Home » » KATIBA ;MWISHO

KATIBA ;MWISHO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Viongozi wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakishikana mikono ikiwa ni ishara ya umoja mara baada ya kuongea na wandishi wa habari kutoa tamko lao kuhusu Wito uliotolewa na Viongozi wa Dini wa kuwataka kurudi Bungeni. Kutoka kushoto ni katibu mkuu wa NCCR mageuzi Mosena Nyambabe ,mwenyekiti wa chadema Freeman Mbowe ,Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba,Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Jaqmes Mbatia na katibu mkuu wa Chadema Wilbrod Slaa wakiwa nje ya makao makuu ya cuf (Picgha na Omar Fungo)
Kuna kila dalili kwamba mchakato wa Katiba mpya unafikia ukomo kabla ya muda wake baada ya jana Rais Jakaya Kikwete, kutoa msimamo wake na kujiweka mbali na lawama kwamba ndiye aliyeingilia mchakato huo, huku Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukisisitiza achukue hatua kuukamua.
Hali hiyo inajitokeza wakati Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, amekwisha kuitisha Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma kuendelea na ngwe ya pili ya kupitisha rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Aprili, mwaka huu.

Jana kwa nyakati tofauti misimamo inayokinzana kuhusu mchakato huu ilitolewa, kwanza na Ukawa wakisisitiza kuwa ni miujiza kwao kurejea bungeni kama masharti waliyotoa ikiwamo kujadiliwa kwa rasimu kama ilivyowasilishwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba hayatatekelezwa.

Ukawa pia wanasisitiza Rais Kikwete aingilie kati kukwamua mchakato huo wakimtuhumu kwamba kwenye hotuba yake ya ufunguzi ndipo mambo yalipoharibikia.

Hata hivyo, akihutubia Taifa jana katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema hivi karibuni amekuwa akilaumiwa kuwa mambo yalikuwa yanaenda vizuri mpaka pale alipotoa hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika.
Pia alisema amekuwa akilaumiwa kwamba anawezaje kuikana Rasimu ya Katiba ambayo na yeye alikuwa ni mmoja wa watu waliotia sahihi katika Rasimu hiyo.

Akijibu madai hayo, Rais Kikwete alisema wanaotoa madai hayo yameitafsiri isivyo sahihi yake katika Gazeti la Serikali lililotangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Tume kumaliza kazi yake ya kuandika Rasimu ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano amepewa kazi tatu kufanya. 

Alizitaja kazi hizo kuwa ni kupokea Rasimu hiyo na Taarifa ya Tume kutoka kwa Mwenyekiti, kuitangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume kwa watu wote kuiona na kuisoma ndani ya siku 30 na kuitisha Bunge Maalumu
Rais Kikwete alisema katika kutangaza katika Gazeti la Serikali sharti linamtaka anayetangaza ajitambulishe kuwa yeye ni nani na atie sahihi yake.

Alisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo, hakumfanyi yeye kuwa naye ni mhusika na maudhui ya kila kinachopendekezwa na Tume.
"Sahihi zilizomo ndani ya Rasimu na Taarifa ya Tume ni za Wajumbe wa Tume, kamwe sahihi ya Rais haimo hivyo hawezi kulaumiwa kuwa anaikana sahihi yake.  Yeye ametimiza wajibu wake wa kutangaza, akaiweka hadharani kwa umma wa Watanzania kuiona na kusoma Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume vilivyotayarishwa na  kutiwa sahihi na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Aidha, alisema suala lingine ni madai kwamba alikuwa anapata taarifa ya maendeleo ya mchakato ndani ya Tume mara kwa mara na sasa inakuwaje atoe maoni tofauti kama aliyoyatoa katika hotuba yake kwenye Bunge Maalumu.

Alisema ni kweli kabisa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, Makamu wake, Jaji Agustino Ramadhani na Dk. Salim Ahmed Salim, walikutana na yeye kwa nyakati mbalimbali kuzungumzia mwenendo wa mchakato.

Hata hivyo, alisema hayakuwa mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika maudhui na mapendekezo ya Tume. 
"Ukweli ni kwamba Rasimu zote mbili nilizipata mara ya kwanza nilipokabidhiwa rasmi, tena kwa uwazi. Napenda watu wasijenge dhana kuwa nilipewa Rasimu na kuisoma kabla ya kukamilika na hivyo nilitoa maoni yangu.

Tume hii ilikuwa huru na niliiacha iwe hivyo.  Sikuiingilia kwa namna yoyote ile kupenyeza mambo ninayotaka yawemo," alisema.
Kuhusu madai kwamba mambo yalikuwa yanakwenda vizuri na kwamba hotuba yake iliyavuruga, alisema kuwa lawama hizo hazina ukweli wowote na hayana msingi wowote.

"Kwani mimi hasa siku ile nilifanya lipi la ajabu. Ukweli ni kwamba nilisema yale yale ambayo Tume yenyewe imeyasema katika Rasimu ya Katiba na Taarifa za Tume.

Niliyoyasema kuhusu malalamiko ya watu wa pande zetu za Muungano na uzuri na changamoto za miundo ya Serikali mbili na Serikali tatu ni yale yale yaliyomo kwenye taarifa za Tume.  Nimetumia takwimu zile zile za Tume.  Pengine kilichoonekana kuwa kibaya ni jinsi nilivyozifasiri taarifa hizo na mapendekezo ya Tume," alisema.

Aliongeza:"Jambo lingine ambalo nimelifanya ni kutoa maoni yangu kuhusu baadhi ya vipengele vya Rasimu hususan uandishi na dhana mbalimbali zilizokuwamo.  Silioni kosa langu kwa kufanya hivyo, kwani Rasimu imetolewa hadharani kwa watu kuijadili.  Na mimi kama raia ninayo haki ya kufanya hivyo kama wafanyavyo wengine.  Kwa nini nilaumiwe kwa kutumia haki yangu hiyo."

Alisema lakini pia yeye ndiye Rais wa nchi, anayo dhamana ya uongozi na ulezi wa taifa.
"Itakuwaje kwa jambo kubwa la hatima ya nchi yetu nilinyamazie kimya.  Watanzania wangeshangaa na wangekuwa na haki ya kuhoji Rais wao ana maoni gani," alisema.

Rais Kikwete aliongeza kuwa na kwa bahati nzuri alitoa maoni yake mahali penyewe hasa, na kwa uwazi, kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Hata hivyo, alisema ni muhimu kusisitiza kuwa hakutoa maoni yake kama maagizo wala kushurutisha na ndiyo maana kila wakati aliwakumbusha Wajumbe kuwa mamlaka ya uamuzi ni yao.

"Yangu yalikuwa maoni tu wana hiyari ya kuyakubali au kuyakataa.  Niliwataka Wajumbe wasome na kuielewa vyema Rasimu.  Nilisema wasome sura kwa sura, mstari kwa mstari na neno kwa neno.  Niliwaomba wajiridhishe kuhusu uandishi na dhana mbalimbali.

Nilitoa mifano ya mambo yahusuyo uandishi ambayo ni vyema wayatazame.  Pia nilitoa mifano ya dhana ambazo niliwasihi wajiridhishe juu ya kufaa kwake kuwapo," alisisitiza huku akiwataka Ukawa wakubali kurejea bungeni kuendelea na mjadala wa Rasimu ya Katiba.

Wakati Rais Kikwete akiyasema hayo, Ukawa kwa upande wao wamesisitiza kuwa hawatarajii kama kutatokea muujiza wa kuwafanya wao kurejea katika Bunge hilo kwa kuwa mpaka sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado hawajaonyesha dalili za kubadilisha msimamo wao wa muundo wa serikali mbili badala ya maoni yaliyotolewa na wananchi ya serikali tatu yaliyomo kwenye rasimu ya katiba.

Akisoma tamko la Ukawa mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaama jana kuhusu wito wa viongozi wa dini wa kuwataka kurudi katika Bunge hilo, Mwenyekiti Mwenza wa Umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema mpaka sasa hakuna dalili yoyote ya wao kurudi kwa sababu hawajahakikishiwa madai yao.

Profesa Lipumba alisema hawatarajii kama kutatokea muujiza wa kuwafanya wao kurejea katika Bunge hilo kwa kuwa mpaka sasa CCM bado hawajaonyesha dalili za kubadilisha msimamo wao wa muundo wa serikali mbili badala ya maoni yaliyotolewa na wananchi ya serikali tatu yaliyomo kwenye rasimu ya katiba.

Alisema Ukawa wanawashangaa viongozi wa dini kwa kuwataka warejee katika Bunge hilo wakati hawajawahi kuwaita wakazungumza nao ili kufahamu sababu za msingi zinazowafanya wakatae kurudi bungeni.

Profesa Lipumba alisema viongozi wa dini wamekuwa wakikaa na viongozi wa serikali, lakini hakuna hata siku moja wamewahi kuwaita Ukawa na kuzungumza nao.

Alisema badala yake viongozi wa dini wamekuwa wakisimama katika majukwaa tofauti kuwataka Ukawa warejee bungeni bila kufahamu sababu za msingi za wao kukataa kurudi bungeni.

Profesa Lipumba alisema Ukawa wanaheshimu wito wa viongozi wa dini, lakini ni vema wangekuwa wamezungumza na pande zote mbili wafahamu sababu zinazowafanya wakatae kurudi bungeni, badala ya kuishia kuzungumza na upande mmoja na kutoa matamko.

“Sababu ya msingi iliyotutoa bungeni ni mkakati uliokuwa ukitekelezwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa CCM kupuuza maoni ya wananchi waliyokusanya na kuratibiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo inapendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu,” alisema Profesa Lipumba.

Aliongeza: “CCM wameukana na badala yake wanataka muundo wa serikali mbili, ambao haujapendekezwa na wananchi walio wengi."

“Kwa sababu muundo wa muungano ndiyo moyo wa rasimu ya katiba, hivyo ukiunyonga hautakuwa na Rasimu ya Katiba inayotokana na maoni ya wananchi. Ukawa tunatetea maoni ya wananchi yaheshimiwe na ndiyo njia bora ya kutufanya turidhiane. Bunge Maalumu la Katiba halina uwezo na kibali cha kuvunja misingi mikuu ya maoni ya wananchi na kazi ya tume.”

Pia alikumbusha kuwa Ukawa walikwazwa na lugha za ubaguzi, uchochezi, matusi na kejeli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wajumbe wa CCM ndani na nje ya Bunge hilo.

Alisema lugha hizo pia zilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Profesa Lipumba alisema viongozi wa dini ni watu wenye nafasi ya kipekee katika jamii kwa kuwa wamepewa wajibu wa kuongoza watu hapa duniani, hivyo wanaheshimu miito yao.

Hata hivyo, aliwataka kutambua kuwa sababu ya wao kutoka bungeni ni kutokana na kuwapo kwa njama za kuhujumu mchakato wa katiba ikiwa ni pamoja na viongozi wa serikali kuingilia mchakato huo kwa kutoa kauli za kejeli na uchochezi.
Alisema licha ya viongozi wa dini kutoa kauli hizo, hawajawahi kuwaomba radhi, badala yake wanaendelea kutoa kauli hizo na hakuna kiongozi wa dini wa kukemea.

“Tunaamini viongozi wetu wa kiroho wanao uwezo wa kuangalia pande zote mbili na kutoa miito yenye ukweli, usawa na haki. Tunawasihi  kabla ya kututaka kurejea bungeni  wangetumia busara hiyo hiyo kutusikiliza na sisi kama, ambavyo wanasikiliza viongozi wa CCM. Hatujawasikia wakitoa wito kwa wabunge wa chama hicho wala kumkemea  waziri mkuu na Lukuvi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema leo watakuwa na kikao na Msajili wa Vyama vya Siasa na kwamba, muafaka wa wao kujerea bungeni au kutorejea utajulikana, lakini hawategemei kutokea kwa muujiza katika kikao hicho.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema dalili inavyoonyesha mpaka sasa hakuna uwezekano wa wao kurudi bungeni kwa kuwa misimamo ya uchakachuaji wa rasimu haijabadilika.

Naye Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, pia aliunga mkono msimamo huo kwa kusema hawatakuwa tayari kurudi bungeni kama katika kikao cha leo CCM hawatakubali kujadili rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Mbowe alisema dalili ya kutokuwa na nia njema ya kufikia maridhiano pia imeonyeshwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta, kwa kutoa matamko akisema hata Ukawa wasiporejea, Bunge litaendelea.

Alisema kauli hiyo inaonyesha yeye kama kiongozi wa Bunge hilo ameonyesha udhaifu wa kutokuwa na nia ya kufikia maridhiano tena kipindi, ambacho mazungumzo kati ya CCM na Ukawa bado yanaendelea.

Ukawa wameendelea kutoa msimamo huo wakati tayari Bunge hilo likiwa limekwishaitishwa kuendelea na vikao vyake Agosti 5, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya kuwaita wajumbe iliyotolewa juzi na Ofisi ya Katibu wa Bunge hilo, wajumbe wote wanatakiwa kuwasili mjini Dodoma, kuanzia keshokutwa kwa ajili ya kuanza mkutano huo kama ilivyopangwa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Agosti 4, mwaka huu, itakuwa siku maalumu kwa ajili ya mambo ya kiutawala na kwamba, wajumbe wote wanapaswa kufika ofisi za Bunge, majira ya saa 4:00 asubuhi.

Bunge hilo lililoanza Februari 18, mwaka huu, lilitumia takriban siku 21 za mwanzo kujadili na kupitisha kanuni za kuliongoza, ikiwamo kuunda kamati 16, kati ya hizo, 12 za kujadili sura za Rasimu ya Katiba.

Kamati hizo zilijichimbia katika kumbi mbalimbali mjini Dodoma na kujadili sura ya kwanza na ya sita, huku mjadala mzito uliosababisha Bunge kuingia kwenye mvutano mkubwa ni sura ya sita inayozungumzia muundo wa Muungano.

Kundi la wajumbe wengi, wakiongozwa na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatetea muundo wa sasa wa serikali mbili uendelee kwa maelezo kuwa ndiyo utakaodumisha Muungano.

Kundi la Ukawa linaloundwa na vyama vya upinzani, vikiwamo Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na baadhi ya vyama vidogo lilisimamia serikali tatu kwa hoja kwamba, rasimu ilipendekeza serikali tatu kutokana na maoni ya wananchi.

Aidha, baada ya kamati hizo kumaliza kazi na kurudi kama Bunge Maalumu, wenyeviti wa kamati hizo waliwasilisha taarifa ya wengi, huku wengine wakiwasilisha ya wachache.

Hata hivyo, mjadala huo ulijikita katika kurushiana vijembe, maneno yasiyo na staha, matusi, kudhihaki waasisi, kumshambulia Jaji Warioba kwamba alichakachua takwimu na kupendekeza serikali tatu kwa maslahi yake binafsi.

Hata hivyo, wakati mjadala wa sura hizo ukiwa katikati, kundi la wajumbe wanaounda Ukawa walitoka nje ya ukumbi Aprili 16, mwaka huu, kususia mchakato huo kwa madai kwamba, CCM imeliteka Bunge na mjadala huo kutokana na kufuta mapendekezo ya tume ya sura hizo mbili na kupenyeza rasimu yake.

Hadi Bunge hilo linaahirishwa, ngwe yake ya kwanza Aprili 25, mwaka huu, wajumbe wa Ukawa walikuwa nje ya Bunge kwa takriban siku tisa, huku wakianza kuzunguka maeneo kadhaa ya nchi kuwaeleza wananchi juu ya mwenendo wa Bunge kupitia mikutano ya hadhara.

Bunge hilo liliahirishwa kupisha Bunge la Bajeti, Mei, mwaka huu na litaendelea tena Agosti 5, mwaka huu kwa siku 60 zilizoongezwa na Rais Kikwete.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa