Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa kamati namba nne, Christopher Ole Sendeka
Akizungumza mjini Dodoma jana, Katibu wa Bunge Maalum, Yahya Khamis
Hamad, alisema kikao cha Kamati ya Uongozi kilichoitishwa jana
kilishindwa kujadili taarifa ya kamati hiyo ndogo baada ya kutokuwamo
kwa taarifa inayohusu Mahakama ya Kadhi.
“Kamati ndogo ilipewa jukumu la kuangalia suala Mahakama ya Kadhi,
uraia pacha na muundo wa Bunge, hata hivyo jana walipowasilisha walitoa
taarifa pungufu na kusababisha wajumbe kuwarudisha wakamilishe,” alisema
Hamad.
Alisema katika taarifa yao, kitu kilichoonekana kufanyiwa kazi kwa ukamilifu ni muundo wa Bunge pekee.
Hamad alieleza kwamba, kamati hiyo imepewa muda hadi Jumatatu ijayo
iwe imekamilisha kazi hiyo na taarifa yao iwasilishwe Kamati ya Uongozi
kwa ajili ya kufanyiwa kazi kabla ya kuanza vikao vya Bunge hilo
Jumanne ya wiki ijayo.
Kamati 10 kati ya 12 za Bunge Maalum la Katiba kwa muda wa siku 15
zilikuwa zikijadili sura mbalimbali za Rasimu ya Katiba na kazi hiyo
ilihitimishwa juzi.
Kwa sasa kazi inayofanyika ni wenyeviti wa kamati hizo kuwasilisha
taarifa za mijadala hiyo kwa Kamati ya Uandishi, ambayo itaziandaa na
kuziweka katika utaratibu wa maoni ya walio wengi na ya wachache, ambayo
yatawasilishwa ndani ya Bunge zima Septemba 2, mwaka huu kwa ajili ya
kusomwa na kuanza mjadala wa Bunge zima.
Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge jana,
baadhi ya wenyeviti wa Kamati za Bunge Maalum, walisema wanatarajia kuwa
masuala yaliyoleta mvutano mkubwa ndani ya mijadala ya kamati,
yataendelea kutuletea mvutano mkali kwenye mjadala wa Bunge zima.
Mwenyekiti wa kamati namba nne, Christopher Ole Sendeka, alisema
pamoja na mivutano huyo kamati yake ilimaliza kujadili rasimu na
kukubaliana kupitisha kwa baadhi ya vifungu kwa kupiga kura.
“Kulikuwa na mjadala mkali katika masuala muhimu kama ardhi, haki
za wakulima na wafugaji uraia pacha na muundo wa Bunge,” alisema
Sendeka.
Hata hivyo, Sendeka alifafanua kwamba kwa siku kadhaa hakuwapo
katika vikao vya kamati yake kutokana na kupata matatizo ya kifamilia.
“Pamoja na kuwa nje ya kamati, nashukuru wenzangu walijadili haya na kukubaliana kwa pamoja,” aliongeza.
Akizungumzia kuhusu kamati namba tatu, Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Dk. Francis Kasabubu, alitetea misuguano iliyoibuka katika kamati yake
kwamba ni jambo zuri katika kupatikana kwa Katiba mpya.
“Kunapotokea misuguano na kupingana kwa wajumbe ni dalili nzuri,
tofauti za kimtazamo inaleta afya hasa katika kazi ya kuandaa katiba
mpya,” alisema.
Alisema kwa upande wa kamati yake, kuliibuka hali hiyo lakini
walijaribu kuzungumza na mwishowe walipitisha mapendekezo yao yote.
Mwenyekiti wa kamati namba moja, Ummy Mwalimu, alisema kitu ambacho
walipata nacho shida na kukosa ufumbuzi hadi jana ni suala la mfuko wa
fedha wa pamoja.
“Tulikubaliana kwa pamoja kuweka pembeni suala hilo hadi tupate
ufafanuzi wa kitaalamu kutoka Wizara za Fedha upande wa Tanzania Bara na
upande wa Zanzibar, jambo la kufurahisha tulijadiliana vizuri na ibara
zote tumezipitia na kufanya maboresho pale inapotakiwa,” alisema
Mwalimu.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment