hicho cha leo kilitanguliwa jana jioni na kikao kingine cha Sekretarieti ambacho hupanga ajenda zitakazojadiliwa.

“Baadhi ya viongozi wa juu, tayari wameshawasili akiwamo Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula ambaye alishinda jana kutwa nzima hapa ofisini akijaribu kuandaa mazingira, Pia nimemuona Nape Nnauye, lakini Rais Kikwete   ambaye ni Mwenyekiti wa CCM yeye ataingia kesho (leo) asubuhi kwa ndege…Na jioni hii (jana) tunampokea Katibu Mkuu (Abdurahaman Kinana),” kilisema chanzo hicho.

NIPASHE lilimshuhudia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiwasili mjini hapa majira ya saa 8:36 mchana akitokea jijini Dar es Salaam na kukutana faragha na baadhi ya mawaziri katika ukumbi wa Mkapa.

Wajumbe wa kamati kuu waliotakiwa kuwa wamefika Dodoma kwa ajili ya kikao hicho ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Stephen Wassira; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka; Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa; Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Pindi Chana.

Wengine ni Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi; Dk. Salim Ahmed Salim,  Profesa Makame Mbarawa, Dk. Maua Daftari, Hadija Aboud  na Waziri wa Nchi, Ofisi Makamu wa Rais (Muungano), Samia Hassan Suluhu.

Taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa miito ya wadau inayotolewa hivi sasa kila kona ya nchi, ikimtaka  Rais Kikwete aliahirishe bunge hilo, imekuwa ikimpasua kichwa na kwamba kilichozungumzwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema mwishoni mwa wiki iliyopita alisema ni maono ya serikali kukubaliana na wadau, lakini kwa sharti la kuwaanda kisaikolojia Watanzania.

“Zipo ajenda nyingine ambazo nadhani zitajadiliwa, lakini kubwa ni hoja zinazotolewa na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, shinikizo la vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutaka maridhiano na Rais Kikwete baada ya kususia Bunge Maalum la Katiba, kupokea taarifa ya Kamati ya Maadili ambayo ilipewa kazi ya kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada wake waliofungiwa kwa muda wa mwaka mmoja,” chanzo hicho kilisema.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa kutokana na joto la kisiasa kupanda hususani shinikizo la kutaka kutafutwa kwa maridhiano na kuahirishwa kwa Bunge hilo vinaweza kuwafanya CCM walegeze msimamo wa kuendelea na vikao vya Bunge Maalum.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipozungumza na NIPASHE jana jioni, alisema kwamba  ajenda ya kikao hicho ni kupokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa Bunge Maalum la Katiba.

Nape alisema kikao hicho ni mfululizo wa vikao vya Kamati Kuu na siyo cha dharura ila ni kamati maalum.

Nape aliongeza kuwa katika kikao hicho watapeana taarifa kuhusu mambo yanayoendelea katika Bunge Maalum la Katiba.
Nape alikanusha taarifa kwamba kikao hicho pia kitajadili suala la wanachama wake sita waliopewa dhabu ya mwaka mmoja kutojihusisha na shughuli za chama hicho na kuwa chini ya uangalizi kutokana na tuhuma kuwa walianza kufanya kampeni kabla ya muda rasmi kinyume cha kanuni na taratibu za CCM.

Wanachama hao waliochukuliwa hatua hiyo Februari mwaka huu ni mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano), Stephen Wassira; Naibu waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

“Wanaosema kuja ajenda kuhusu adhabu ni uzushi, ni maneno ya mitaani,” alisema Nape na kuongeza kuwa watu wasijenge hali ya wasiwasi na kwamba chama hicho kitatoa taarifa rasmi baada ya kikao hicho.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa