Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Vigogo hao wa fedha jana walikutana na baadhi ya
wajumbe wa Bunge Maalumu, kujaribu kupata mwafaka wa jinsi suala hilo
litakavyowekwa kwenye Katiba Mpya.
Bunge la Katiba limelazimika kuwaita Dodoma
watendaji hao ili kusaidia kukwamua mgogoro wa mapato ya muungano, ambao
uliwagawa wajumbe wa kamati za Bunge hilo wakati wa mjadala wa sura ya
14 kwenye Rasimu ya Katiba.
Pamoja na Profesa Ndulu, wengine waliokuwapo ni
Katibu Mkuu Hazina, Dk Servacius Likwelile na mwenzake kutoka Zanzibar,
Mussa Omar ambao walikuwa na kibarua kigumu cha kupunguza ufa
uliowatenga wajumbe wa Bunge hilo katika misingi ya Ubara na Uzanzibari.
Sura ya 14 ya rasimu ndiyo inayozungumzia masuala ya mapato ya muungano na mgawanyo wake.
Suala la mgawanyo wa mapato ni moja ya mambo manne
magumu yaliyosababisha mvutano mkubwa katika kamati za Bunge hilo kiasi
cha kusababisha Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu kuunda kamati ndogo
ili kulifanyia kazi.
Kutokana na kusababisha mivutano hiyo, Kamati
Namba Moja iliamua kutolijadili kabisa suala hilo na badala yake, kuomba
uongozi wa Bunge uwalete watendaji wakuu wa masuala ya fedha ili watoe
mwongozo wa kuwawezesha wajumbe kujadili na kupata mwafaka wa jinsi
fedha zitakavyoweza kusimamiwa na kugawanywa. Mwenyekiti wa kamati hiyo
ambaye pia ni Naibu Waziri - Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu
alisema walishindwa kupigia kura sura ya 14 baada ya kuona ina utata.
“Ni kweli hatukupigia kura sura ya 14 pekee,
tuliona ina utata mkubwa ambao unahitaji ufafanuzi wa kina na bila shaka
baada ya semina ya leo (jana) tutakutana kufanya uamuzi,” alisema
Mwalimu.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Hamis Hamad
alisema: “Kamati zote zimemaliza kazi, isipokuwa Namba Moja haikupigia
kura sura ya 14 wakitaka ufafanuzi wa kitaalamu, ndiyo maana tumewaleta
wataalamu leo.”
Alisema pamoja na kupigia kura sura hiyo, lakini
hata kamati nyingine zilionekana kutoelewa vizuri sura hiyo, hivyo ujio
wa wataalamu ulilenga kuwawezesha kujadili sehemu hiyo ya Katiba wakiwa
na uelewa mpana.
Habari zinasema sura iliyojitokeza kwenye mijadala
ya kamati zote 12 ilihamia kwenye semina hiyo, ambako ufa ulidhihirika
baina ya wajumbe wa pande hizo mbili za muungano, lakini watendaji hao
kwa kushirikiana na wataalamu wengine walifanikiwa kutoa mwelekeo wenye
matumaini.
Hoja zilizojiri
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema hoja kubwa
zilizojitokeza zilihusu uwiano wa mgawanyo wa mapato, kuanzishwa kwa
tume ya pamoja ya kusimamia mapato na Zanzibar kuruhusiwa kukopa fedha
nje na katika mashirika ya kimataifa bila kupata ridhaa ya Hazina.
Hivi sasa Zanzibar inapata asilimia 4.5 ya mapato
ya muungano huku Tanzania Bara ikipata asilimia 95.5 kutokana na wingi
wa idadi ya watu na eneo lake kijiografia, suala ambalo limekuwa
likilalamikiwa kwa muda mrefu na Wazanzibari kwamba wananyonywa.
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe alinukuliwa
akizungumza katika kikao hicho kwamba kanuni ya mgawanyo wa mapato
inayotumiwa sasa ilitokana na ushauri wa kitaalamu uliotolewa na Shirika
la Fedha la Kimataifa (IMF) na kwamba unaweza kupitiwa upya ikiwa
kutakuwa na haja hiyo. Mmoja wa wajumbe kutoka Zanzibar alinukuliwa
akihoji kwa nini upande huo wa muungano ambao ni nchi kamili usipewe
asilimia 50 ya mapato yatakayopatikana katika mfuko huo.
“Katibu Mkuu (Likwelile) aliposimama kujibu
hakukataa lakini alisema kiwango cha asilimia pia kinazingatia uwekezaji
kwenye mfuko husika na kwamba kama uwekezaji ni sawa, basi hakuna shaka
kwamba hiyo asilimia 50 inawezekana,” kilisema chanzo chetu.
Kuhusu suala la mfuko wa pamoja, habari zinasema
wajumbe wengi walionekana kuwa na mwelekeo wa pamoja lakini walikosoa
kutoanzishwa kwake hadi sasa, licha ya kwamba suala hilo liliamuliwa
miaka 14 iliyopita.
Katika Kamati Namba Mbili, suala la tume ya pamoja
limeongezwa na kupewa Ibara ya 221B, huku ikipendekezwa kwamba tume ya
pamoja ya fedha iwe na wajumbe wasiozidi saba watakaoteuliwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar. Watatu
watatoka Zanzibar na wanne Tanzania Bara.
Tume hiyo, pamoja na mambo mengine inapendekezwa
iwe na jukumu la kuchambua mapato na matumizi yanayotokana au yanayohusu
utekelezaji wa mambo ya Muungano na kutoa mapendekezo kwa serikali zote
mbili kuhusu mchango na mgawo wa kila mojawapo wa serikali hizo.
Hata hivyo, ndani ya kamati kadhaa, wajumbe kutoka
Tanzania Bara walikuwa na msimamo kwamba lazima Zanzibar ipate idhini
ya Hazina kabla ya kukopa fedha nje kwani Serikali ya Muungano ndiyo
mdhamini mkuu wa mikopo hiyo.
“Hatuwezi kuruhusu Zanzibar wakope wanavyotaka,
lazima Serikali ya Muungano ijiridhishe kwamba masharti yote kuhusu
ukopaji yamezingatiwa, vinginevyo tunaweza kuiingiza nchi katika
matatizo makubwa,” kilisema chanzo kingine.
Akizungumzia kikao hicho, Mwalimu alisema semina
waliyoipata itawawezesha kufanya uamuzi sahihi watakapokuwa wakijadili
sura hiyo ya 14.
Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi alisema kuwa semina hiyo imemsaidia kwa kiasi kikubwa ingawa ilikuja kwa kuchelewa.
Kwa upande wake Mbunge wa Dimani, Abdallah Sharia Ameir alisema semina ya jana ingawa imechelewa itatoa mabadiliko makubwa
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment